UONGOZI wa shehia
ya Wawi wilaya ya Chake chake Pemba, umesema uko makini na utatuzi wa migogoro
ya madai, na kuwataka wananchi wanaposhindwa kupata sulhu wenyewe, kuwafikishia
migogoro hiyo, kwa kuikabidhi kamati yake ya utatuzi wa migogoro.
Sheha wa shehia hiyo Sharifa Waziri
Abdalla, alisema kwa sasa anayokamati makini na yenye watu wenye uwezo mzuri wa
utatuzi wa migogoro, hivyo ni fursa ya kipekee kwa wananchi, kuitumia kamati
hiyo.
Alieleza kuwa, kwa sasa anao wasaidizi
wa sheria wenye sifa kubwa katika utatuzi, askari shehia, wajumbe wake ambao
wameshapata elimu ya utatuzi wa migogoro, jambo ambalo linampa faraja.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi, leo Aprili 23, 2024 Sheha huyo alieleza kuwa, haifai kwa jamii, kuifikisha migogoro hiyo ya
madai mbele ya vyombo vya sheria, kabla kwanza kupitia kwenye kamati yake.
Alifahamisha kuwa, utaratibu
uliokubalika ni kwamba, migogoro yote ya madai, lazima kwanza yasikilizwe ngazi
ya shehia na kisha uamuzi upatikane, na ikiwa pande moja haikuridhika, inaweza
kuvifikia vyombo vyingine.
‘’Wananchi wa shehia ya Wawi, sasa
njooni na migogoro yenu ya madai kupitia kamati yangu, maana ninaowatendaji
makini, ambao wanaweza kuonesha njia ya kufikia sulhu,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine Sheha huyo wa
shehia ya Wawi, aliwataka wananchi hao, kuendelea kufuatilia mikutano mbali
mbali ya wazi, inayoitishwa na kamati yake, ili kupata elimu ya sheria.
‘’Wasaidizi wa sheria, askari
shehia wanaungana na wajumbe wangu kuendesha vikao mbali mbali, kwa ajili kutoa
elimu au tahadhari ya jambo, ni wajibu wananchi kuhudhuria,’’alifafanua.
Hata hivyo, aliwakumbusha wajumbe
wa kamati yake, kuongeza ufahamu wa masuala mbali mbali yanayojitokeza katika
jamii, ili wanapotoa elimu iweze kuzaa matunda.
Wakati huo huo Sheha huyo, aliikumbusha
jamii kuacha kuzifanyia sulhu kesi zote za jinai, zikiwemo za udhalilishaji, na
atakaebainika kufanya hivyo, hatua za kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria zitafuata.
‘’Hata kwa wajumbe wa kamati yangu,
hili jambo la kuzifanyia sulhu kesi za udhalilishaji halipo, hivyo na jamii iendelee
kukemea, maana kufanya hivyo kunadhoofisha mapambano dhidi ya ukatili,’’alieleza.
Kwa upande wake Msaidizi wa sheria
wa shehia ya Wawi na Mgogoni Fatma Hilali Salim, alisema changamoto kubwa
katika utendaji wao wa kazi, ni jamii kutohudhuria mikutano wanayoiitisha.
Alieleza kuwa, wamekuwa wakikosa
elimu na maagizo muhimu kwa kule baadhi yao kutohudhuria mikutano wanayoiitisha,
jambo ambalo linachelewesha kufikia malengo yao.
‘’Mikutano yetu huzungumzia elimu
ya sheria mbali mbali, kama za ardhi, udhalilishaji, wizi, migogoro ya ndoa,
matunzo ya watoto, namna ya ukamataji na hata mirathi, hivyo wananchi wakipuuza
wanakosa elimu,’’alifafanua.
Katibu wa sheha wa shehia ya Wawi
Sham Haroub Said, aliwataka wananchi kuhakikisha kila mmoja, anakuwa mlinzi kwa
mwenzake, ili kuona hakuna anaezifanyia sulhu kesi za udhalilishaji.
Wanachi wa shehia hiyo, wamewataka
wenzao kuhakikisha wanahudhuria mikutano mbali mbali inayoitishwa shehiani humo,
ili kufikia lengo la utunzaji amani.
Mkuregenzi wa Jumuiaya ya Wasaidizi
wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema bado
wanampango wa kuwanoa zaidi wasaidizi wa sheria, ili kuwasaidia wananchi.
Mratibu wa CHAPO Mohamed Hassan
Abdalla, alisema kwa sasa wanaomradi wa upatikanaji haki, ambapo pamoja na shughuli
nyingine utakutana na baadhi ya masheha kujenga ukaribu zaidi na ofisi yao.
mwisho
Comments
Post a Comment