RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi, ameziagiza taasisi, serikali ya Mkoa na Wilaya kuhakikisha wawekezaji
wanaajiri vijana wa maeneo ambayo watawekeza, ili azma ya Serikali kukiinua
kisiwa cha Pemba kiuchumi iweze kufikiwa.
Alisema kuwa, sio jambo zuri kuona mwekezaji anaajiri vijana wa mbali
na kuwaacha vijana wa eneo husika, hivyo ni vyema lisimamiwe vizuri hilo, ili
kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji, hali ambayo itasaidia kukuza
kipato cha wananchi na kuimarika kiuchumi.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa barabara katika maeneo huru ya
uwekezaji Micheweni Aprili 23, 20204, ikiwa ni katika shamra shamra za maadhimisho ya miaka 60 ya
Muungano wa Tanzania Dk. Mwinyi alisema, Serikali ya awamu ya nane ya Mapinduzi
Zanzibar imedhamiria kukiinua kisiwa cha Pemba kiuchumi, hivyo ipo haja kwa
wananchi kunufaika na uwekezaji utakaokuwepo.
Dk. Mwinyi alieleza kuwa, kuna mambo mbali mbali yanayofanyika kwa
ajili ya kuinua kipato cha wananchi wa Pemba, ikiwa ni pamoja na kujenga uwanja
wa ndege wa kimataifa, bandari za kisasa, barabara zenye kiwango cha juu na
miundombinu mengine ambayo itasaidia kuimarisha maisha yao.
Aidha alisema kuwa, ili uchumi uweze kukua kwa haraka, Wizara ya
Uwekezaji isiwe nyuma bali ichangamkie fursa za uwekezaji, ili lengo la serikali
liweze kufikiwa.
Akizungumzia Muungano Dk. Mwinyi aliwataka wananchi wa Zanzibar
kuulinda na kuuthamini Muungano wa Tanzania, ili uweze kudumu na kuendelea
kunufaika nao.
"Lazima tujivunie kuwa na Muungano huu na wala asitokee yeyote
kuubeza kwa sababu kuna mengi tunayoyapata ya kimaendeleo kupitia Muungano
wetu, hivyo hatuna budi kuulinda na kuudimisha," alisema Dk. Mwinyi.
Dk. Mwinyi aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao sambamba na
kuishukuru kampuni ya ujenzi wa barabara hizo ya IRIS, kwa kazi nzuri
waliyoifanya na kusema kwamba wataendelea kuwapa kazi zao.
"Mradi huu umesimamiwa na Mamlaka ya Uwekezaji ‘ZIPA’ ambapo
tumeokoa fedha nyingi," alisema Mkandarasi huyo.
Nae Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema kuwa,
wana kila sababu ya kuendeleza Muungano ili uweze kudumu, kwani kuna maendeleo
makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka 60.
"Kuna mambo mbali mbali ya maendeleo ambayo yametekelezwa na
Serikali ya awamu ya nane, ambapo Dk. Mwinyi amejipanga kusimamia imara ili
kuhakikisha yanafanikiwa ipasavyo," alisema.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya alisema,
ushirikiano kati ya Serikali na wananchi, imesaidia kufanikiwa kila hatua,
hivyo aliwataka wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na
Serikali, katika kuwaletea maendeleo ya kiuchumi.
Alieleza kuwa, wananchi wa Micheweni wana mategemeo makubwa ya kupata
maendeleo ya kiuchumi kutokana na wawekezaji watakaowekezwa katika maeneo huru
pamoja na ujenzi wa bandari ya Shumba Mjini na ndio maana wanahamasika kuwaunga
mkono, ili kuhakikisha wanafanikiwa.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji
Zanzibar Sharif Ali Sharif alisema kuwa, wanaendelea kupata matumaini makubwa
ya kimaendeleo, kwani ujenzi huo wa barabara katika maeneo huru ndio utachapuza
uwekezaji na wananchi watafurahia zaidi.
"Mpango wa Serikali wa kukiinua kisiwa cha Pemba kiuchumi naamini
utafanikiwa kwani mambo mengi yameshaanza kutekelezwa na wawekezaji wameshaanza
kujitokeza hii ni faraja kwetu," alieleza Waziri huyo.
Mwakilishi wa Jimbo la Micheweni Shamata Shaame Khamis alisema kuwa,
amefarajika sana kuona uchumi wa wananchi wa Jimbo lake wataimarika kiuchumi
kutokana na uwekezaji utakaokuwepo.
Muungano wa Tanzania huadhimishwa kila ifikapo Aprili 26 ya kila
mwaka, ambapo kauli mbiu ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania ni 'Tumeshikamana,
tumeimarika kwa maendeleo ya Taifa letu'.
MWISHO .
Comments
Post a Comment