NA HAJI NASSOR, PEMBA:::-
MKUU wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar
Zahoro Massoud, amesema mchango na juhudi za kupambana na ukatili na
udhalilishaji, zinazofanywa na Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba TUJIPE, kama
zitaungwa mkono, matendo hayo yanaweza kuwa historia hapo baadae.
Alisema,
moja ya tasisi inayofanya kazi ya kushirikiana na jamii na ngazi ya serikali ni
TUJIPE, hivyo ni wakati kwa wadau wa haki za wanawake na watoto, kuwaunga mkono
katika mapambano hayo.
Mkuu huyo wa
Mkoa, aliyasema hayo Gombani Chake chake leo Juni 6, 2022, wakati akizungumza kwenye kongamano
la kujadili changamoto za vitendo vya ukatili na udhalilishaji, lililoandaliwa
na ‘TUJIPE’ kwa ufadhili wa the foundation for Civil Society.
Alisema,
wanaofikiria kuwa serikali pekee inaweza kumaliza matendo hayo ndani ya jamii
amekosea, bali juhudi kama za TUJIPE na wengine, wakiungana ni njia moja wapo
ya kupunguza matendo hayo.
‘’TUJIPE
mmekuwa mkinialika mara kwa mara, katika mikutano au makongamano na hata
uzinduzi wa miradi ya kupinga ukatili na udhalilishaji, ni mwanzo mzuri na
wengine waige,’’alieleza.
Aidha Mkuu
huyo wa mkoa, ameikumbusha jamii kushirikiana na vyombo vya sheria, katika
mapambano hayo, ili kuona watuhumiwa wanatiwa hatiani.
‘’Haipendezi
kuona mahakama inamuita mzazi, au mlezi au mwengine, ambae anaweza kutoa
ushahidi na kukataa, na kufanya hivyo, ni kudhoofisha juhudi za serikali na
wadau wake,’’alifafanua.
Mapema Mratibu
wa ‘TUJIPE’ Pemba Tatu Abdalla Msellem, alisema wamekuwa wakiendesha mradi wa kupinga ukatili na udhalilishaji kuanzia mwaka 2019, ambao kwa sasa umeshasambaa shehia 13 za wilaya ya Chake
chake na Micheweni.
‘’Moja ya
eneo la mradi huo ni kuwaelimisha wanafunzi, namna ya kujikinga na vitendo vya
ukatili na udhalilishaji, na ndio maana vipo vilabu 13, kweye skuli
kadhaa,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Mratibu huyo alisema moja ya changamoto inayozorotesha kumaliza
vitendo hivyo, ni ucheleweshaji wa hukumu.
Kwa upande wao wakuu wa wilaya
za Micheweni na Chake chake, walisema kama serikali imeshazirekebisha sheria,
sasa kilichobakia kwa jamii, ni kushirikiana na vyombo husika, ili washtakiwa
waadhibiwe.
Mkuu wilaya
ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, alisema juhudi na ushirikiano wa pamoja
unahitajika kila wakati, ili inapotokezea matukio hayo, iwe rahisi kufikishwa
mbele ya vyombo vya sheria.
Nae Mkuu wa
wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, alisema ndani ya kipindi cha uongozi
wake, atahakikisha watuhumiwa wa matukio hayo, wanafikishwa mahakamani.
Kamanda wa
Polisi mkoa wa kusini Pemba, Richard Tatedei Mchomvu aliwataka wanaharakati,
kuiangalia upya sheria ya Mtoto nambari 6, yam waka 2011 ya Zanzibar.
‘’Pamoja na
uzuri wa sheria ya Mtoto, lakini vipo vifungu ambavyo havizungumzii adhabu kwa
wazazi wanaofanya uzembe juu ya malezi, sasa hapa napo lipo tatizo,’’alishauri.
Akiwasilisha
mada ya hali halisi ya matukio hayo, Wakili wa serikali Ali Amour Makame, alisema
changamoto wanayokumbana nayo, ni waathiria kukataa kutoa ushahidi.
‘’Sasa
watoto wanaolalamikia kubakwa ama kulawitiwa, wanapokwenda vituo vya Polisi
hutoa maelezo mazuri, lakini wanapofika mahakamani, huyakana maelezo yao,’’alieleza.
Kaimu
Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba Safia Saleh
Sultan na Mratibu wa Chama cha Waandishi wa habari Tanzania ‘TAMWA’-Zanzibar
ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said, walisema kesi zinazowahusu wanyonge, hupata
hatia mara moja.
‘’Jamii
inatulalamikia kuwa, kesi ikimuhusu mfano mteule wa rais au mwenye fedha zake, mara
zote wanasema haipati hukumu ya kifungo, na wanatueleza bado hakuna utayari,’’alisema
Kaimu Mratib wa ZLSC.
Baadhi ya
washirikia wa kongamano hilo, akiwemo Azizi Simai Alawi wa Wawi, Mohamed Ali Hassan waliishauri ‘TUJIPE’
kutoa elimu hiyo ngazi ya skuli na madrassa, ili kuwafikia watoto moja kwa
moja.
Sheha wa
shehia ya Kichungwani Yussuf Ali Salim, Mkurugenzi wa ‘KUKHAWA’ Hafidh Abdi Said na mwananchi Hasina
Hassan Kaduwara walisema, bado hakuna adhabu kali kwa washtakiwa wa makosa hayo.
Mwisho
Comments
Post a Comment