NA HAJI NASSOR, PEMBA:::-
MKURUGENZI wa Jumuiya
ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake 'CHAPO' Nassor Bilali Ali, amewataka
wasaidizi wa sheria wapya, wa majimbo ya wilaya hiyo, kufanyakazi kwa bidi, ili
kuisaidia jamii, kupunguza matendo ya udhalilishaji.
Alisema,
jamii inakabiliwa na majanga kadhaa pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya,
migogoro ya ndoa, ardhi na matunzo ya watoto, hivyo ni wajibu wao kuona hayo
yanapungua.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, baada ya kuwapokea wasaidizi hao wa sheria, alisema
amefarajika kuona, Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, imewapa mafunzo
vijana hao.
Alisema,
moja ya eneo la Zanzibar ambalo haliko salama na majanga mbali mbali ni wilaya
ya Chake chake, hivyo wasaidizi hao wa sheria, wanayokazi ya kufanya ndani ya
jamii.
‘’Karibuni
sana kwenye jumuiya yetu hii, na sisi tumefarajika kuona, tumepata damu changa
ya kupambana na majanga mbali mbali, ili tuwe na taifa lenye amani,’’alieleza.
Aidha
Mkurugenzi huyo, alisema wakati wa utendaji wao kazi watakuwa karibu na wenzao
waliowatangulia, hivyo ni jukumu lao, kuwashirikisha katika harakati zao.
Katika
hatua nyingine, alisema kazi iliyofanywa na Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi
na Utawala Bora kupitia Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, ya kuwa na mradi
wa kuimarisha upatikanaji haki Zanzibar, ni jambo jema.
‘’Kupatikana
kwa wasaidizi wa sheria 50 Unguja na Pemba na wale watano wa majimbo ya wilaya
ya Chake chake, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo,’’alieleza.
Hata
hivyo, amewakumbusha wasaidizi hao wa sheria, kujiendeleza kielimu zaidi, ili
hapo baadae wawe wanasheria kamili.
Nao
wasaidizi hao wa sheria, walisema walikuwa na hamu kubwa ya kupata mafunzo
hayo, na sasa kilichobakia mbele yao ni kuihudumia jamii.
Mtarajiwa
msaidizi wa sheria Jimbo la Ziwani Nassra Bakar, alisema anachoomba ni
ushirikiano wa karibu na wasaidizi wa sheria wakongwe, ili kufanikisha ndoto
zake.
Kwa
upande wake mtarajiwa msaidizi wa sheri Jimbo la Ole Tuheni Talibu, alimuomba
Mkurugenzi huyo, kuangalia uwezekano, wa kuandaa mikutano katika majimbo yote.
Nae
mtarajiwa msaidizi wa sheria Jimbo la Chake chake Wahid Kombo, alisema kazi
anayoiona ya kuanza nayo, ni kukutana na wanafunzi wa madrassa, ili kuwapa
elimu ya kujikinga na matendo ya udhalilishaji.
Jumuiya
ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ iliyopo mkabala na Tume za
Uchaguzi Chake chake, ambayo imeanzishwa mwaka 2016, moja ya malengo yake ni
kuisaidia jamii kufikia upatikanaji wa haki, elimu, ushauri na msaada wa
kisheria kwa maskini na watu wenye ulemavu bila ya malipo.
Mwezi
Mei mwaka huu, jumla ya wasaidizi wa sheria 18 wa mjimbo ya uchaguzi ya Pemba,
waliungana na wenzao 32 wa majimbo ya Unguja, kupata mafunzo ya awali ya
wasaidizi wa sheria, yalioendeshwa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kwa
ufadhili wa LSF.
MWISHO
Comments
Post a Comment