NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WAZAZI wanawake wa
kijiji cha Jamvini shehia ya Ndagoni, wilaya ya Chake chake Pemba, wametakiwa
kutenga muda wa kukaa na watoto wao, ili kuwaonesha njia za wao kuwa viongozi
mapema, ikiwa ni pamoja na kuwalea bila ya ubaguzi.
Ushauri huo umetolewa
na Masaidizi wa sheria Jimbo la Ziwani, shehia ya Wesha Khadija Said Khalfan,
wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, kwenye mfululizo wa mikutano ya
kutoa elimu, inayoratibiwa na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake
chake ‘CHAPO’.
Alisema, njia moja wapo
ambayo inafaa kuafutwa kwa wazazi hao, ni kuacha ubaguzi wa malezi kama vile
kubagua kazi ndani ya familia zao.
Alieleza kuwa, kazi
kama za kwenda dukani, kushughulikia mifugo, kubeba kuni zinatakiwa zisitolewa
kwa ubaguzi, bali watoto wa kike wafanyishwe, ili kukataa dhana ya ubaguzi.
Msaidizi huyo wa
sheria alieleza kuwa, njia nyingine ambayo inaweza kuwatayarisha watoto wa kike
kuwa viongozi wa baadae, ni kuwashirikisha katika mambo yanayofaa ikiwa ni pamoja
na madrassa au skuli anayotaka kusoma.
‘’Sio vibaya hata
kidogo mtoto wa kike, akaulizwa atanaka kusoma madrassa au skuli ipi, na wakati
mwingine hata kutaka ushauri wake, juu ya aina ya mlo wa siku,’’alieleza.
Aidha alifafanua
kuwa, hata kwa upande wa madrassa na skuli, anaweza kukabidhiwa uongozi kuanzia
wa darasa moja hadi wa skuli nzima, kama njia moja wapo ya kumzoesha mapema.
‘’Kwa mfano skuli
kuna nafasi ya Rais, makamu wa rais, spika na naibu wake na hata nafasi za
uwaziri, zote hizi mwanafunzi wa kike anaweza kuzoeshwa mapema,’’alishauri.
Katika hatua
nyingine, Msaidizi huyo wa sheria wa shehia ya Wesha Khadija Said Khalfan,
alisema hakuna sheria wala katiba yoyote ulimwenguni, inayomzuia mwanamke kuwa
kiongozi.
Alielelza kuwa,
Katiba zito mbili zimeweka mazingira ya usawa mbele ya sheria na kwamba kila
mtu anayo haki ya kugombea, kuchagua na kuchaguliwa pindi akitimiza vigezo na
masharti ya kisheria,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine,
amewakumbusha wanaume kwamba ndio wenye jukumu kubwa la kuzilinda familia kuanzia
watoto wao hadi wa jirani.
Alieleza kuwa,
hipendezi kuona wazazi hao, wanaelekeza nguvu zao zaidi katika kutafuta maisha
pekee, bali waelewa kuwa, sasa ulimwengu umebadilika na yapo majanga ambayo
huwakumba watoto.
Kuhusu kupinga
ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, aliitaka jamii kila mmoja, kuwa mlinzi
kwa mwenzake, ili kuhakikisha hakuna anayezifanyia sulhu kesi za udhalilishaji.
Kwa upande wake Mkaguzi
Msaidizi wa Polisi anayefanyakazi katika shehia ya Ndagoni na Wesha Khamis Ali Khamis,
aliwakumbusha wanawake hao, juu ya wajibu na haki yao ya kushiriki katika kuomba
uongozi ndani ya nchi yao.
Alieleza kuwa, wanawake
hawajaumbwa kwa ajili ya kuwapigia kura wagombe pekee, bali hata wao wenyewe wanatakiwa
kuomba nafasi mbali mbali kwa mujibu wa uwezo wao.
‘’Kwa mfano, mnaweza
kuomba nafadi za uwakilishi, ubunge, urais lakini pia kwa wenye mamlaka,
wanawajibu wa kuwateua kashika nafasi mbali mbali kama za uwaziri na katibu mkuu,’’alieleza.
Nae Mratibu wa
wanawake na watoto shehia ya Ndagoni Shuwarika Ali Mohamed, alisema bado elimu
ya kuomba nafasi mbali mbali majimboni kwa wanawake iko chini, hasa vijijini.
‘’Kwa mfano hata
ndani ya vikundi vyetu vya wanawake wenyewe, wapo wanawake wamekuwa wazito
kujitokeza kuomba au wakiteuliwa kuzishika nafasi hizo,’’alifafanua.
Maryam Issa Haji na
mwenzake Bimkubwa Mwalimu Mwadini, waliwashauri waalimu wa skuli na madrassa,
kuwapa nafasi za uongozi wanafunzi wa kike, ili waanze kujiozesha mapema.
Mratibu wa Chama
cha waandishi wa habari za Wanawake Tanzaania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba,
Fat-hya Mussa Said, alisema wamekuwa wakiendesha miradi kadhaa, yenye lengo la
kuwaonesha njia wanawake haki ya kugombea uongozi.
Mjumbe wa timu ya
wanaume wa mabadiliko Pemba, sheikh Abdalla Nassor Mauli, alisema suala la uongozi
kwa watoto wa kike, linakubalika katika maeneo wanayoyatawala wenyewe.
MWISHO
Comments
Post a Comment