IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA
DIWANI wa Wadi ya Kiuyu Pemba kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Nasra Salum Mohamed amesema, atahakikisha anatatua changamoto zote zinazowakabili wananchi ili kuleta maendeleo katika wadi yake.
Alisema kuwa, ametatua changamoto mbali mbali na anaendelea kushirikiana na wananchi kuziibua changamoto nyengine ili zipatiwe ufumbuzi kwa ajili ya maslahi yao na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika wadi yake alisema,
baadhi ya changamoto alizotatua ni pamoja na kuhamasisha kujengwa vyumba vinne
vya madarasa katika skuli ya Minungwini na vyumba vinne katika skuli ya
maandalizi Kangagani.
Mambo mengine aliyoyatatua Diwani huyo ni kuchimba shimo la vyoo
(chamber) katika skuli ya Minungwini, kuezeka vyumba viwili vya skuli ya
Mjinikiuyu, kujenga matundu manne ya vyoo katika skuli ya tutu Penjewani na
ujenzi wa kituo cha Afya Minungwini.
Diwani huyo alisema pia alitatua changamoto ya umeme katika kijiji
cha Kigongoni, Kage, Kangagani, kupeleka maji katika kijiji cha Kambini,
Penjewani na kusaidia kuchimba visima na kutoa michango ya ujenzi wa visima
katika maeneo mbali mbali, ili kuona kwamba changamoto za jamii zinatatuka.
"Najitahidi sana kusikiliza kero za wananchi na kuzifikisha
sehemu husika kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi, nashkuru sana tumefikia hatua
nzuri," alieleza diwani huyo.
Diwani huyo alieleza, lengo la kugombea nafasi ya udiwani ni
kutatua changamoto zilizopo ambazo zinawaathiri sana wanawake na watoto, hivyo
aliona atapambana nazo kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi na wadi yake inapata
maendeleo, jambo ambalo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wa mashirikiano na wananchi alieleza kuwa, wamekuwa
wakikaa pamoja na kuibua matatizo yaliyomo kwenye wadi yao na kuzifikisha
kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kutatuliwa.
"Nawashukuru sana wananchi wangu kwa kunichagua na kuniunga
mkono bega kwa bega, tunashirikiana pamoja na viongozi wengine wa jimbo, kwa
kweli tunafanikiwa katika shughuli zetu," alisema Nasra.
Harakati zake za kugombea uongozi Nasra zilianzia pale alipopewa
elimu na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) ya kuanzisha
kikundi cha ushirika kupitia mradi wa WEZA ambapo alianza kujijengea ujasiri na
kujiamini.
"Kwa kweli hapo ndipo nilipoanza kuwa mkakamavu na hatimae
kuweza kusimama mbele za watu kujielezea, hii ilinifanyia niingie kwenye
uongozi," alisema Diwani huyo.
Akielezea changamoto wanazokumbana nazo wakati wa kugombea ni
kukatishwa tamaa kwamba hawawezi na kuambiwa watakuwa wahuni ingawa
wanapofanikiwa wale waliowavunja moyo ndio ambao huwapa ushauri katika
kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wao wananchi wa Jimbo hilo walieleza kuwa, wamekuwa
wapeleka kero zao kwa diwani huyo, ambapo hukaa pamoja na kuzitafutia njia
mbadala za kuweza kutatuliwa.
Mwananchi Fatma Jafar Faki alisema kuwa diwani huyo wanashirikiana
nae bega kwa bega katika kutatua changamoto zinazowakabili, jambo ambalo
linawapa faraja kubwa.
Nae mwananchi Asha Omar Rashid alieleza kuwa, pia amewapa ujasiri
wa kwenda kufikisha barua za malalamiko sehemu husika baada ya kukaa nae pamoja
kuandika kero zao na baadae yeye hwenda kulisemea na kulitilia mkazo.
Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said alisema kuwa,
wanaendelea kuwajengea uwezo wanawake na jamii, ili wawe na muelekeo chanya wa
kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment