Na Nihifadhi Issa Zanzibar@@@@
Katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania imeweka wazi haki za wanawake za kushiriki katika uongozi, ibara ya 21 inasisitiza kuwa kila raia wa jamhuri ya muungano ana haki sawa za kushiriki katika uongozi wa nchi aidha moja kwa moja au kwa njia ya uwakilishi.
Kwa katiba ya zanzibar sehemu inaeleza kwamba kila mtu apewe nafasi sawa katika kupata nafasi za uongozi kwenye serikali, aidha kwa njia ya moja kwa moja ama kupitia wawakilishi wao waliochaguliwa kwa njia ya huru na haki.
Aidha mpango wa utekelezaji wa beijing katika maelezo ya dhamira namba 7 imeeleza uezeshaji wa mwanamke na ushiriki katika vyombo vya maamuzi kwa kuangalia uwiano wa jinsia ili kuhakikisha wanawake na wanaume wanapata nafasi sawa ya kushiriki katika ngazi zote za maamuzi
Licha ya hayo yote ambayo yanayompa nafasi mwanamke kushiriki kikamilifu nafasi ya uongozi lakini kuna changamoto mbalimbali zinazomkwamisha kufikia ndoto hizozakuwa kiongozi ikiwemo suala la rushwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania MH Samia Suluhu Hassan mnamo june 22 2017 kipindi alipokuwa makamu wa Rais wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa Ngazi za juuwa mapambano dhidi ya Rushwa uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam alisema “kupambana na rushwa ni jambo la msingi na muhimu kwani ni mbaya nan a imeharibu sana maisha ya watu, maendeleo ya kiuchumi , kisiasa na kijamii hivyo ni lazima ikomeshwe ili jamii iishi iishi maisha mazuri” alisema Mh Samia
Rushwa hutamalaki katika maeneo mbalimbali nchini ndio maana mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar ZAECA kuwekeza elimu ya rushwa kwa jamii hususan wanawake ili kuwajengea uadilifu Zaidi katika kupambania haki zao.
Mgeni Salami Suleiman Mkuu wa divisheni ya elimu kwa umma ZAECA Amesema uwepo wa sheria mpya namba 5 ya mwaka 2023 ni maboresho ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha rushwa na uhujumu uchumi haipati nafasi huku akieleza kuwa imekuja muafaka kwa wanawake kujisimamia na kuwa mabalozi katika kuelimisha wengine ili kuepukana na tatizo hilo
Akizungumzia sheria hiyo inavyomlinda mwanamke katika masuala ya kufikia ndoto za uongozi amesema dhamira ya serikali ni kufikia usawa wa kijinsia wa asilimia 50/50 ikiwa ni kufuata sheria na mikaataba mbalimbali iliyoiridhia ambayo imetoa haki kwa kila mtu kushiriki katika nafasi za uongozi.
Amesema sheria hiyo imekuja kuongeza nguvu na kusawazisha baadhi ya mapungufu ambayo awali yalikuwepo katika sheria iliyopita kwani inasadikika kuwa waathiriwa wakubwa wa rushwa iwe ya pesa, ngono au yoyoye ile ni wanawake na wengi hushindwa kukabiliana nayo na hupelekea athari mbalimbali katika maisha yao ikiwemo kutojiingiza tena kwenye kinyanganyiro cha kugombea nafasi za uongozi
“katika sheria hii mpya kuna kipengele cha usiri wa taarifa mfano mwanamke amekwaza katika kufikia ndoto zake kwa namna yoyote sheria ipo rafiki yeye kupeleka taarifa zake na haitakiwi kutoka,
“kifungu cha 15 cha sheria hii kinamtaka mfanyakazi wa zaeca wawe na usiri na pindi ikithibitika mahakamani mfanyakazi wa zaeca ametoa risi anachukuliwa hatua ya kifungo miaka mitatu hivyo wanawake pamoja na makundi mengine wawe huru kuleta taarifa”alisema Mgeni
Katika sheria hiyo namba 5 ya mwaka 2023 kifungu cha 52 (1) kinaeleza mtu ambaye kwa namna yoyote atashawishi, atakubali na ataahidiau ataahidi mkufanya ngono au atamfanya mtu mwengine akubali au aahidi kufanya ngono kwa ajili ya kupata huduma au kutotoa huduma ametenda kosa
Aidha (2) ya kifungu hicho kinaeleza endapo ngono imefanyika kwa ajili ya mnufaika wa ngono hiyo afanye jambo amabnli lipo kinyume na sheria, adhabu yake ni kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka saba lakini kisichozidi miaka kumi pamoja na faini isipongua shilingi milioni kumi na tano za kitanzania lakini isiyozidi milioni ishirini za kitanzania.
“Kwa vile wahanga wakuu ni wanawake kupitia adhabu hizi basi iwe rahisi mwanamke akitokezewa na tatizo hilo afike zaeca hatua ichukuliwe ikitokea kila mfanya makosa hayo akafungwa miaka 7 tunaimanai vitendo hivyo vitapungua au kumaliza kabisa”alimalizia mgeni
Makala hii imezungumza na mwanamke ambaye ameomba hifadhi ya jina lake anasema suala la rushwa lipo lakini waliowengi hawalizungumzi kwani wanahisi ni kujitia aibu na kujidhalilisha mwenyewe hivyo wengine huamua kukaa kando.
‘’sitosahau kamwe suala la Rushwa limenifanya hadi leo hamu ya kuwa kiongozi kunitoka nimegombania karibia miongo miwili sikupata nafasi hiyo haikunikatisha tamaa nilijua ndio masuala ya ushindani,
“lakini nakumbuka tulienda mahali fulani katika masuala ya chama na kukawa na uchaguzi nami ni mmoja ya wagombania nafasi zile cha ajabu nikiwa nimelala alikuja kiongozi wa chama akanitaka niuvue utu wangu eti nitapata hiyo nafasi nilichang’anikiwa nikaanza kupiga kelele akatoka tangu siku hiyo nikaamua tu kubaki mwanachama wa kawaida” alisema
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA Zanzibar Dkt. Mzuri Issa Amesema wanawake na wasichana wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kufikia ndoto zao za kimaendeleo ikiwemo rushwa ya ngono na hawana pahali maalum wanapoweza kukimbilia.
“Elimu bado inahitajika na kazi ya kudhibiti vitendo vya rushwa sio ya ZAECA pekee bali inahitaji ushiriki wa kila taasisi hasa ukizingatia kuwa kinga ni bora kuliko tiba”alisema mzuri
Aidha Dkt. Mzuri anasema ”kuanzishwa kwa sheria mpya ya ZAECA kutafungua ukurasa mpya katika mapambano ya rushwa hasa ya ngono katika nafasi za kazi za kitaifa na za kisiasa na hasa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025’’alifafanua
Mwanasiasa Halima Ibrahim anasema ikiwa sheria hiyo mpya itafanyiwa kazi kwa uadilifu itatoa mwanya kwa wanawake kuhamasika kuingia kwenye uongozi “ kwani wataona sasa tumepata mtetezi zile kero tutasilisha sehemu husika na hivyoule usawa wa kijinsia tunaoulilia tutapata mwarubaini wake,
“binafsi napongeza sana juhudi hizi na natoa wito kwa wanawake wenzangu tusivumulie haya masuala ya rushwa ndio yanakwamisha juhudi zetu pengine mtu sifa zote unazo za kuwa kiongozi lakini unakatishwa tamaa kwa kitu kidogo tu tufike sehemu husika tusizembee uongozi ni haki yetu tupinaie tuufikie usawa wa 50/50”alisema Halima.
Comments
Post a Comment