NA HAJI NASSOR, PEMBA
MAMLAKA ya Kuzuia rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar 'ZAECA' Pemba, inamshikilia Askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar 'JKU' kisiwani Pemba, kwa tuhuma za kupokea rushwa, kwa hadaa ya kuwaajiri vijana ajira ya kikosi hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa ZAECA Mkoa wa kaskazini Pemba' Nassor Hassan Nassir, alisema askari huyo anayetambuliwa kwa jina la Zaharan Mohamed Zaharan miaka 33 mkaazi wa Chokocho wilaya ya Mkoani Pemba.
Alisema ZAECA inamshikilia askari huyo kwa kosa la rushwa 'ubadhirifu wa mali na mapato' chini ya kifungu cha 43 (1) (a) cha sheria Mamlaka ya Kuzuia rushwa na Uhujumu wa Uchuni nambari 1 ya mwaka 2012.
Alieleza kuwa, mtuhumiwa huyo kwa nyakati tofauti mwaka huu 2022, akiwa mtumishi wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar 'JKU' akiwa na cheo cha private, bila ya halali alijipatia fedha kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 2.4.
Kamanda huyo wa ZAECA alifafanua kuwa askari huyo akijua kuwa hana uwezo alipokea fedha kwa vijana watatu, akiwaeleza ana uwezo wa kuwapatia ajira, jamboa ni kosa kisheria.
Kwa sasa alieleza kuwa,upelelezi wa shauri hilo, unaendelea kwa kasi na pindi utakapomalizika jalada la kesi yake litafikishwa kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka kwa hatua zao, ili kisha afikishwe mahakamani.
Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kuripoti matukio hayo, kila wanapoyasikia na kuwaomba watumishi wa umma kujitenga mbali na rushwa .(chanzo: Jamii TV Online)
mwisho
Comments
Post a Comment