NA HAJI NASSOR, PEMBA
JAMII nchini, imeshauriwa kutengeneza
mazingira rafiki sasa ikiwemo utoaji wa huduma kwa nusu gharama, ili ndugu na
jamaa zao watakapofikia umri wa uzee, iwe rahisi kuyatumia mazingira hayo, bila
ya vikwazo.
Ushauri huyo
umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, alipokuwa
akizungumza na wanajumuia ya Wazee na wastaafua Zanzibar ‘JUWAZA’ kwenye
mkutano wa mashauriano wa utekelezaji wa haki za wazee na wastaafu, uliofanyika
Chakechake.
Alisema, hivi
sasa kila mmoja hajaona umuhimu wa kuweka mazingira hayo rafiki na ya kudumu,
kwa ajili ya wazee waliopo sasa, hadi hapo umri utakapofika na kuanza kukumbana
na changamoto.
Alieleza
kuwa, kila mmoja na kwa nafasi yake, awe serikalini au tasisi binafsi, anapaswa
kutengeneza mazingira sasa, ili akifikia uzee, apunguze vikwazo kwenye shughuli
zake.
“Kwa mfano
hata hospitali zetu, zianze sasa kuweka madirisha maalum kwa ajili ya wazee,
wenye vyombo vya usafiri waanze na nusu nauli, au kuondoa foleni kwa wazee
kwenye misururu ya kupiga kura,’’alipendeleza.
Katika hatua
nyingine, Mkuu huyo wa wilaya alisema, kwa upande wake serikali, imekuwa
ikijitahidi kuweka mikakati ya kuwasaidia wazee hao, ikiwa ni pamoja na
pencheni jamii.
“Ndio maana
hata sasa kunamchakato unaendelea kuona wanaonufaika na pencheni jamii ya shilingi
20,000 kila mwezi sio lazima utimize miaka 70 hata kati ya 65 na 60, iwe wote
wananufaika,’’alieleza.
Hata hivyo
alipendekeza kuwa, wakati umefika sasa kwa wazee wa Zanzibar, kuwa na nafasi
maalum ya uteuzi ndani baraza la wawakilishi, ili waelezee changamoto zao.
Katibu wa ‘JUWAZA’ Ghanima Othman Juma, alisema wanataka wapewe kipaumbele kila eneo, kuanzia ngazi ya shehia, jimbo, wilaya mkoa na taifa.
“Kwa mfano, tunapofika kipindi cha kwenda kwenye uchaguzi, tushirikishwe, utungaji wa sera mbali mbali, uandaaji wa bajeti ya nchi na hata suala la uteuzi wa miradi,’’alipendekeza.
Nae Mjumbe wa Kamati tendaji wa ‘JUWAZA’ Amina Shaaban, alisema wamekuwa wakiwafuata viongozi kadhaa, ili kuona wazee wanakuwa na ahuweni ya maisha.
“Hivi sasa, tumeshapanga kuonana na Makamu wa Kwanza wa rais Zanzibar, kunachangamoto tunataka kumfikishia, maana hata hili suala la pencheni jamii inayotolewa sasa, ni juhudi za JUWAZA,’’alieleza.
Akiwasilisha
mada kwenye mkutano huo, mtoa mada Omar Mohamed Ali, alisema wazee wanamchango
mkubwa kwa taifa, hasa kwa uwelewa wao.
Wakichangia
mada kadhaa, wazee hao akiwemo Daud Ali Hamad kutoka Konde, alisema bado kuna
changamoto kwenye ulipaji wa fedha za pencheni jamii, kwa kupewa wengine ambao
hawajatimiza miaka 70.
Mzee Omar
Ali Khamis alisema, Mfuko wa Hifadhi wa Jamii Zanzibar ‘ZSSF’ haujawatendea
haki wa kukosa kuwaongezea pencheni yao, licha ya kulitumikia taifa kwa muda
mrefu.
“Hata ‘ZECO’
na ‘ZAWA’ kwenye huduma zao hawajawajali wazee, iwe kwenye malipo au kuingiwa
huduma, kunauzembe unafanyika,’’alieleza.
Sensa
iliyofanyika ya watu na maakazi ya mwaka 2012, ilionesha Zanzibar kuna wazee
wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wapatao 58,311 wanawake 28,424 na wanaume
29,887.
Eneo jengine
imeonesha kuwa, falimia 17 kati ya 100 zilizopo Zanzibar zinaongozwa na wazee,
huku wazee 60 kila 100 imegungulika hawapati mapato ya kujikimu.
Mwisho
Comments
Post a Comment