NA HAJI NASSO, PEMBA
ZANZIBAR ni
muunganiko wa visiwa viwili Unguja na Pemba.
Kwa miaka mingi sasa visiwa hivi vimekua vikisifiwa katika suala
uwepo wa amani ya kutosha visiwani humo.
Viongozi mbali mbali wa serikali, NGOs, mashirika na wadau
wamaendeleo wamekua mstari wa mbele kuhimiza suala la amani na utulivu, kabla
ya Uchaguzi, wakati na hata baada ya uchaguzi mkuu wa vyama vingi.
Tumekua tukizowea kuona uvunjifu wa amani hujitokeza zaidi kabla
au baada ya kipindi cha uchaguzi mkuu wa vyama vingi, nakusahau muda mwengine
na badala yake kutokea vurugu zinazoelekea kwenye mapigano.
Vipo viashiria vingi au sababu na maarufu vinavyopelekea
uvunjifu wa amani kama vile kupindwa kwa demekrasia, kucheleweshwa kwa haki,
ukosefu wa huduma za kijamii na ubaguzi.
Wengine husahau na wakati mwengine kupuuzia sababu za uwepo wa
ajira za watoto kuwa zinaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani nchini.
WAZAZI
Ali Mtwana Haji (57) ni mkaazi wa shehia ya Tumbe Magharibi, anasema ajira za watoto sio chanzo cha
uvunjifu wa amani, kama baadhi ya watu wanavyofikira.
Anasema ijapokuwa serikali inakataza ajira, bado hakujatokea mapigano au mivutano katika
maeneo watoto wanapofanyia ajira hizo.
“Mimi bado sijaona mikwaruzo yoyote bandarini kwetu, licha ya
vijana baadhi ya siku kufukuzwa na kuwekewa vikwazo,”amesema.
Anasema tatizo ni kubwa bandarini kwao, nashangazwa na mikakati
inayopangwa bandarini juu ya kuzuiliwa watoto kutokupara samaki, ilhali pesa
wanazopata wanasaidia famili zao.
Mwaka Hamadi Mbwana mzazi (45) anasema ajira sio chanzo kwani kama
inavyofiriwa, bali watoto wanachokipata hutumia na familia zao.
“Hatokua mwanangu akirudi anakuja na samaki na vijisenti kidogo,
halafu ukamfukuza unataka akatafute pesa wapi, nakazi gani wakati hii ndio kazi
nyepesi kwake,”anahoji.
Mjaka Hija Shaali (42) anasema kutokana na hali za maisha suala la
ajira kwa watoto wao ni msingi mkuu wa kuendeleza familia zao.
“Naelewa kuwa ajira kwa watoto ni marufuku kuanzia kwa sheha
hadi serikali kuu, na hua tunawakataza lakini hakujawahi kutokezea mivutano
baina yetu na watendaji wa serikali,”anasema.
Anasema mwaka 2015 watoto walipofukuzwa, baadhi ya wazazi walipinga
sana tukio hilo, huku akishutumiana na kuwekeana usahasama baina yao.
Mtumwa Rashid Kai (38) anasema ajira za utotoni chanzo cha uvunjifu wa
amani, pale watoto wanapofukuzwa bandarini na wazazi kutokukubali na kuanza
kujibizana.
“Tayari baadhi ya watu waliwawekeana uhasama na kusulushishwa,
ili mradi watoto wao kuachiwa kuendelea na kazi zao za uparaji wa samaki,”alisema.
Ramadhan Hamad Juma (55)anasema ajira sio chanzo, bali ni mtu kama
anataka kufanya matukio maovu anafanya bila ya kuwepo bandarini, kutokana na
muda mrefu vijana wanapara samaki na hatujasikia mizozo yoyote.
WATOTO
Yussuf Hija Shaame (14)mkaazi wa Tumbe kaliwa, anasema ajira za utotoni sio chanzo cha
uvunjifu wa amani, na wapo muda mrefu bila ya kuhusishwa na matukio maovu
bandarini hapo.
Amesema sisi wengi tuliopohapa kila mmoja anajuwa anachokifanya,
licha ya baadhi ya wakati madalali hutufukuza ili tuwende skuli.
“Nisipokuja hapo basi nyumbani natetwa, ati watu watakula nini
wadogo zangu, imekua ni kazi yangu ya kawaida kwa sasa ila muda wa skuli
ukifika nishaondoka,”alisema.
Yassir Shaame Pandu (17) mkaazi wa chimba, tuliwahi kufukuzwa ila baadhi ya wazazi
walituombea tukaendelea kuwepo mpaka sasa, hapa sisi wengine tunajiepusha
kuingia katika vikundi viovu huko mitaani.
“Kipindi tulipofukuzwa baadhi ya watu walitaka kupigana,
kutokana na kutuzuia sisi kisingizio hatuendi skuli wala chuoni, kazi yetu
kupara samaki tu”anasema.
Naye Chumu Ramadhan
Heri (16) muuza Visheti bandarini Tumbe, anasema kutokana na hali ngumu ya
familia yao, hanabudi kufanya biashara hiyo na fedha anazozipata zinasaidia
nyumbani kwao.
“Hutokea baadhi ya siku watoto wanafurushwa hapa, zaidi muda wa
skuli unapofika na wale wakaidi hukatazwa moja kwa moja kuwepo hapa,”amesema.
Pandu Jafar Ismail (18) anasema ajira sio chanzo cha uvunjifu wa
amani, ni mtoto mwenyewe kama ni mkorofi basi atatimiza malengo yake popote
pale na sio lazima bandarini hapa.
“Sisi tupo hapa muda mrefu wapo wanaokuja na wakiondoka fedha
zao zinaishia kwenye madawa ya kulevya na mambo mengine,”alisema.
“Wapo wanaokwenda
kutafuta pesa na kwenda kutafuta dawa za kulevya, akeshalewa chochote
atakachokifanya ni sawa kwake, ulevi ni baba wa maasi na hapo amani itaanza
kuondoka kwa wenzake,”amesema.
Anasema bandari imekua ni
kubwa, inawezekana watoto walianza wawili kipindi hiko, sasa inafika darasa
zima lakini hatujawahi kuona uvunjifu wa amani bandarini hapa.
Mariyam Suleiman Mustafa mchuuzi samaki katika soko la Machomanne,
anasema uvunjifu wa amani unatokea pale watoto wanapoondosha uwamifu katika
utengenezaji wa samaki.
“Ingekuwa wazazi wanauelewa
juu ya umuhimju wa elimu kwa watoto wao licha ya hali ngumu ya kimaisha iliyopo,
basi sizani kama wange waruhusu watoto wao kujiingiza katika biashara yoyote
katika umri mdogo kwa kisngizio tu maisha,” alisema.
WAVUVI WA SAMAKI
Juma Khamis Kambi anasema watoto wamekuwa ni wengi na hata wakikatazwa,
wazazi wao wanakuwa wakali kutokana na baadhi yao kutumwa kwa ajili ya kusaidia
familia zao.
“Ngalawa au madau yanapofika
tu, basi utawaona wanakuja na biashara zao wengine huleta madafu au mafenesi,
ili tuwapatie samaki na sisi tunafanya hivyo, wengine wanawauza baadae na
wengine wanapeleka kwao,”amesema.
Katika hatua nyengine Kombo sheha Hassan amesema watoto
waliopo wanakosa fursa zao za kielimu, kutokana na tamaa za wazazi wao kwa kitu
kidogo wanachopata nao kuona ndio kazi kwa mtoto wake.
“bandarini hapa watoto
wanaojishuhulisha na ajira ni wengi mmo na uvunjifu wa amani unaweza kuja pale
unapowakataza watoto kupara samaki, kuosha madau, kubeba ndoo za madagaa au
shazi la samaki,”anafafanua.
MADALALI WA SAMAKI BANDARINI
Abdi Khamis Juma anasema
hakuna anayefurahishwa na hali iliyopo katika bandari ya Tumbe, ila ukosefu wa
mashirikiano baina ya wazazi na madalali ndio sababu inayopelekea wimbi hilo.
“Baadhi ya Madalali wenzetu
na Wazazi hawapo tayari katika hili, sisi wengine tunapoweka mikakati basi
wengine wanaivunja na kutuona sisi wabaya,”amesema.
Anasema wapo wazazi
wanawatuma watoto wao ndio wakawa wakali katika hili na kuwa tayari kupigana
ili wasifukuzwe, hebu tizama mpaka jioni mtoto anafika shilingi 8,000 hadi shilingi 20,000 hutegemea na msimu.
Naye mkuu wa madalali bandarini hapo Mtawa
Khamis Haji, anasema watoto waliopo bandarini hakuna hata mmoja anayekwenda
skuli, huku wazazi wao wakishindwa kuwafuatilia.
MASHEHA WA SHEHIA ZA TUMBE
Kaimu sheha wa shehia ya Tumbe Mashariki Ali Omar Ali, anasema ajira
hizo zinakuwa chanzo cha uvunjifu wa amani, kutokana na ukosefu wa elimu pamoja
na umasikini kwa familia.
“Mtu akikosa elimu
anaweza kufanya lolote hata kama linaweza kuvunja amani na anacho kitizama yeye
ni maslahi yake binafsi, ndio mfano kama hawa wazazi wahaowaruhusu watoto wao
kupara samaki,”anasema.
SHEHA wa shehia ya Tumbe Magharibi Massoud Khamis Kirando, anasema
baadhi ya watoto wanaokwenda bandarini inakuwa ni maagizo kutoka kwa baadhi ya wazazi wao kama sehemu ya
kusaidia familia yao.
“Tunapowafukuza sisi
huonekana ni maduwi wakubwa kwa wazazi wa Tumbe na vijiji vya jirani, yote ni
kutokana na ukosefu wa elimu, ”amesema.
WADAU WA MAENDELEO
Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Maendeleo Tumbe(JUMATU) Nassor Suleiman Nassor, anasema ajira zinakuwa chanzo
cha uvunjifu wa amani pale usimamizi wa sheria zinapokuwa zinalegalega.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya
kupunguza Umaskini na kuboresha hali za wananchi (KUKHAWA) Hafidhi Abdi Saidi,
anasema unapomzuwia mtoto asiende kwenye ajira hizo katika umri mdogo,familia
haitambuwi wamezuiliwa kwa sababu gani.
“Ukosefu wa elimu kwa
watoto, unapelekea kuingia katika vikundi viovu ikiwemo wizi, udhalilishaji na
uuzaji ama utumiaji madawa ya kulevya mwishokupelekea familia kugombana,”amesema.
VIONGOZI WA SERIKALI
Diwani wa Wadi ya Tumbe
Ali Juma Shaibu, anasema umasikini wa familia ndio chanzo kikuu cha watoto kujiingiza
katika ajira za utotoni na wanapokatazwa wazazi wanakua wakali.
“Hakuna siku ambayo
watoto wanakua hawapo, siku zote wapo na wala hawaendi skuli, wakikatazwa
wazazi wanakuwa wakali na kupelekea uhasama na kuchukiana.
MKUU wa Wilaya ya
Micheweni Mgeni Khatib Yahya, anasema mtoto anapojiajiri akiwa mdogo anakosa
haki zake za msingi ikiwemo elimu.
Amesema kuwa ajira za
utotoni zinaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani, kutokana na wazazi wanakuwa
wabishani na viongozi wao serikali wanapokatazwa kutokuwaruhusu watoto wao
katika ajira.
“Kutokana na wazazi kuwa
wabishi juu ya suala la ajira za utotoni ndio maana watoto zaidi ya 7609
wamekatisha masomo na kundi kubwa wapo katika ajira za utotoni,”alisema.
SHERIA YA MTOTO NO:6/2011
Kwa mujibu wa sheria hiyo,
imekataza mtoto kuajiriwa kinyume na sheria kumuajiri
au kumtumia mtoto katika kazi zenye madhara.
MWISHO
Comments
Post a Comment