NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@
TUME ya haki za binaadamu na utawala bora, ofisi ya Pemba, imetoa wito kwa vyama vya
siasa kuzingatia na kuhakikisha ushiriki
wa watu wenye ulemavu katika mikutano ya kampeni zinazoendelea, kwa kuwawekea
mazingira rafiki kwa kuzingatia aina zao za ulemavu.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi Ofisini kwake Chake Chake Pemba, Afisa Mfawidhi wa tume hiyo Pemba
Suleiman Salim Ahmad alisema, katika kuhakikisha ushiriki nzuri wa watu wenye
ulemavu katika upigaji kura, ni vyema ni
vyema vyama vya siasa kuhakikisha
ujumuishi wao katika kampeni zinazoendelea.
Alisema kwamba, mazingira mazuri kwa
watu wenye ulemavu katika mikutano ya kampeni itasaidia kufuatilia sera zinazotolewa
na wagombea wa vyama vya siasa katika nafasi za Urais, Uwakilishi, Ubunge na
Udiwani, jambo litakalopelekea kuchagua viongozi wanaowataka kwa usahihi.
Alisema kua, pamoja na jitihada mbali
mbali zinazofanya na wadau na watetezi
wa haki za binaadamu, bado kunapengo kubwa katika ujumuishi wa watu wenye
ulemavu katika masuala mbali mbali
ikiwemo siasa.
" Pamoja na jitihada mbali mbali
zinazofanywa, baadhi ya vyama vya siasa havijazingatia mahitaji ya watu wenye
ulemavu katika mikutano yao, jambo linalowanyima haki yao ya msingi ya
kufuatilia sera za vyama zitakazo wasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kura zao"alisema.
Alisema kua ili kuziba pengo
hilo ni vyema kwa vyama vyote kuhakikisha wanaandaa mazingira rafiki kwa watu
wenye ulemavu wa aina mbali mbali, kwa kuzingatia aina ya mahitaji kutokana na
ulemavu wao.
"Ili kuziba pengo lililopo ni
vyema vyama vya siasa kuhakikisha wanaandaa mazingira rafiki kwa watu wenye
ulemavu wa aina zote, mfano kuweka wakalimani kwa ajili ya viziwi, kufanya
mikutano katika mazingira jumuishi kwa watu wenye ulemavu wa viungo na uoni,
pia kuweka wasaidizi ili kuhakikisha kila mtu anakua salama katika eneo husika,
"alisema.
Akieeleza athari zinazoweza
kujitokeza endapo hapatakua na ujumuishi wa watu wenye ulemavu wakati huu wa
kampeni alisema, ni pamoja na kupoteza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura,
kutokana na kutopata taarifa za kutosha kuhusu kiongozi anae mtaka, ama kukosa
kuchagua kiongozi mwenye sifa.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na
mwandishi wa habari hizi mmoja wa watu wenye ulemavu wa uziwi chini ya
mkalimani wake Yumna Mbarouk Yussuf alisema, hadi sasa hajapata ujumbe stakili
kutoka kwa wagombea ambao utamuwezesha kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua
kiongozi.
Alisema kwamba ipo haja ya vyama vya
siasa kuhakikisha ujumuishi wa kila mtu katika kampeni zao, ili kila mmoja
apate taarifa za kutosha juu ya kuchagua kiongozi anaemtaka.
Nae mmoja wa watu wenye ulemavu wa
viungo Said Saleh Sultan alisema, mazingira yaliomo katika maeneo ya
kampeni sio rafiki sana kwao jambo
linalorudisha nyuma ushiri wao.
Kwa upande wake Katibu wa chama cha
Mapinduzi Mkoa wa kusini Pemba Kajoro P. Vyohoroko alisema, chama hicho
kimeshaanza kuchukua hatua ikiwemo kutenga eneo maalumu kwa watu wenye ulemavu
katika mikutano ya hadhara, ambayo yanamuhusisha mgombea wa urais wa Jamuhuri
na Zanzibar.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC) jumla ya watu wenye ulemavu wapatao 8,021 wanatarajiwa kushiriki
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 visiwani Zanzibar.
Aidha Sheria ya Watu wenye
Ulemavu Zanzibar Namba 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 29 kinaeleza umuhimu wa
watu wenye ulemavu kuweza kufikia miundo mbinu mbali mbali pamoja na taarifa,mawasiliano
na haki zote za kibinaadamu na za msingi.
MWISHO
Comments
Post a Comment