NA HAJI
NASSOR, PEMBA
IKUMBUKWE
kuwa, mwaka 2010 na hasa baada ya marakebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984, ilifuta nafasi ya Waziri Kiongozi, kuwa kama mtendaji mkuu wa serikali.
Na hapo sasa, ikamtambua Makamu wa Pili wa rais kuwa ndie atakaekuwa
mtendaji mkuu wa serikali, ingawa imeongeza kiongozi mwengine anaitwaye Makamu
wa Kwanza wa rais.
Huyu mwenyewe, hutokana na kile chama kilichoshika nafasi ya pili,
kwenye chaguzi mkuu wa vyama vingi nchini, na Katiba ikimtaja kuwa atateuliwa
na rais.
Kumbe wa Zanzibar suala la kuwa na serikali ya Umoja wa Kitaifa sio
geni, wala huu mwaka 2020 sio mara ya kwanza, maana ilianza mwaka 2010.
Ingawa mwaka 2015, ilisita kidogo kwa sababu za hapa na pale, lakini
mwaka huu tena, chini ya rais wa Zanzibar wa awamu ya nane Dk. Hussein Ali
Mwinyi akitokea chama cha Mapinduzi ‘CCM’ imerudi tena.
Na kwasasa, (marehemu) Makamu huyo wa Kwanza wa rais ni yule yule
aliyeanza mwaka 2010, ingawa kwa sasa akihudumu ndani ya chama cha siasa cha
ACT-Wazalendo.
Zanzibar imekuwa ikitofautisha na mataifa kadhaa ya Afrika kama vile
Burundi, kwamba zinapotokezea hitilafu za ndani yenyewe, hukaa chini na kutatua
jambo hilo.
Na ndio maana, kwa sasa ndani ya serikali ya Umoja wa Kitaifa ‘SUK’ na
hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, viongozi wetu wapendwa Maalim Seif
Sharif Hamad na Dk. Hussein Ali Mwinyi sasa wanafanya kazi pamoja.
Wote wakati wa kunadi sera zao, walishaawahidi wananchi wa Zanzibar kuwa,
watahakikisha wanawaunganisha wazanzibari wote, kwa kuwaweka pamoja kwa upendo,
ili kuchapuza maendeleo.
Nakumbuka sana mwezi Oktoba mwaka 2020, wakati alipokuwa mgombea wa
urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi, uwanja wa Gando
Wete, aliahidi kuwaunganisha wazanzibari.
“Kama mkinichagua kuwa rais wa Zanzibar, pamoja na mambo kadhaa, pia
nawaahidi kuwaunganisha wazazibari, ili kuona tunakuwa kitu kimoja na neema
tuitumie wote,’’alisema Dk. Mwinyi.
Akaenda mabali zaidi, akisema mshikamano wa wazanzibari ndio jambo la
mwanzo, maana wanapotengana inakuwa vigumu hata kuwatumikia, kwa kuwaletea
maendeleo.
Maneno kama haya, pia yalitamkwa na aliyekuwa mgombea wa urais wa
Zanzibar marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, wakati
akiwa kwenye uwanja wa mkutano Ditia Wawi Chake chake.
“Kwanza, mkinichagua nitahakikisha umoja, mshikamano, maridhiano ya
wazanzibari ndio jambo la kwanza, na ndio kipaumbele changu kama
mkinichagua,’’alisema wakati huo Maalim.
Akafafanua kuwa, wazanzibari ni watu wastaarabu, wapenda umoja,
mshikamano na hawapendi kugawanywa, wala kuishi kwa chuki hivyo nae azma yake
ni kuwaleta pamoja.
Haya ya viongozi wetu wapendwa, yamedhihirika Disemba 8, mwaka jana,
kwenye hafla ya kuapishwa kwa Makamu wa Kwanza wa rais Zanzibar, Maalim Seif
Sharif Hamad ambae sasa ameshatangulia mbele ya haki.
Ambae aliweka mbele maslahi ya taifa na kuwaangalia wazanzibari wote
waliopo nje na ndani, na kukubali kwa moyo mkunjufu, kuwa sehemu ya serikali ya
Umoja wa wa Kitaifa Zanzibar ‘SUK’.
Wazee wa zamani wana msemo wao kuwa, waungwana wawili daima
hawapoteani, na wengine wakasema chanda chema huvishwa pete, hapa utaona Dk.
Mwinyi na Maalim Seif ni waungwana wawili waliopoteana na kisha kuonana.
Sasa Zanzibar kuanzia Disemba 8 ya mwaka 2020, inaendeshwa kwa mfumo
wa serikali ya pamoja, kwa lengo la kuchapuza maendeleo ya wazanzibari wenyewe.
Na ndio maana marehemu Maalim Seif amesema dhamira ya yeye na
Rais wa Zanzibar, Dk. Husein Ali Mwinyi kufanya kazi kwa pamoja ni kuondoa yale
madhaifu yote, ambayo hupelekea wazanzibari kutofautiana na kuleta chuki
miongoni mwao.
Anasema, kuwepo kwa Serikali yenye
muundo wa umoja wa kitaifa, ni njia moja ya kubaini sababu ya kupata dawa
kulinda tena Zanzibar isirejee katika migogoro isio ya lazima.
VYOMBO VYA HABARI VINAFANYAJE KULINDA AMANI NA
MARIDHIANO NA MIGOGORO?
Kwa Pemba, waandishi wa habari kuanzia
mwaka 2002 waliamua kuanzisha Klabu yao, inayojulikana kwa jina la Klabu ya
waandishi wa Habari Pemba PPC.
Ambapo pamoja na mambo mengine ni
kutaka kuwajengea uwezo waandishi wa habari, waandaji wa makala ili kuripoti
habari zilizoshiba.
Ndio maana hata hivi karibuni PPC
katika kufanikisha hilo, ilishirikiana na Shirika la Internews na kuandaa
mkutano wa kuwajengea uwezo waandishi namna bora ya kuandika habari za amani na
maridhiano.
Mkutano huo wa siku moja, ambao
ulifunguliwa na Mwenyekiti wake Bakari Mussa Juma, na kufanyika Chake Chake,
aliwaambia waandishi kuwa unalengo la kuwajengea uwezo.
“Mkutano kama huu sio wa mwanzo wa
kuwajengea uwezo nyinyi waandishi na lazima nilishukuru Shirika la Internews
kwa kukubali kushirikian na sisi,’’anasema.
Mwandishi mkongwe Khatib Juma Mjaja,
ndie aliwakumbusha mbinu waandishi hao, namna bora ya kuandika habari za
maridhiano na amani.
“Tusitumie maneno ya kejeli, dharau, kukebehi
tunapoandia habari, makala na utengenezaji vipindi kwani maridhiano yaliofikiwa
Zanzibar yameangalia maslahi mapana ya nchi,’’alisema.
Moja kati ya eneo linalotegemewa mno na
kila ili kufikisha ujumbe wa kwa haraka ni kwenye vyombo vya habari, kwa kule
sauti na upeo wao kufika mbali tena kwa haraka.
Wapo wanaoamini kuwa chombo cha habari ni kama kisu au panga, kikitumika
vibaya kinaweza kuwa janga na kusababisha taharuki, ingawa kikiwa kizuri huwa
furaha na upendo kwa wote.
Hapa Meneja wa redio Jamii Micheweni Ali Massoud Kombo, anasema katika
kuhakikisha wanayaenzi, kuyalinda maridhaino sambamba na kutunza amani na
utulivu, wanaandaa vipindi mbali mbali.
Anasema, wao kama redio ya kijamii wamevutiwa na kupendezewa mno, na
namna ya uwepo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, akiamini ndio
suluhisho kwa maendeleo ya kweli.
Anasema, wameanzisha kipindi chao ambacho huwa kizungumzia umuhimu na
faida za maraidhiano kwa wazanzibari, sambamba na utunzaji wa amani kama chachu
ya kufikia maendeleo hapa Zanzibar.
Kipindic hao huruka hewani kila wiki mara mbili, (Ijumaa na Jumatatu),
ambapo jina la kipindi hicho ni ’itunze amani yako’ ambapo huwa baina ya dakika
30 hadi 45.
Anasema hutegemeana na aina ya wasemaji, ambapo kwa mfano kama wiki
iliyopita, walikwenda hewani hadi dakika 55, walipoweka mada ya ‘umuhimuwa maridhiano’.
“Sisi tunazungumzia amani na maridhiano kwenye kipindi hicho, maana
kilichofanywa na viongozi wetu ni jambo jema na hasa kwa maslahi ya
wazanzibari,’’anasema.
Hapa anawakaribisha wanaharakati, wanasiasa, wanasheria na jamii yote
kuzitumia dakika 45, bila ya malipo kuzungumza na jamii ya Micheweni, juu ya
umuhimu wa kutunza na kuyaenzi maridhiano.
Pamoja na vipindi hivyo maalum, Meneja huyo wa redio Jamii Micheweni,
anasema wamekua wakiandika habari za umuhimuwa maridhiano na nafasi jamii
katika kuendeleza hilo na amani kwa ujumla.
Lakini sio redio Jamii Micheweni pekee, wanaoendesha vipindi vya aina
hiyo, lakini kwa mujibu wa mtengenezaji vipindi wa kituo cha redio cha Istqama
Othman Ali Juma, nao wanaendesha vipindi vya aina hiyo.
Anabainisha kuwa, kila siku wanamkusanyiko wa matukio kupitia jina la
kipindi baraza ya ‘V.I.P’ ambapo ndani yake huelezea faida za kutunza amani na
utulivu.
Wameamua pia kuelezea maridhiano kwa mfumo wa kuwaacha wasikilizaji
wakipiga simu ‘live’, ili kuhakikisha wanatoa maoni yao, ingawa wote wanaonesha
kuridhishwa na maridhiano hayo.
“Inaonekana wananchi kwa kule kuzingatia maslahi mapana ya Zanzibar,
wanaunga mkono serikali ya Umoja wa Kitaifa wakiamini ndio msingi mkuu wa
maendeleo,’’anasema.
Kaimu Meneja wa Redio Jamii Mkoani, Said Omar Said, anasema kwa muda
mrefu ndani ya kituo chake, wanaendesha kipindi cha utawala bora, ambapo
hukusanya mambo kadhaa yakiwemo amani na utulivu.
“Sasa baada ya kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa Zanzibar, na sisi
tumebadilisha mwelekeo, hivyo kila Jumanne huwa tunadakika kati ya dakika 30
hadi 45 tukigusia maridhiano,’’anasema.
Akiongeza kuwa, mfumo wa kipindi hicho huwa kwa mfumo wa kurikodi na
wakati mwengine kwenda mubashara ‘live’ ili kuwapa nafasi wasikilizaji kutoa
maoni yao.
“Wengi wa wasikilizaji wetu wanaonesha wamevutiwa mno na Malim Seif,
kukubali kuingia kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa, ingawa wakiomba mamlaka
husika kusimamia hilo,’’anasema.
Amesema wataendelea kutengeneza vipindi vya kuhamasisha jamii
maridhiano hayo, kwa vile ndio mwarubaini wa kuwa na siasa za ustaarabu na
kuvumiliana.
Juma Mussa Juma, anatengeneza kipindi cha sauti ya amani kupitia
Shirika la Utangazaji Zanzibar ‘ZBC’, ambapo anasema hukusanya makundi mbali
mbali.
Kwa mfano wiki iliyopita, aliendesha kipindi na vijana juu ya kujadili
nafasi yao, katika kuitunza, kuiendeleza na kuiheshimu amani iliyopo Zanzibar.
Changamoto ambayo ipo masikioni kwa vijana, awali walidhani kua suala
la amani na utulivu kwa ajili ya kipindi cha siasa, na mwanzo walikuwa woga
kuzungumza baadae walielewe.
“Kwa sasa, najitayarisha kuongeza suala la maridhiano ndani ya kipindi
hiki, ili kuzungumza na makundi mbali mbali juu ya umuhimu na faida za
maridhiano yaliopo Zanzibar,’’anasema.
NINI
KIFANYIKE KUENDELEZA MARIDHIANO, AMANI ZANZIBAR?
Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar Harusi Miraji
Mpatani, wakati akfungua mafunzo kwa waandishi wa habari kupitia mradi wa Jenga
amani Yetu, alisisitiza haja ya kuridhiana.
“Migogoro huzaliwa baada ya jamii kutopenda kuridhiana, ambapo sasa
hata viongozi wetu wakuu wameona ipo haja hilo kufanyika,’’alieleza.
Hata mradi wa jenga amani yetu, ni eneo moja la kuona makundi ya jamii
yanapata uwelewa na sasa kufungua ukursa mpya.
Wapo wanaoona kuwa, elimu kwa jamii inahitaji kwani, bado wapo
wanaodhani kuwa, suala la kuendeleza maridhiano ni jambo la kisiasa na sio
utamaduni.
Haji Khamis Mussa wa Wawi, anasema elimu ya kuitambua vyema serikali
ya Umoja wa Kitaifa, isambaazwe hasa kwao vijana, ili iwe rahisi kuwafahamisha
wengine.
Ingawa hivi karibuni, Mufti Mkuu wa Zanzibar sheikh Saleh Omar Kaabi,
wakati akifungua kongamano la viongozi wa dini ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Wawi,
alisema utamaduni wa maridhiano, upo wa asili.
Alibainisha kuwa, utamaduni wa wazanzibari tokea asili, walijengeka
kwa kuvumiliana, kusameheana, kupendana, kukosoana na kuridhiana, ili jambo
fulani liende mbele.
Mwisho
Comments
Post a Comment