IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
MKURUGENZI wa Mwamvuli wa Asasi za Kiaraia Zanzibar (ANGOZA) Hassan Khamis Juma amesema, kutokana na maeneo mengi kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi kisiwani Pemba, kuna haja kwa wadau kushirikiana pamoja katika kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo katika jamii.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa masuala ya mabadiliko ya tabia nchi katika Ukumbi wa Wizara ya Kilimo Pemba, Mkurugenzi huyo aliwataka kuyafanyia kazi mafunzo hayo kwa ajili ya kujenga mazingira bora ya sasa na baadae.
Alisema kuwa, wamejikita kutoa mafunzo hayo hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ya ukanda wa bahari, ili kuelimisha jamii katika udhibiti wa mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameathiri sehemu mbali mbali kisiwani hapa.
"Tunaamini kwamba elimu hii tutaitumia ipasavyo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili mulete mabadiliko chanya katika jamii," alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha aliwataka kufanya kazi vizuri ili wanajamii waelewe, jambo ambalo litasaidia kuepuka kukata miti ovyo sambamba na kuyaweka mazingira ya vijiji vyao katika hali ya kuvutia.
Kwa upande wake Mjumbe wa ANGOZA Pemba Khalfan Suleiman Juma alieleza kuwa mafunzo hayo ni fursa adhimu kwao, hivyo waitumie ipasavyo na kuwafikishia wengine, ili washirikiane katika kudhibiti janga hilo linaloendelea kuathiri siku hadi siku.
"Tuelewe kwamba mafunzo hayo ni faida yetu na faida ya vizazi vijavyo, hivyo tujitahidi tunawarithisha watoto wetu elimu bora kwa maisha yao yote," alifahamisha.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo Afisa Kitengo cha Mabadiliko ya Tabianchi kutoka Idara ya Mazingira Zanzibar, Dk. Salim Hamad Bakar alifafanua kuwa, kila mmoja ana wajibu wa kutenda haki kulingana na mazingira anayoishi.
"Kila mmoja ana haki ya kuhakikisha hachafui mazingira na wala hasababishi athari yeyote inayoweza kupelekea madhara, bali tunatakiwa kudhibiti," alisema Afisa huyo.
Alisema kuwa, kumekuwa ongezeko la taka, uharibifu wa maeneo ya kilimo, fukwe na vyanzo vya maji ambavyo husababisha mafuriko na hatimae huleta maradhi ya mripuko.
Aidha alieleza kuwa, kuna baadhi ya wanajamii wamekuwa wakikata miti ovyo bila kuipanda, hali inayosababisha maji ya bahari kupanda juu kwenye makaazi ya watu pamoja na kuingia kwenye mashamba, hali ambayo inaweza kusababisha ongezeko la umasikini.
"Mabadiliko haya tumeyasababisha kwa mikono yetu wenyewe, hivyo kupitia mafunzo haya tuhakikishe tunapanda miti kwa wingi, hatutupi taka ovyo, tulime na tule vyakula vinavyostahiki," alisema.
Afisa Mazingira Wilaya ya Micheweni Salum Mjaka alisema mafunzo hayo ni muhimu kwao, kwani yamewaongezea uelewa ambao itawasaidia katika kutekeleza kazi zao za kutoa elimu kwa jamii.
Kaimu Afisa Kilimo Wilaya ya Micheweni Asha Khamis Saleh na Abdulrahim Ali Omar kutoka taasisi ya Kwanini Foundation walisema, kupitia mafunzo hayo wamejifunza vitu vingi na kuahidi kupita kwa wanajamii kutoa elimu ili kuhakikisha wanadhibiti mabadiliko ya tabia nchi kila sehemu.
MWISHO.
Comments
Post a Comment