NA HAJI NASSOR, PEMBA
OFISI ya Mufti Zanzibar ni moja kati
ya Idara zinazomilikiwa na serikali ya Mapinduzi, ambapo miongoni mwa majukumu
yake ni kusimamia, kuratibu na kutoa uamuzi ‘fat-wa’ kwa yale mambo husika.
Ofisi hii,
katika kufanikisha shughuli zake imekuwa ni wadau wake mbali mbali, iwe ni wa
ndani au nje ya Zanzibar, ikiwa tu wadau hao, wana malengo na maazimio
yanayofanana.
Kwa mfano,
ofisi hii ya Mufti kwa upande wa kisiwani Pemba imekuwa ikifanyakazi karibu mno
na taasisi isiyo ya serikali ya ‘Marafi wa Zanzibar’ ‘Friend of Zanzibar’
pamoja na taasisi ya Interfarce.
Taasisi hizi,
zimekuwa zikifanya shughuli mbali mbali wanazoshirikiana na Ofisi ya Mufti kwa
upande wa Pemba, ili kuhakikisha, jamii ya watu wa Pemba kwa ujumla wao,
wanaishi kwa amani na maridhiano.
Friend of
Zanzibar, kuanzia tokea mwaka 2010 na Interface kuwanzia mwaka 2015, zimekuwa
bega kwa bega na ofisi hii, kwa kuwajengea uwezo wananchi, waelewe maana na
amani na maridhiano, faida zake, athari za kuikosa tena sio tu kwa ajili ya
uchaguzi mkuu, bali hata kwenye maisha ya kila siku.
Tasisi hizi,
zimekuwa zikikutana mara kwa mara na makundi mbali mbali, kama vile ya
waandishi wa habari, maimamu, masheikh, waalimu wa madrssa, makundi ya vijana
na wanawake wa kiislamu.
Aambapo yote
kwa yote, ni kuona jamii inakuwa na tabia ya kuvumilia, kusameheana,
kuhurumiana, kupendana, kusaidia na suala la kuishi kwa amani.
Ndio maana,
kwa mfano tasisi ya marafiki wa Zanzibar iliendesha mkutano wa umuhimu wa
kutunza amani na kuhimiza maridhianuo, ambao ulihusisha makundi ya vijana,
wanawake, masheikh na maimamu iliyofanyika baina ya tarehe 5 Disemba hadi 7
mwaka huu mjini Chake chake.
Mkutano huo
wa siku moja, ambao uliandaliwa na kufadhiliwa na taasisi ya ‘Marafiki wa
Zanzibar’ ulikuwa na lengo la kuwakumbusha viongozi hao, umuhimu wa amani
katika maisha ya kila siku.
Ingawa pia
uzoefu unakubali kuwa, kila unapomalizika uchaguzi mkuu suala la amani huwa
tete, hivyo mkutano huo pia ulilenga kuona amani inakuwa endelevu.
Aliyeufungua
mkutano huo, alikuwa Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar anayefanyia kazi zake
kisiwani Pemba, sheikh Mahamoud Mussa Wadi, ingawa kabla ya kufanya tukio hilo,
Kaimu Katibu wa Mufti Pemba Sheikh Said Ahmad, aliwaeleza washiriki kuwa,
mkutano huo ni ile mikutano iliyoanza kabla ya uchaguzi, kufanyika tena karibu
na uchaguzi na huo.
Sheikh Said,
amasema Ofisi ya Mufti kwa kushirikiana na taasisi ya ‘Friend of Zanzibar’
imekuwa mstari wa mbele, kuona suala la amani inakuwa ndio utamaduni wa
wananchi wote, kwa vile faidi yake hutumiwa na wote.
“Suala la
amani, utulivu, maridhiano na mshikamano sasa liwe ndio utamaduni wetu, maana
hata viongozi wetu wakuu hapa Zanzibar sasa wanafanya kazi pamoja,’alieleza.
Anasema
ikiwa kila kiongozi wa dini na kwa nafasi yake atahimiza umoja, mshikamano,
maridhiano, kusameheana, kupendana suala la kuchafuka kwa amani Zanzibar
litakuwa ndoto.
Katibu wa
taasisi ya friend of Zanzibar sheikh Abubakari Kabwogi, ambae nae alisema suala
la amani ni tunu muhimu katika nchi yoyote.
Anasema,
pamoja na changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza kabla na wakati wa uchaguzi,
lakini amani iliyopo leo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, imechangiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa
dini ya kiislamu.
Anasema
kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na viongozi hao kwa kule kuwaelimisha
wafuasi wao, ndio maana leo ambapo uchaguzi umeshamalizika kisiwa cha Pemba
kinaendelea kuwa amani.
Anawakumbusha
masheikha hao kuwa, kila jamii inakuwa na migogoro, akimaanisha ndio sehemu ya
maisha ya kila siku na wale ambao wameshafiriki ndio pekee ambao hawana tena
migogoro.
Ingawa
Katibu huyo anasema uboro wa jamii yenye migogoro kisha ni kukaa chini na kupatana,
kama ilivyofanyika kwa sasa ndani ya serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibra
‘SUK’.
Katibu huyo aliwaambia
viongozi hao, wao ndio pekee ambao wako karibu mno na waumini kuliko kiongozi
yeyete yule, kwa kule kukutana nao mara tano (5) kwa siku, kwenye nyumba za ibada.
‘Fursa ya
kukutana na waumini mara tano kwa siku, itumieni ili kuwaeleza umuhimu wa amani
na maridhiano yaliopo Zanzibar, kwani huo ndio utamaduni wa
wazanzibari,’’anasema.
Hata hivyo
amesifu kazi kubwa inayofanywa na Ofisi ya Mufti, akisema kuwa, kama kunakuwa
na vyombo ambavyo wanazionyesha kazi hizo nje ya Pemba, basi kila mmoja
engefurahia.
Sheikh
Mahamoud Mussa Wadi, wakati akifungua kongamano hilo, aliwakumbusha washiriki
kuwa, kongamano hilo ni endelevu ya mikutano inayofanywa na ofisi hiyo, ikishirikiana
na taasisi ya marafiki wa Zanzibar.
Aliwataka
viongozi hao, sasa kwa vile uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, umeshamalizika, ni
wakati wa kushirikiana na serikali iliyopo madarakani, katika kuleta maendeleo
ya taifa.
“Viongozi
wetu sasa wanafanyakazi pamoja, je sisi viongozi wa dini ya kiislamu tunafanya
nini ikiwa hatutoshirikiana nao kupata maendeleo ya kweli,’’alieleza.
Naibu huyo
anasema, kila mmoja awe muumini wa dini ya kiislamu au wa dini nyingine
anahitaji maendeleo popote alipo, sasa ili kufikia hayo, tuweke pembeni itikadi
za vyama vyetu na kushirikiana na Serikali yetu ya Umoja wa Kitaifanya kazi
nayo.
Kwenye eneo
jingine, aliongeza kuwa ubora wa mwanadamu anaekoseana na mwenzake, hupendeza
zaidi kama akiomba radhi, mashama, na anaeombwa kusahamehe ni bora.
Naibu Mufti
akazidi kusisitiza kuwa, ni vyema kwa jamii kuacha kufuata matamanio ya shetani
‘ibilisi’ kwani hupenda mno yale mazuri kuyageuza kuwa mabaya, na mabaya kuyafanya
kuwa mazuri kwa lengo la kuupoteza umma.
Kaimu Katibu
wa Ofisi ya Mufti Pemba Sheikh Said Ahmad Mohamed, kubwa anawataka viongozi wa
dini ya kiislamu kuwaeleza wafusi wao juu ya umuhimu wa kuvumiliana, kupendana,
kusamehena na kuombana msahama, ili kuhakikisha amani haichafuki tena.
Alikemea
tabia ya viongozi wa dini, wakiwemo maimamu na makhatibu kushabikia vyama,
kwani kufanya hivyo kunaweza kukawagawa wafuasi wao.
Anasema,
sasa kilichopo mbele yao hasa baada ya kuwepo kwa maridhiano ndani ya serikali
ya Umoja wa Kitaifa ‘SUK’ ni kuhubiri umoja, mshikamano, amani na utulivu.
“Hatuna budi
kuungana na viongozi wetu wa nchi, sasa wenyewe wanafanya kazi pamoja, sasa
kilichobakia kwa sisi viongozi wa dini, kuhakikisha hatuwi chanzo cha
machafuko,’’anafafanua.
Anasema, wapo wanaovitumia viriri vya msikiti
kama majukwaa ya kutoa misimamo yao, au kuonesha mapenzi juu ya chama fulani,
jambo linaloweza kusababisha mgawanyiko na kuanza kuchafuka kwa amani na kisha
kuzuka migogoro msikitini.
Mapema, sheikh
Saleh Abdull Adam wa Mkoani Pemba, aliwasisitiza wenzake, kuacha kuonesha wazi wazi
mahaba na mapenzi ya vyama vyao vya siasa kwa jamii, kwani kufanya hivyo,
kunaweza kupelekea kuwagawa wafuasi.
“Wakati huu,
sisi viongozi wa dini na masheikh lazima tujuwe kuwa wajibu wetu ni
kuwaunganisha wananachi, iwe kwa kutumia hutuba au mihadhara,’’anasema.
Lakini hata
Khamis Salum Ali wa wilaya ya Chake chake, alisema ijapokuwa sasa mfumo wa
vyama vingi unaonekana kuwa ni tatizo, lakini sio haki kwa viongozi wa dini
kuwagawa waumini.
“Kwa mfano,
mfumo huu wa vyama vingi, leo umepelekea kuwepo kwa maridhiano, umoja,
mshikamano sasa je sisi masheikh tuvuruge haya, hili sio sahihi,’’anasema.
Kwa upande
wake sheikh Juma Haji Hamad wa wilaya ya Wete, alisema, ili kuhakikisha
maradhiano yaliofikiwa Zanzibar yanadumu, ni vyema kuanzisha kamati (kikundi)
kwa viongozi na wanataaluma wote, kuanzia ngazi ya shehia.
“Hili
lililofikiwa na Kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo na rais wa awamu ya
nane Dk. Hussein Ali Mwinyi, linataka kusimamiwa kuanzia kule kwenye shehia
hadi taifa,’’alipendekeza.
Sheikh huyo,
anasema huu sio wakati wa kufukua makaburi kama anavyosema rais wa Zanzibar,
hivyo hivyo na huku kwenye siasa, kama nchi imetulia tushirikiane kuijenga
Zanzibar.
Haji Haji
Khamis Mbwana, imamu wa msikiti wa Ijumaa Micheweni, alisema sasa wakati umefika
kwa kuanzishwa vilabu vya amani na ushirikiano katika kila skuli ya Zanzibar.
Lakini,
sheikh huyo akaenda mbali zaidi, akisema kama sasa taifa limeshatulia, sio
busara na wajiepushe viongozi wa dini kutumiwa na wanasiasa, kwani inawezekana
kutumiwa huko wakatoka nje ya maadili na kusababisha jazba.
Mara baada
ya kumaliza kula kiapo hapo Disemba 8, mwaka 2020, cha kuwa Makamu wa Kwanza,
Maalim Seif Sharif Hamad, alisema kilichomsukuma kuitaka nafasi hiyo, ni
kuiangalia Zanzibar kwanza.
“Zanzibar
kwanza kisha chama, hivyo sisi ACT, kwanza tumevutiwa na aina ya uongozi wa
rais wa awamu ya nane Dk. Hussein Ali Mwinyi, pili ni kuendeleza maridhiano ya
wazanzibari,’’anasema.
Mara baada
ya shughuli hiyo, rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi, alisema Zanzibar itajengwa na wazanzibari wenyewe.
“Leo tukiwa
ndani ya serikali ya Umoja wa Kitaifa, sasa kilichobaki kwa wananchi na
kuyaenzi, kuyaendeleza, na kuyaheshimu maridhiano hayo,’’anasema.
Zanzibar
kufuatia marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iliweka kwenye
sehemu yake ya pili, kifungu cha 39 kilitaja kuwepo kwa Makamu wawili.
Ambapo
kifungu cha 39 (3), kimesema Makamu wa Kwanza atatakiwa awe na sifa ya kuwa
Mjumbe wa baraza la Wawakilishi na atateuliwa na rais, baada ya kushauriana na
chama anachotoka Makamu huyo.
Ambapo
kifungu kidogo cha (5) cha Katiba hiyo, kimesema Makamu huyo wa Kwanza, atakuwa
ni Mshauri mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake.
Aidha
kifungu cha (6) kimemtaja kuwa rais pia atamteua Makamu wa Pili wa rais, kutoka
miongoni mwa wajumbe wa baraza la wawakilishi, kutoka katika chama anachotoka
rais.
Watanzania
na Zanzibar kwa ujumla wanatarajia kuingia tena kwenye uchaguzi wa awamu wa saba,
wa mfumo wa vyama vingi hapo mwaka 2025.
Huku hayo
yakifanyika, hivi karibuni aliyekuwa Afisa Mdhamini wizara ya Habari, Utalii na
Mambo ya Kale Pemba Khatib Juma Mjaja, alisema dhana ya utunzaji wa amani inawahusu mno waandishi wa habari.
Hayo
aliyabainisha kwenye mkutano wa siku moja, ulioandaliwa kwa pamoja baina ya
Klabu ya waandishi wa habari Pemba PPC na Shirika la Internews.
Ambapo
baadhi ya waandishi walioshiriki kwenye mkutano huo, walisema PPC na Internews
wamefikiria jambo jema kuwakumbusha namna ya kuandika habari za maridhiano hasa
kipindi hiki Zanzibar ikiwa imezaliwa upaya.
Mwisho
Comments
Post a Comment