MGOMBEA MWENZA wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi CCM Dk. Emanuel John Nchimbi amesema, katika miaka mitano inayokuja wamedhamiria kuongeza kasi ya zoezi la utafiti wa rasilimali za bahari, ili wananchi wapate maisha bora, kwani uchumi wa buluu umeleta mafanikio makubwa katika nchi.
Dk. Nchimbi ameyasema hayo wakati wa mkutano wa mkuu wa kampeni uliyofanyika katika viwanja vya Kinyasini Jimbo la Gando Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema, wanayo imani na matumaini makubwa kwamba ndani ya bahari kwa upande wa Pemba kuna rasilimali nyingi ambazo zitawasaidia wananchi kuwa na maisha bora, hivyo ilani ya CCM ya mwaka 2025/2023 imeweka wazi suala la kuongeza kasi ya zoezi la utafiti, ili kuimarisha zaidi uchumi wa wananchi.
"Pia tutaimarisha ufungaji wa samaki, vizimba vya samaki na ukulima wa zao la mwani ili kuinua kipato cha wananchi na kuwaletea manufaa katika familia zao," alisema Dk. Nchimbi.
Dk. Nchimbi alisema kuwa, anaamini kwamba chama kitapata ushindi wa kishindo, kwani wanajivunia mambo makubwa yaliyofanywa na marais kipindi kilichopita ambayo yamesababisha kuinua uchumi wa Zanzibar kwa asilimia 7.5.
"Kwa kweli uchumi umekuwa sana visiwani Zanzibar na hii ni kutokana na mashirikiano makubwa ya wananchi na wanachama wa chama cha Mapinduzi CCM, tunaona fahari kubwa kwa kazi zinazofanywa na marais wetu hawa," alisema.
Aidha alifafanua kuwa, ilani imeweka wazi suala la kuimarisha kilimo cha uzalishaji, kilimo cha umwagiliaji maji na kusema kuwa katika kufanikisha hilo ilani imeweka mkazo kwenye upatikanaji wa pembejeo, mikopo nafuu na masoko ya bidhaa, ili kuhakikisha kila siku kunakuwa na uhakika wa chakula.
Alieleza kuwa, wataendeleza amani na usalama sambamba na kulinda Muungano wa Tanzania, kwani unaendeleza umoja, undugu na kuondoa ubaguzi baina yao.
Vile vile alifafanua kuwa, wamedhamiria kujenga makumbusho ya historia ya Mapinduzi ili ifahamike na vizazi vyote vya sasa na vijavyo, kwa sababu Mapinduzi ndio yaliyomkomboa mzazibari, ndio yaliyowafanya wazanzibari wawe sawa, yameleta umoja, hivyo wanajivunia sana.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Mohamed Said Mohamed (Dimwa) alisema, ikiwa watamchagua Dk. Samia basi wajue kwamba atakuwa na msaidizi mzuri ambae ni kiongozi mwenye hofu ya Mungu na yuko tayari kuwatumikia wananchi.
Alisema kuwa, maendeleo mengi yamefanywa na Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Zanzibar kwa kujenga majengo ya kisasa ya kutolea huduma pamoja na kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini kupitia mradi wa TASAF, jambo ambalo limewakomboa na maisha duni.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mohamed Aboud Mohamed alieleza kuwa, Dk. Nchimbi ni mwadilifu, mwenye imani, anaependa watu na anajua mahitaji ya watu, hivyo atakuwa mshauri mzuri wa Dk. Samia.
"Dk. Mwinyi amefanya kazi ya kuwaunganisha wananchi, hivyo hakuna ubaguzi wa kidini, kijinsia, umoja na mshikamano umetawala visiwani hapa, lililobaki twendae tukapige kura ifikapo Oktoba 29 mwaka huu na tuwachague viongozi wetu," alisema Mjumbe huyo.
Mbunge mstaafu wa Arusha Sesilia Pereso aliwaomba wananchi kumchagua mama Samia pamoja na viongozi wengine wa CCM ili waongoze tena awamu ya pili kwa ajili ya kuwaletea maendeleo katika nchi.
Alisema, chama kimewaletea mama hodari, shupavu na ana sifa zote za kuongoza awamu nyengine, hivyo kila mmoja anapaswa kuweka kura ya ndio kwake ili awaletee wananchi maendeleo.
"Kazi alizozifanya mama Samia katika miaka minne iliyopita ni uthibitisho tosha kwamba ana uwezo wa kuongoza, kwa pamoja tuwapigie kura viongozi wa CCM ili watuletee maendeleo," alisema Mbunge huyo mstaafu.
Mbunge wa Jimbo la Gando Salum Mussa Omar na mwakilishi wa Jimbo hilo Maryam Thani Juma wamewataka vijana kutodanganywa na wasiopenda maendeleo bali wawachague viongozi wa CCM ili maendeleo zaidi yawafikie.
Walisema, kila kona yanaonekana maendeleo yaliyofanywa na chama cha Mapinduzi CCM, hiyo ni heshima kubwa kwa wananchi, hivyo ni vyema wakalipa fadhila kwa kuwapigia kura za nduo viongozi wa CCM.
"Nawahakikishia marais wetu watashinda kwa kishindo kwa sababu wananchi wameniambia kuwa kwa maendeleo wanayoyaona hakuna sababu ya kuikosesha kura CCM," alisema mgombea ubunge wa Gando.
MWISHO.
Comments
Post a Comment