IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
"WANANCHI wa Wadi yangu wana upendo na mimi, nilipochaguliwa walinifurahia sana, hivyo sina wasiwasi na ushindi,"
Hayo si maneno ya mtu mwengine bali ni ya Mtumwa Suleiman Salum mwenye umri wa miaka 41 mkaazi wa Ole Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.
Mtumwa ambae ni mgombea udiwani Wadi ya Ole kupitia chama cha Mapinduzi CCM, anasema atakapofanikiwa kuchaguliwa atahakikisha wananchi wake wanafurahi zaidi, kwani atawashirikisha kila hatua ili kuona wanafanikiwa kwa haraka.
Anaeleza, Wadi yake ni tofauti na nyengine kwani hata wananchi wa vyama vya upinzani wanampenda na kumuunga mkono, kutokana na kuwajali bila kuwabagua, hivyo anaimani atachaguliwa kuwa diwani wa Wadi hiyo.
Wananchi wa Wadi yake walifurahi sana kuona kiongozi huyo mwanamke amepitishwa na wajumbe ili aweze kushika nafasi hiyo, kwani wanaamini kwamba, changamoto zao nyingi zitapatiwa ufumbuzi kipindi kitakachokuja.
"Kwa kweli sina wasiwasi na nafasi hii na nawaomba wananchi wazidishe imani kwangu kwa kunipa kura za ndio, ili niweze kuwaletea maendeleo katika Wadi yetu," anasema mgombea huyo.
Amefanikiwa kuwa mgombea wa nafasi hiyo baada ya kuchaguliwa na wajumbe waliomuamini kwenye Wadi yake, ili awatumikie wananchi.
"Wajumbe waliniamini na ndio maana wakanichagua ili nigombee nafasi hii, wanajua kwamba nitaibua changamoto na kuzifikisha sehemu husika kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi," anafafanua mgombea huyo.
Mtumwa alijipanga kuchukua fomu kwenye Wadi baada ya kuona nafasi aliyonayo haiimpi fursa ya kuwaletea wananchi maendeleo kwenye Wadi.
Mama huyo aliibuka ushindi na kuwashinda watu watatu waligombea na kusema kwamba atahakikisha anasaidiana na viongozi wake wa Jimbo kutatua kero zilizomo kwenye wadi atakayoisimamia.
Mgombea huyo anasema, harakati zake za uongozi zilianzia mwaka 2002 akiwa Mjumbe wa Kamati ya siasa Wadi, ambapo aliitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2025 alipoamua kugombea nafasi ya udiwani.
"Lengo langu ni kutatua kero za wananchi na ndio maana nikaamua sasa nigombee nafasi ya udiwani ili niibue changamoto zinazowakabili wananchi wa Wadi yetu na kuifikisha sehemu husika kwa lengo la kutatuliwa," anasema mgombea huyo.
Mgombea huyo anasema, mgombea urais kupitia chama chao cha CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi amefanya maendeleo mengi katika awamu iliyopita, hivyo anahitaji wasaidizi imara na wenye moyo wa kujitolea ili kufikia pale wanapopataka.
Anasema kuwa, kupitia miradi mbali mbali watashirikiana na mbunge pamoja na mwakilishi katika kutekeleza, ili kuona kwamba wanafanikiwa kuleta maendeleo katika Wadi.
Anaeleza kuwa, atasimamia kuhakikisha wanafikisha miradi na kuwanufaisha wananchi wote wa matawi matatu ya Wadi hiyo.
"Kama ni maendeleo nitaleta na nitawasimamia vizuri na hawataendelea kunyimwa miradi, kwani nitahakikisha na Wadi yetu inanufaika," anaeleza.
Anasema, wananchi wake watarajie maendeleo katika Wadi yao, kwani amejipanga kupambania kwa hali na mali ili wafaidike na miradi ya kimaendeleo.
Alipofanikiwa kuingia kwenye Wadi kugombea, alifurahi sana na kumshukuru Mungu kwa kumjaalia kupata nafasi hiyo kwani sio ujanja wake kuipata.
Mtumwa anafafanua kuwa, jamii yake inamuunga mkono na kumfurahia kwani wajua kwamba ni mpambanaji mwenye kiu ya kuwasaidia.
"Wamefarijika sana kuona mwanamke anagombea kwa sababu wanajua kwamba wanaweza kuleta mabadiliko ya haraka katika jamii," anaeleza.
Wakishirikiana na wananchi atajitahidi kuibua changamoto na kuzifikisha sehemu husika sambamba na kumtafuta mbunge na mwakilishi kwa ajili ya kumuwezesha kupitia mfuko wa Jimbo ili nao wakatekeleze.
Anasema, mashirikiano kati yake na viongozi wake wa Wadi ni mzuri kwani wanansaidia kupiga kampeni ya pamoja na ya nyumba kwa nyumba, hiyo inaoneshea wazi kwamba wanamuunga mkono.
Aliwataka wananchi watulie katika kipindi hiki cha siasa kwani kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo wahakikishe wanadumisha amani iliyopo.
"Siasa isiwe chanzo cha kutenganisha watu na kuhasimiana, bali kila mmoja ajitahidi ifikapo Oktoba 29 akapige kura kwa ajili ya viongozi bora," anasema.
Anawaomba wananchi kuwachagua viongozi wa chama cha Mapinduzi CCM kwa ajili ya kuwaletea maendeleo endelevu katika nchi.
Kuingia katika uongozi Mtumwa, hakushawishiwa na mtu bali alifikiria na kuona kwamba njia pekee ya kuwasaidia wananchi ni kugombea nafasi hiyo, ndipo alipoamua kuchukua fomu ili kuingia kwenye kinyang'anyiro.
"Japokuwa nilishinda kura za maoni lakini baadhi ya wajumbe hawakuridhika na wala sijui kwa nini, hizi ndio changamoto tunazokumbana nazo kwenye kusaka nafasi za uongozi," anasikitika.
Kwa vile kura zilitosha kuwa mshindi wa kugombea nafasi hiyo, azidi kupata ujasiri na kujiamini, hali ambayo imtasaidia kufanya kazi zake bila kuyumbishwa na changamoto yeyote inayoweza kutolea.
Dada wa mgombea huyo Khadija Suleiman Salum anamuelezea mdogo wake kwamba, tangu akiwa mdogo alikuwa na shauku kuwa kiongozi, hivyo walimjenga vile anavyotaka kwa kumpa elimu, ili atakapokuwa kiongozi afanye kazi zake kitaaluma zaidi.
"Tulimuona mwanzo kuwa ana ndoto za kuwa kiongozi, hivyo tulimpa mashirikiano na mpaka sasa tuko pamoja nae, tunamuombea afanikiwe ili atimize lengo lake," anaeleza dada wa Mtumwa.
Anasema, Mtumwa anaweza kutekeleza majukumu yake vizuri kwani kwani ni mtendaji, mtafutaji na anajituma katika mambo mbali mbali ya kuleta maendeleo yake na familia, hivyo atakapopata nafasi hiyo anaamini atailetea maendeleo Wadi yake.
Katibu wa Wadi ya Ole CCM Hamad Mussa Omar anasema, Mtumwa ni mtendaji mzuri, mwenye uelewa na mtunza siri, hivyo akipata nafasi hiyo ana uwezo mzuri wa kuongoza.
"Pia ana ufahamu wa kazi kwa sababu tayari ameshafanya kazi kwenye miradi mbali mbali, hivyo atawasaidia kufuatilia miradi iliyopo Manispaa ya Chake Chake, ili kuhakikisha inafika katika Wadi yetu," anaeleza Katibu huyo.
Katibu huyo anasema, kwa vile Mtumwa ni mtendaji mzuri, atapita kwenye vijiji kutafuta changamoto zilizopo na kuziwasilisha kwa mbunge na mwakilishi, ili washirikiane kuzitatua.
Alimtaka mgombea huyo, baada ya kuchaguliwa na kuwa kiongozi asiupe kipaombele uluwa (uongozi), kwani unaweza kumfanya ajione amefika na sio kuwatumikia wananchi, jambo ambalo litavuja uaminifu wake kwa wananchi.
"Namuomba ajitahidi sana kwa sababu uongozi ni dhamana, hivyo atakapofanikiwa kupata nafasi hiyo ashirikiane na wananchi kama anavyoshirikiana wakati huu, uongozi asiuvae sana mpaka akasahau majukumu yake," anasema.
Mgombea huyo ameolewa na ana watoto watatu, ambapo ana elimu ya diploma katika fani ya masuala ya biashara aliyoipata katika chuo cha Zanzibar College Business Education (ZCBE).
MWISHO.
Comments
Post a Comment