NA HAJI NASSOR, PEMBA:::-
AMA kwa hakika katika siku saba za
wiki, waislamu huvaa mavazi ya stara wakiamini kuwa ndio maamrisho ya Muumba
hasa kutokana na kuwepo aya na hadithi zinazoeleza hayo.
Suala ka
kujistiri kwa waislamu ndio la kwanza katika maisha yao ya kila siku, na wengi
wao hufanya hivyo kwa siku zote ingawa kwa siku ya Ijumaa huvaliwa kanzu nyeupe
na kofia.
Uislamu ndio
njia ya maisha sahihi kwa mwanadamu, maana kila kitu kilichopo duniani
kimeelezwa ndani ya uislamu, jinsi ya kutenda au kuacha kutenda jambo hilo.
Roho za watu
na kusaidiana nalo halikuachwa ndani ya uislamu na kumbe sio mavazi pekee kama
wengine wanavyofikiria kwa kule kuvaa vazi hilo kila siku ya Ijumaa.
Ndio maana
leo naja kwenu waislamu kuwataka ule mng’aro wa kanzu na kofia zenye kupendeza
zinazovaliwa siku ya Ijumaa ni vyema zikaendana na roho za watu.
Maana
uislamu wala haupendi kuona mvaaji wa kanzu na kofia nzuri na kukimbilia
msikitini mapema, ikawa nafsi yake imetawaliwa na choyo, roho mbaya na ubaguzi.
Iweje mtu
ikifika Ijumaa ajitie kanzu yenye kung’aa na kofia yenye kupendeza lakini huyo
huyo, yeye na jirani yake ni kama paka na moshi?
Au ndio wale
tunaowaita waislamu wa mavazi, lakini mioyo yao iko wazi kwa kutosema na
majirani zao, au ndugu wa baba na mama lakini ikifika Ijumaa kanzu aliovaa
utasema huyu ni Al-haji wa Makka.
Hebu tukaeni
na kufikiria ni kwenye uislamu tunatakiwa tukae na kuishi na wenzetu, au ibaki
yatosha kuvaa kanzu na kofia nzuri na pengine hata kuwahi Masjidi mapema,
lakini kwenye nafsi, bado kuna moshi wa husda na choyo.
Hebu
tuzionee huruma kanzu na kofia zetu tunazovaa Ijumaa, ili kesho na keshokutwa
zisijetusuta, maana roho zetu haziko nyeupe kama yalivyo mavazi yetu.
Ingependeza
zaidi kuona roho na nafsi zetu zinaendana na kanzu zetu tunazozivaa siku ya
Ijumaa, ambayo ni sikukuu kwa waislamu, badala ya roho zetu kuwa nyeusi mithili
ya maji ya mkondoni au lami.
Na pengine
sasa ingekuwa jambo jema zaidi kuona, swala zetu zinaanzia kwa ndugu, jamaa,
wazazi, marafiki na majirani zetu kwa kuishi nao kama uislamu ulivyoagiza, ili
sasa tukivaa zile kanzu zetu zifanane na matendo yetu.
Haingii
akili na wala haikubaliki ndani ya uislamu kuona jirani mmoja hasemi na
mwenzake, kwa sababu wanazozijua mwenyewe, iwe kwa sababu ya rangi, kabila,
eneo analotoka au hata chama, maana uislamu hakuna neno ubaguzi.
Sasa lazima
tujikite katika kuisaka pepo kuanzia ndani ya nafsi zetu kwa kuzisafisha badala
ya kujipendezesha kwa mavazi, na pengine hapo mtu kujiona ameshaokoka, ingawa
hajui hali za jirani yake.
Yote
kwa yote mavazi yetu hasa kwa siku ya Ijumaa yanayopendeza na kung’aa basi
yaendane na roho na nafsi za mvaaji.
Lakini hata
na masheikh na wanazuoni wetu, mnayonafasi ya kulisemea hili kwa mnaowaongoza,
maana inawezekana wapo wanaofikiria kuwa uislamu ni mavazi.
Lakini ni
fardhi au lazima kwa muislamu mwanamke na mwanamme kusaka elimu tena hadi
China, ili kujitambua na kujielewa, maana mavazi na imani ni vitu viwili
tofauti.
Mimi naamini
kila kitu kinawezekana ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake, tena bila ya
kusubiri kusimamiwa, huku akiamini kuwa mtenda wema ajitendea nafsi yake.
Mwisho
Comments
Post a Comment