NA HAJI NASSOR, PEMBA:::-
MKUU wa mkoa wa kaskazini Pemba
Salama Mbarouk Khatib, leo Juni 11, 2022 ameungana na vilabu vitatu vya mazoezi
kikiwemo cha Gombani Fitness Club, na wadau wengine wa haki za mtoto wakiwemo
TAMWA, kwenye matembezi maalum ya kuelekea kilele cha siku ya mtoto wa Afrika, hapo
Juni 16, mwaka huu.
Mkuu huyo wa
mkoa, akiongozana na vilabu hivyo vya mazoezi, walianza matembezi yao Polisi
Madungu na kumalizia uwanja wa michezo Gombani wilaya ya Chake chake.
Baada ya
kumalizika kwa mazoezi hayo, pia yaliohudhuriwa na wakuu wa wilaya za Chake
chake na Mkoani, Mkuu huyo wa mkoa, aliwataka wanamazoezi hao, kuwa wazazi wema
kwa watoto wao.
Alisema,
wapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakijitoa mishipa ya fahamu, kwa kuwabaka watoto
wao wa kuwazaa, jambo linalosikitisha.
‘’Kwanza nianze
na nyinyi, muwe baba na mama wema kwa watoto wenu, maana sasa hali imekuwa
ikitisha kwa majanga wanayofanyiwa watoto wetu,’’alieleza.
Hata hivyo,
amesema wakati umefika sasa kwa wanaume wanaowatekeleza watoto wao, kwa
kuwakosesha huduma na hasa baada ya ndoa kuvunjika, kushughulikiwa kisheria.
Katika eneo
jengine, amewakumbusha wananchi umuhimu wa kushiriki mazoezi, kwamba faida zake
ni kubwa ikiwa ni pamoja na kukimbiza magonjwa hasa nyemelezi.
‘’Lakini
sasa nichukue fursa hii, kwa wenzetu wa Gombani Fitness Club, ZAPHIAS na
kikundi cha Obama vyote vya Chake chake kwa kuiunga mkono serikali katika
ulinzi wa mtoto na haki zake,’’alieleza.
Mapema Mkuu
wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, alisema hakuna namna bora kwa
mtoto kufanyiwa, kama kulelewa na kukua katika makuzi ya maadili mema.
‘’Sasa kama
baba anambaka mtoto wake wa kumzaa au kaka anambaka ndugu yake, watoto wetu waende
wapi, na je watapata makuzi na malezi bora,’’alihoji Mkuu huyo wa wilaya.
Afisa
Mdhamini wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali
Mfamau, aliwataka wanaume kuwahudumia kwa furaha watoto wao, kama walivyokuwa
na furaha wakati wa kuwatafuta.
Katibu wa
Gombani Fitness Club Khalfan Amour Mohamed, alisema wameguswa mno na haki za
mtoto, na ndio maana wameamua kufanya matembezi hayo.
‘’Sisi sote
tumepitia kwenye hatua ya utotoni, tunajua raha na machungu walioyapata wazazi
wetu, sasa na sisi tunataka kizazi cha sasa, kiishi kwa amani,’’alieleza.
Kwa upande
wake Mratib wa TAMWA -Pemba Fat-hya Mussa Said, alisema kundi la watoto
limekuwa likiishi kwa wasisi mkubwa, kutokana na maadui wao kuishi nao nyumba
moja.
‘’Sasa
watoto hawajuwi wakimbilie wapi, maana wabakaji na wadhalilishaji ndio
wanaopaswa kuwapa huduma za kila siku, sasa lazima mkazo uwekwe, kwenye kuwalinda,’’alishauri.
Mwisho
Comments
Post a Comment