NA HAJI NASSOR, PEMBA:::-
‘’WATU wote ni sawa mbele ya sheria,
na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya
sheria,’’ ndivyo inavyofafanua Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Maelekezo
hayo utayafuma mara ukiifungua Katiba hiyo, kwenye kifungu chake cha 12 (1),
ingwa suala la kupata msaada wa kisheria, haliguswi moja moja, lakini msingi wa
hilo upo.
Ndio maana
hapo sasa, kwa kuzingia msingi huo wa sheria mama yaani Katiba (ground norm), tunaweza kusema
kwa kinywa kipana kuwa, haki ya kupata msaada wa kisheria unamgusa kila mmoja.
Nikuulize, msingi
wa usawa mbele ya sheria kwenye kifungu hicho cha 12, kweli unaweza kuwa na
maana, iwapo wenzetu walioko kizuizini, ambao pia uhuru wao umedhibitiwa wasiwe
na haki ya kupata msaada wa kisheria?
Kwa hakika,
tena kwa jicho hata lisilokuwa na uwana sheria utagundua kuwa, haki ya kupata
msaada wa kisheria unawahusu, hata walioko kizuizini.
AZIMIO LA HAKI ZA BINADAMU
Haki ya mtu
kuwa huru, na kutokamatwa au kuwekwa kizuizini kumbe ni kinyume na sheria, na
miongozo kadhaa iwe ya kimataifa, kikanda, Afrika na hata kwetu Tanzania,
haikubali.
Huko ni
kumnyima mtu huyo haki yake ya kibinadamu, ambapo imewekwa kwenye Azimio la
Dunia la Haki za Binadamu, lile la mwaka 1948.
Ieleweke
kuwa, utu wa mwanadamu, unahitajika kuthaminiwa kama haki muhimu, ya mwanadamu
yeyote ambayo huipata, kwa kule kuwa yeye ni mwanadamu tu.
TANZANIA
Kwa mfano
taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, zinatambua na zinaendelea
kutambua haki hii ya mtu kwenda atakapo, pasi na kuvunja sheria.
Lakini kwa
hili aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar Jaji Mshibe
Ali Bakari, alikuwa akitoa ufafanuzi juu ya haki, akisema kukamatwa ndani ya kambi
ya Jeshi, hakuna utetezi.
‘’Haiwezekani
ukaingie kwenye kambi ya Jeshi la wananchi wa Tanzania, au Chuo cha mafunzo,
kinga iwe una haki ya kwenda, utakapo, hapo sio sahihi,’’anafafanua.
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Pemba PPC, Said Mohamed Ali, amekuwa
akisema hakuna uhuru usio na mipaka.
‘’Kila mmoja
anakumbuka alipokuwa na miezi sita, mwaka mmoja hadi miwili, akiweza kulala na
wazazi wake, ingawa kila umri ukiongezeka, alikuwa anatengwa,’’anasema.
KATIBA YA ZANZIBAR YA MWAKA 1984
Kwa bahati
nzuri mno, Katiba hiyo inatambua kuwa mtu anapowekwa kuzuizini kwa taratibu za
kisheria, haitohesabiwa kuwa ni ukiukwaji wa katiba.
Inatambua
kuwa, kila mtu yupo huru na hivyo kimsingi analindwa dhidi ya kukamatwa,
kufungwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa, kunyang’anywa uhuru wake.
MSINGI WA KUPATA MSAADA
WA KISHERIA UNAPOKUWA KIZUIZINI
Haki hii
imewekewa msingi na nyaraka za kisheria kabisa 'legal documents', ikiwemo Katiba ya Zanzibar ya mwaka
1984, Sheria ya Msaada wa Kisheria nambari 13 ya mwaka 2018 na hata Sera ya
sheria hiyo ya mwaka 2017.
SHERIA YA MSAADA WA
KISHERIA NAMBARI 13 YA MWAKA 2018
Zanzibar
imekuwa ikihakikisha, suala la utawala bora linaimarika, ambapo kabla ya ujio
wa sera na sheria hii, suala la upatikanaji wa msaada wa kisheria, iwe kwa
walio huru ama kizuizini, halikutambulika rasmi.
Ndio maana,
Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan
Said, akasema sasa hakuna sababu kwa wananchi, kuonewa kwa kutokujua sheria.
‘’Idara hii
imeanzishwa kwa ajili ya wananchi wanyonge, wasiojiweze na hata wenzetu wenye mahitaji maalum, ili kupata msaada, ushauri na elimu ya sheria bila ya
malipo,’’anasema.
Lakini hili
sasa, sheria hiyo imekuja kama vile ni mwarubaini wa kuimarisha utawala bora na
utawala wa sheria Zanzibar, kwa kule kuweka wazi kwa makundi mbali mbali.
Mfano sheria
hiyo, imeweka wazi haki ya msaada wa kisheria kwa watoto na watu wengine,
waliopo vizuizini katika vyuo vya mafunzo, Polisi au nyumba nyingine za
mahabusu ya watoto.
Kwa mfano
vifungu vya 41 (1(i), 34 na cha 35 vya sheria hiyo, vimeweka msingi wa
upatikanaji wa haki hiyo, kwa mtu aliyepo kizuizini, kwa kutambua mahitaji
yake.
Zuri la
uwepo wa sheria hiyo, imekwenda usoni, kwa kule kuweza kushurutisha hata Chuo
cha Mafunzo, Jeshi la Polisi au nyumba ya mahabusu ya watoto, kweka mazingira
ya upatikanaji wa msaada huo.
Azma hii,
imewalazimisha wakuu ya maeneo hayo ya uwekaji watuhumiwa kizuizini, mara wawaekapo
kuwapa taarifa kwa upana, juu ya haki yao ya upatikanaji wa msaada wa kisheria.
Hivi
karibuni Mkurugenzi wa Jumuiya wa wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake
Nassor Bilali Ali, aliwaambia wananchi wa shehia ya Michungwani, kuwatumia
wasadizi wa sheria.
‘’Wapo ambao
wameshanufaika na msaada wa kisheria na wengine walikuwa kizuizini, kwa zaidi
ya saa 24 wanazopaswa kushikiliwa, lakini kisha walipata dhamana,’’anaeleza.
Humud
Is-haka Ngwali wa Pujini, ni mmoja wa wanufaika wa msaada wa kisheria, wakati
alipokuwa na tuhuma za kuvamia shamba la mtu mwaka 2020.
‘’Pengine kama
sio uwepo wa sheria hiyo, mimi ningeshikiliwa Polisi, mpaka upelelezi
ukakamilika, lakini zilipopita saa 24, niliombewa na msaidizi wa
sheria,’’anakumbuka.
JE MAWAKILI WA KUJITEGEMEA WANA
NAFASI GANI?
Ilishazoeleka kuwa, kazi hii wenyewe ni wale
wasaidizi wa sheria, ambao wapo kila Jimbo la uchaguzi la Zanzibar, kwa wastani
kati ya wawili hadi wanne.
Lakini,
kumbe hata Mawakili wa kujitegemea na hasa kupitia Jumuiya yao ya Mawakili
iliyosajiliwa Zanzibar, wanayo haki, na fursa ya kutoa msaada wa kisheria kwa
waliopo vuzuizini.
Maana, yapo
mashauri ‘kesi’ ambazo ni nzito na pengine wasaidizi wa sheria, wanaweza kuwa
wepesi, lakini uwepo wa mawakili hao, huweza kuwasaidia wananchi waliopo
vuzuizini.
JARIDA LA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA
Ingawa kwa
mujibu wa jarida nambari 003 na Julai hadi Disemba mwaka 2021, linalotolewa na
Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, limetaja uwepo wa Wakili mmoja.
‘’Mpaka sasa
ni wakili mmoja pekee, aliyejitokeza kusajiliwa kutoa msaada wa kisheria, na
hivyo ni dhahiri kuwa, waliopo kuzuizini hawatonufaika na huduma
hiyo,’’linafafanua jarida hilo.
Kwenye
andiko lake hilo ukurasa wa 11, linatoa rai kwa mawakili wa kujitegemea, pamoja
na jumuiya yao kuhamasisha wengine zaidi kujitokeza kuwasadia walioko
kizuizini.
WANANCHI NA WADAU WA HAKI ZA BINADAMU
Khadija
Hassan Omar wa Wawi mwenye ulamavu wa viungo, anasema, haki ya kupatiwa msaada
wa kisheria kwa waliopo vizuizini, lipewe kipaumbele.
Khamis Issa
Haroun wa Wambaa Mkoani, anasema kama sheria inatambua kuwa watu wote ni sawa
mbele ya sheria, suala la walioko chini ya ulinzi kupata msaada wa kisheria,
litambuliwe.
Mtoto Mayasa
Himid Othman maiaka 16 wa Mchanga mdogo, anasema suala la upatikanaji wa msaada
wa kisheria, sasa linatakiwa kuwa na sheria yake.
‘’Wapo
watoto wenzetu wamekuwa wakiwekwa kizuizini kinyume na sheria, sasa lazima
mawakili na hata wasaidizi wa sheria, wapewe meno ya kutoa msaada
huo,’’anasema.
Kamanda wa
Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, anasema Pemba hakuna chuo cha
Mafunzo kwa ajili ya watoto, hivyo lazima msaada wa kisheria, wanapokuwa
kizuizini liangaliwe.
Mwenyekiti
wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Khadija Shamte Mzee, anasema hawatosita
kuzifanyia marekebisho, sheria ili ziende sambamba na matakwa ya wakati uliopo.
Wakili wa
watoto wanaokinzana na sheria kutoka Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’
Pemba Siti Habib Mohamed, anasema haki ya msaada wa kisheria iendelee
kuwanufaisha walioko kizuizini, kwa vile nao ni bindamu.
Mara baada
ya kuwaapisha Makatibu wakuu, rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliwataka kuzifanyia marekebisho sheria
ambazo zimepitwa na wakati.
Mwisho
Comments
Post a Comment