HIVI NDIVYO TAMWA -ZANZIBAR ILIVYOFANIKIWA KUWAJENGA WAANDISHI VIJANA, MASUALA YA WANAWAKE NA UONGOZI
Na Nihifadhi Abdulla, UNGUJA.
Jitihada mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa siku hadi siku kuhakikisha usawa wa kijinsia unachukua nafasi yake kwa kupitia mikataba ya kimataifa, kikanda, sera, sheria, matamko na mbinu nyengine tofauti
Mpango wa utekelezaji wa beijing katika maelezo ya dhamira namba 7 imeeleza uezeshaji wa mwanamke na ushiriki katika vyombo vya maamuzi kwa kuangalia uwiano wa jinsia ili kuhakikisha wanawake na wanaume wanapata nafasi sawa ya kushiriki katika ngazi zote za maamuzi
Aidha Mkataba wa kikanda wa nchi za kusini mwa afrika kifungu cha 12 kinasisitiza ushiriki sawa wa wanawake kufikia asilimia 50/50 kwenye nyanja za maamuzi, pia kifungu namba 13 kinaeleza kuwekwa mikakati madhubuti ya kuwawezesha wanawake kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi na upigaji kura na kuondosha mila na desturi potofu zinazopingana na maendeleo ya mwanamke katika siasa na uongozi
Chama cha waandishi wa habari wanawake TAMWA Zanzibar ni taasisi inayotetea mambo mengi ya haki ikiwemo za wanawake katika kuhakikisha kunakuwepo na fursa sawa na kufikia lengo la uongozi wa 50 kwa 50.
Waswahili husema “kidole limoja hakivunji chawa” katika mipango ya TAMWA ya kuwawezesha wanawake kuingia katika uongozi imeamua kushirikiana na waandishi wa habari Vijana visiwani zanzibar ili kuunga nguvu ya pamoja kuhakikisha lengo linafikiwa.
Mkurugenzi wa chama hicho dkt. Mzuri issa anasema TAMWA wameamua kushirikiana na waandishi hao kwani wananchi wanaviamini vyombo vya habari na vinawafikia waliowengi wa wakati mmoja
Alieleza kuwa kwa kuhakikisha waandishi vijana wanafanya kazi ya kuelimisha jamii kuhusu usawa wa kijinsia kwa uweledi waliwajenga kwa kuwapa mbinu zitakazowasaidia kuandika na kutangaza yatayoibua upatikanaji wa haki hiyo
“waandishi wa habari wanauwanja mpana na wanayajua mengi hivyo tumeamua kushirikiana nao kwa kuwapatia kwanza mafunzo namna bora ya kuandika na kuhamamsisha masuala ya wanawake katika uongozi, “wananchi waliowengi wanaamini vyombo vya habari na wanajifunza pia kipi kimejiri kwa mfano kila sehemu iwe radio, tv, mitandanao ya kijamii na magazeti wakisikia masuala ya 50 kwa 50 wanawake na uongozi tunaimani wanahamisika zaidi” alifafanua dkt. Mzuri
Afisa mradi wa kuwawezesha waandishi wa habari vijana kuandika habari za wanawake na uongozi kutoka TAMWA zanzibar (YMF) Tatu Ali Mtumwa amesema waandishi wa habari Vijana wamekuwa chachu ya maendeleo kwa kuhamasisha usawa wa kijinsia ili kufikia 50/50 kwa wanawake na wanaume katika ngazi za maamuzi.
“tumeamua kulenga zaidi kwa vijana kazi hii inataka moyo ya kupambana na kujitoa ili wawe waandishi bora na wa mfano kuanza sasa na majukumu yao yote ya kila siku kuwa wahamasishaji wa masuala haya ya wanawake na uongozi na mengineyo yenye lengo kutetea haki na kuleta maendeleo”alisema Tatu
Aliendelea kusema kuwa tamwa imewajenga waandishi hao kuandika kazi zao kwa kuzinagtia mikataba Na wawe wajuzi wa kutumia tamwiku ili iwe rahisi kulinganisha hali iliyopo na inayotarajiwa “sio kama mwanzo hawaandiki lakini tumeona haja ya kuwapatia ujuzi zaidi wa kutumia matumizi sahihi takwimu kutumia, mikataba na matamko mbalimbali kwani hiyo ni kielelezo tosha kwamba mwandishi anaandika kitu ambacho anauhakika nacho”alifafanua.
Berema Suleiman ni miongoni mwa waandishi wa habari vijana anasema awali alikua akifanya kazi zake kikawaida bila ya kutumia tawimu “baada ya kupata elimu kutoka TAMWA mwanzo iliniwia vigumu lakini sasa naona utofauti kwani kazi ambayo inavielelezo huwa na mvuto haichoshi kusoma wala kusikiliza
‘‘Hii imenifanya kujua mambo mengi mfano suala la masheha kumbe ni asilimia ndogo sana ya wanawake mwanzo niliona ni kitu cha kawaida tu sasa nikiaandaa kazi zangu sipati shida kuwasilisha kwa jamii kwani huwa imeshiba takwimu na pia natumia mikataba au sheria kuithibitishia jamii kwamba kitu ninachowasilisha kipo sahihi kisheria’’alieleza Berema
Mbali na hayo TAMWA Zanzibar imeamua kuchukua juhudi mahususi za kuandaa tuzo ili jamii itambue mchango wa wanawake na uongozi katika sekta mbalimbali ili kuinua hali za wanawake na kuongeza ushiriki wao katika masuala ya uongozi katika ngazi zote za maamuzi kama ilivyoelezwa katika katiba ya nchi, mikataba, na itifaki mbalimbali za kimataifa.
Kwa muda wa miaka mitatu mfululizo sasa hutolewa tuzo hizo za umahiri wa uandishi wa habari za wanawake na uongozi zinazoangazia maeneo mbalimbali ya kupigania haki ya wanawake na mabadiliko ya kufikia 50/50
Kwa mwaka huu tuzo hizo zilitolewa machi 9, 2024 katika ukumbi wa SHAA uliopo mkoa wa mjini magharib ambapo jumla ya kazi 529 ziliwasilishwa kutoka vyombo vya habari mbalimbali vya Zanzibar ikiwa na dhamira ya endelevu inayoakisi waandishi wa habari kuongeza sauti za wanawake na kuchangia katika maendeleo yao.
Katika mkutano mkuu wa wanachama wa TAMWA Zanzibar uliofanyika April 4, mwaka huu huko Tunguu Dkt. Mzuri alisema juhudi za TAMWA za kuwajengea uwezo waandishi wa habari vijana zimezaa matunda.
“vijana wetu wa YMF wengi wamewasilisha kazi za kushindanisha na asilimia kubwa walioshinda katika vipengele vile ni wao hii inaonesha dhahiri kuwa tayari wameanza kubobea kwani ushindani ulikuwa mkubwa na wengine ni marra yao ya kwanza kushindanisha kazi zao
“Hatujakosea kuekeza nguvu kwao kwani tayari matunda yameonekana huu usiwe mwanzo kwao bali waendeleze juhudi hizo kama sehemu ya masiha yao katika kuwatetea wanawake kupata haki yao ya uongozi na kufikia usawa wa kijinsia” alieleza Dkt. Mzuri.
Hassan Mselem kutoka Pemba amesema akiwa mwandishi wa habari kijana TAMWA imemjenga kujiamini katika kazi zake kwa kumuelekeza namna bora ya kuandaa vipindi kwani mwanzo hakuwa mtumiaji wa takwimu huku akieleza kuwa taasisi zinazotetea ghaki za wanawake zinapaswa kuiga juhudi za TAMWA.
“binafsi naipongeza TAMWA kuwa miongoni mwa wanufaika wa mradi hii imenisadia kufanya kazi zangu kwa uweledi tofauti na mwanzo na ikanipelekea kupata ushindi katika tunzo za uandishi wa habari mahiri za takwimu kuhusu masuala ya wanawake na uongozi yalioandaliwa na wenyewe TAMWA
“juhudi hizi zinapaswa kuigwa na taasisi nyengine katika kuhakikisha lengo hasa la usawa wa kijinsia linafikiwa kwa bila ya kuibua na kuonesha uwezo wa mwanamke katika kuongoza hatutofika tunapopataka” alimalizia Hassan
Zuhura Juma Said ambae ni mwandishi kijana alieibuka mshindi katika tuzo hizo kupitia mtandao wa kijamii amesema kabla ya mafunzo hakuwa na uelewa mpana wa masuala ya wanawake na uongozi na mara nyingi alikua akiandika habari kuhusu changamoto zinazowakwamisha wanawake kufikia ndoto za uongozi.
“kiukweli awali nilikua naandika vinavyokwamisha wanawake kuwa viongozi lakini sasa naandika hata kazi wanazozifanya ambazo zinaonesha utendaji na uwajibikaji wao hivyo jamii inaona uwezo wa mwanamke katika uongozi, “naishukuru TAMWA kwa kunipika bila wao nahisi nisingefika hapa wamenipa fursa ambayo nimeona manufaa yake naomba huu usiwe mwanzo iwe ni endelevu kwa wengine ili nao wapate kuandika habari ama makala zenye ubora” alimalizia zuhra
Mradi uliotekelezwa na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na shirika la National Endowment for Democracy (NED) wa kuwawezesha waandishi wa habari vijana YMF kuandika habari za wanawake na uongozi umewashirikisha waandishi vijana ishirini na nne (24) kutoka Unguja na Pemba.
mwisho
Comments
Post a Comment