NA HAJI NASSOR, PEMBA
KILA leo serikali hii ya Mapinduzi ya
Zanzibar, imekuwa ikitumia gharama kubwa na hadi kufikia kutoa mikopo, ili
kuhakikisha wananchi wake wanapata elimu ya juu kwa maslahi yao na taifa kwa
ujumla.
Siamini
kabisa, kwamba eti serikali hii itumie gharama ya kuwasomesha watu kisha
wakirudi masomoni, waje wakae vibarazani wasubiri uteuzi wa rais, la hasha
bali ni kuisaidia nchi kufikia uchumi wakati.
Maana wapo
wasomi walioandika vitabu na tunavisoma leo hii wakisema kuwa, ili nchi iendelee basi
chachu yake kubwa ni kwa wasomi wa ndani kutumia elimu yao kwa ajili maendeleo.
Sasa leo
nawauliza hawa wasomi wetu wenye chungu na darzeni ya digrii, kama sio masta na
PHD wamalizapo vyuo vikuu na kurudi nchini, mbona hatuwaoni wakifanya jambo au
wasubiri uteuzi wa rais?
Jamani
wasomi wetu kama hili ni kweli kwamba mmelewa na kusubiri uteuzi wa rais ili
ushike nafasi fulani, je kwa mtindo huo ndio tutaufikia uchumi wa kati.
Maana zipo
nchi ambazo leo hii zinaendelea kutumiminia misaada ya hali na mali, je
waliamka tu siku moja asubuhi na kuwa na uwezo mkubwa wa viwanda, jawabu sio
sahihi.
Bali
walifanya kazi kubwa ya usiku na mchana bila ya kujali kwamba waliajiriwa
serikalini au walifikia uchumi mkubwa eti wasomi wake kwa kuteuliwa………..
Mbona haya
hayaingii akilini mwa waliowengi, lazima wasomi wetu wa Zanzibar wajikurupushe
na pengine hata kuanzisha umoja wao mithili ya Dayaspora, ili kuona wanaisaidia
nchi na wananchi wake.
Hivi sasa
kila chochochoro, kila mtaa na kila kijiji kama sio kila familia, utasikia pana
kijana tena shababi ana mastar, PHD, digrii mbili na mwengine ni daktari mwenye
elimu ya MDs kama sio specialization, lakini wote hawa wanafanyaje au ndio
wanaongojea uteuzi?
Maana hawa
kama wakiungana pamoja na kuitumia elimu yao ipasavyo, basi wanaweza kufanya
jambo ambalo pengine serikali yengehitaji mtaalamu kutoka masafa mapana ya
dunia.
Idadi ya
wasomi wetu wanaohitimu kila mwaka na kubahatika kurudi nchini wala sio ndogo
kihivyo, sasa kama wote hawa eti wanasubiri bomba la Ikulu, watangaazwe kisha
ndio waanze kuonesha ujuzi wao wa kikazi, tumechelewa.
Kwani
hamuwezi kukusanyika kwa mfano nyote mliosomea kilimo cha vitunguu au jinsi ya
ukulima wa pilipili manga kisha mkaanzisha umoja wenu na kuendesha kilimo hicho
cha kisasa kupitia mikopo itolewa na serikali, na kupunguza foleni ya ajira
serikalini?
Mbona wapo
wachache ambao hata hawaingii kwenye kundi la wasomi wanaotajika, leo hii wameshawaokoa vijana wetu kadhaa na wanaendelea kujiletea maendeleo
yao.
Chonde
chonde wasomi wetu, elimu mliokwenda kuichuma vyuoni sasa tuone matunda yake,
maana tumekuwa tukiimba kila siku kuwa, mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe.
Hebu
ondoweni fikra butu kuwa, kuiletea maendeleo nchi yako, kwamba eti lazima
uajiriwe serikali au kiongozi wa nchi akupe shavu la uteuzi.
Kumbukeni
kuwa, maandiko matakatifu yameshaeleza wazi kuwa, mwenye kujua hata aya moja
basi awafikishie na wenzake, sasa wewe, yule na hao wanaosubiri uteuzi wa rais
ndio waoneshe kazi, tutafika kwa mtindo huu.
Lakini hata
wakuu wa taasisi kwa wale watendaji ambao tayari wamo serikalini, msisite
kuwatumia mara warudipo vyuoni, maana mabadiliko huanza kwa mtu mmoja wakati
mwengine.
Mbona hili
la wasomi wetu kusahau uteuzi na kuanza sasa kuifanyia kazi elimu yao,
linawezekana kwani hao walioendelea leo walikuwa na akili zipi na sisi tumekosa
zipi.
Mwisho
Comments
Post a Comment