NA HAJI NASSOR,
PEMBA
…..hii sio mara
ya kwanza, kwa gwiji wa siasa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa Makamu wa
Kwanza wa rais ndani ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kabla ya kufutwa matokeo ya
uchaguzi mkuu wa 2015, Maalim Seif, kwa wakati huo akihudumu na Chama cha
Wananchi CUF, alishika nafasi hiyo kutoka 2010 hadi 2015.
Wakati huo Dk. Ali Mohammed
Shein wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwa Rais wa awamu ya saba, akipokea
kijiti hicho kutoka kwa muasisi wa maridhiono hayo Amani Abeid Karume.
Maalim, ameamua kurudi tena
kuwa Makamu wa Kwanza, kwa sasa akiwa pamoja na rais wa awamu ya nane, wa
Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Kwa ustaarabu, uvumilivu,
ukongwe wa kisiasa na kuweka mbele zaidi maslahi mapana ya wazanzibari, ndio
maana Disemba 8, mwaka 2020, Zanzibar ilizaliwa tena upya.
Upya wake, unakuja maana
licha ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kuanzia mwaka 2010 kutaka kuwepo kwa
serikali ya Umaja wa Kitaifa, ‘SUK’ lakini hitilafu za hapa na pale mwaka 2015 ‘SUK’
haikuwepo.
Leo hii tukiwa ndani ya ‘SUK’
ni furaha na mbwembwe za wazanzibari, kwa kule viongozi wetu wakiamua
kufanyakazi pamoja tena bila ya kujali vyama vyao, kwa hakika hili ni jambo
jema mno.
Hapa sasa tunajufunza kuwa, Dk.
Mwinyi ameshapandisha tanga la safari ya kuiongoza Zanzibar chini ya muundo wa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ‘SUK’ ukiwa unaendelea.
Ni punde tu, tangu taifa hilo lenye mamlaka ya
ndani, kutoka katika uchaguzi mkuu, uliomazika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka
2020.
Historia ya Umoja wa Kitaifa
Siasa za Zanzibar,
daima huanza na moto mkubwa wa ushindani wa kisiasa na kisha kumalizika kwa
maridhiano na maelewano makubwa.
Ndio maana, wazee walishasema
wagombana nao ndio wapatanao, maana kwa Zanzibar kupatana ni pahala pake, kwa
kule wananchi wake walivyoshiba demokrasia ya kwli.
Kumbe hata kabla ya
Mapinduzi ya 1964, Zanzibar chaguzi zake zilikuwa za ushindani mkubwa, ambapo
kisha baada ya kurudishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi 1992 ushindani wa
kisiasa, ukarudi kama awali.
Kwa wazanzibari, kama
walivyo watu wa mataifa mengine, nao hukosana hapa na pale, ingawa wao
hawawatumii wasuluhisi kutoka nje, bali wenyewe tu, basi na mwafaka hupatikana.
Moja ya jambo kubwa
lililoafikiwa ni kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, huku lengo
kuu likiwa ni kuwaleta pamoja wazanzibari, ili waijenge nchi yao.
Ndio maana, hata Makamu wa Kwanza wa rais wa
Zanzibar, Jemedari Maalim Seif Sharif Hamad, akasema kilichowasukuma kukubali
kushirikiana na serikali, ni kuwaleta pamoja wananchi na sio chengine.
“Leo tumeshafungua
ukurasa mpya wa umoja, mshikamano, maelewano kwa wazanzibari sote, bila ya
kujali vyama vyetu vya ACT, CCM wala CHADEMA kilichopo mbele yetu ni kuwaleta
pamoja wazanzibari,’’alisema Makamu wa Kwanza hivi karibuni.
Kila mmoja ni shahidi
kuwa, uchaguzi mkuu wa vyama vingi ule wa mwaka 2010, na 2015 na huu wa 2020
ulifanyika kwa amani kubwa tena bila fujo lolote, kwa kule viongozi wakuu
kufahamiana.
Uteuzi wa Maalim Seif
umepokewa vipi?
Vijana wa kisiwa cha Pemba,
wanasema kwanza ni jambo jema na zuri, kwa mkongwe huyo wa siasa kukubali
kuingia ndani ya serikali ya Umoja wa Kitaifa ‘SUK’.
Wanasema kauli za Rais
wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza, Makamu wa pili katika kuendeleza mbele Zanzibar,
lazima zienziwe na zitunzwe kwa vitendo na kila mmoja.
Omar Khamis Haji miaka
26 wa Mtambile anasema, wameyapokea vyema maridhiano hayo, na sasa kilichobakia
ni kwa kila mmoja, na kwa nafasi yake ayatekeleze kwa vitendo.
Kama alivyo Omar, na
hata Khamis Muhidini Juma 30 na Fauzia Kheir Hassan miaka 21 wa Kipapo, wanasema
kilichobakia wao kama vijana, ni kuhamasishana ili kuendeleza mbele maridhiano
hayo.
Hata Mohamed Khamis
Juma miaka 34 wa Wete Limbani, anasema, maendeleo ya vijana hayatopatikana,
ikiwa nchi haina maridhiano miongoni mwao.
“Sisi tunawategemea
viongozi wetu, watusafishie njia za kutimiza ndoto zetu, sasa kama hakuna
maridhiano, umoja na mshikamano ni vigumu kusimama,’’anasema.
Hata Siti Mohamed Omar
wakati akizungumza kwenye kongamano la amani lililofanyika Wesha hivi karibuni,
alisema wameridhishwa mno na uwepo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Hii ni ishara kubwa
kuwa, sasa ile Zanzibar yenye neema itafika pahala pake, maana matakwa ya
Kikatib ya uwepo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa yameshafanyika,’’anasema.
Mwenyekiti wa Jumuiya
sauti ya Vijana Pemba Said Mussa Rashid, anasema vijana wako wazi kuona
maridhiano hayo yanafanyiwa kazi.
Anasema,
watahamasishana kama vijana, kuona kwanza umoja, mshikamano, amani na
maridhiano hayo yanakuwa endelevu kwa maslahi mapana ya taifa.
Hivi karibuni, Naibu
Mufti Mkuu wa Zanzibar sheikh Mahamoud Mussa Wadi, akifungua kongamano la amani
kwa vijana, alisema wao wana nafasi kubwa ya kutunza amani na utulivu.
Anasema vijana ndio kundi
kubwa na lisilotabirika katika nchi yoyote, sasa lazima waelewe nafasi yao, na
kuhakikisha hawaitendei vibaya nchi yao.
“Sasa uchaguzi mkuu wa
vyama vingi umeshamalizika, na viongozi wameshapatikana na serikali ya pamoja
imeshaundwa, ni wajibu wa vijana sasa kusaka fursa,’’alieleza.
Kamanda wa Polisi mkoa
wa kusini Pemba Ahmed Khamis Makarani, anasema lazima vijana wasikubali
kutumiwa ovyo ovyo, hasa kwenye kuelekea kuyatia doa maridhiano na amani ya
Zanzibar.
Kamanda huyo,
aliwasisitiza vijana, kuwa wanapoilinda amani iliyopo, ndio mwenye kazi ya boda
boda, kilimo, afya, uvuvi na usanii ataifanya kwa ufanisi.
“Sasa uchaguzi umeshamalizika,
kila mmoja kwa nafasi yake na alipo, awe balozi mzuri wa kuilinda amani,
maridhiano na hasa hawa vijana maana ni wepesi kuharibika,’’anasema.
Kwani hata rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi,
katika hutuba zake mbali mbali amekuwa akirudia kuwa, katika mazingira ya sasa
ya siasa za Zanzibar, muundo huo wa serikali utasaidia pakubwa.
Anasema, kwani neema
ambayo aliwahidi wananchi kwenye kampeni, haitowafikia ikiwa, nchi hiyo wananchi
wake hawako kwenye mshikamano wa kijamii na utulivu wa kisiasa.
“Ndugu zangu, lazima
tuelewa kuwa, amani, maridhiano na mshikamano ndio jambo moja kubwa na la
kwanza, katika kufikia maendeleo ya kweli,’’anafafanua.
Hata Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kula kiapo kushika nafasi hiyo,
alisema hatovumiliwa yeyote, ambaye ataleta chokochoko za kuwagawa wazanzibari
na kurudisha uhasama miongoni mwao.
Amewataka wananchi visiwani
Zanzibar, kudumisha amani na umoja uliopo na kuwabeza wale wote wanaopinga
umoja uliopo nchini, ili kuipatia nchi ya Zanzibar maendeleo kwa haraka.
Amesema kuwa, kuwepo kwa Umoja na Ushirikiano
kwa wazanzibari, ni jambo muhimu katika nchi na kuwataka watu waachane na
itikadi za mambo ya kisiasa katika masuala ya kusimamia maendeleo yao.
“Kama tukiwa wamoja ni rahisi nchi yetu kupiga
hatua kimaendeleo, katika nyanja zote na kuwa mfano wa nchi nyingi za bara la Afrika,”ameeleza
Maalim Seif.
Sambamba na hilo, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais
amewataka wazanzibar, kuacha ubaguzi wa rangi au wa kisiasa, kwani mbora mbele
ya Mwenyezi Mungu ni yule mchaji zaidi.
Pia Maalim Seif, amesema dhamira ya yeye na Rais
wa Zanzibar, Dk. Husein Ali Mwinyi kufanya kazi kwa pamoja ni kuondoa yale madhaifu
yote, ambayo hupelekea wazanzibari kutofautiana na kuleta chuki miongoni mwao.
Amesema, kuwepo kwa Serikali yenye muundo wa
umoja wa kitaifa, ni njia moja ya kubaini sababu ya kupata dawa ya kuilinda
Zanzibar, isirejee tena katika migogoro isio ya lazima.
Kundi jengine ambalo limekuwa
lipewa tahadhari, ili mardhiano yasiingie doa pamoja na vijana, lakini pia waandishi
wa habari na kalamu zao.
Na ndio katika kuhakikisha
waandishi wa habari wanakuwa weledi katika kuandaa vipindi, makala na habari Kituo cha Huduma za Sheria Zanzjbar ZLSC, kwa ufadhili wa EU chini ya tasisi ya Search for Common Ground na LHRC iliendesha mfunzo ya siku kadhaa kwa waandishi w ahabari.
Kwenye mkutano huo
uliofanyika mjini Chake chake, waandishi waliohudhuria mkutano, waliahidi kuwa
wabunifu na weledi ili kuhakikisha maridhiano na amani inamea Zanzibar.
Meneja kituo cha redio cha
Zenj FM na Zenj TV, Is-haka Mohamed Rubea alipongeza hatua ya PPC na Internews
kukutana na waandishi wa habari.
Nae Khadija Mahmoud Chande
mwakilishi wa Channel Ten, alisema ukumbusho na mbinu walizopewa zimewapa
ufahamu mkubwa.
Akizungumza kwenye mkutano
huo Afisa Ufuatiliaji na tathmini wa mradi wa Jenga Amani Yetu Khamis Haroun Hamada, alisema wameamua kuwajengea uwezo
waandishi, ili waandae vipindi na makala kwa uweledi.
mwisho
Comments
Post a Comment