NA AMRAT KOMBO, ZANZIBAR
Kila binadamu ana malengo maishani, lakini kuyatekeleza kunahitaji mipango thabiti na ujasiri wa kipekee. Kwa Laila Rajab Khamis, maarufu kama Laila, ujasiri huo umekuwa silaha kubwa iliyomfikisha kwenye nyanja za siasa na kumuwezesha kuwa miongoni mwa wanawake wachache wanaopigania nafasi za juu za uongozi Zanzibar.
Laila alizaliwa mwaka 1968 Kengeja, Pemba, akiwa mtoto wa tatu kati ya watoto kumi wa familia ya Mzee Rajab. Elimu yake ya awali ilifika darasa la kumi katika Skuli ya Uwelene. kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa mfanya biashara wa nguo mwaka 2000.
Hata hivyo, ndoto yake haikuishia kwenye biashara pekee, bali kuandika historia ya uongozi kama mwanamke jasiri. Safari yake ya kisiasa ilianza rasmi mwaka 2008 alipojiunga na chama cha NCCR-Mageuzi na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Rahaleo.
Hatua hiyo ilimfungulia mlango kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mlezi wa chama na hatimaye Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Zanzibar.
“Lengo langu kubwa ni kuwatetea wanawake na watoto katika masuala ya kijamii. Nimeona Rais Samia, mwanamke mwenzangu, ameweza kuiongoza Tanzania ,kwanini yeye asishiriki? Familia yake imesimama bega kwa bega naye licha ya tofauti za vyama.
“Mimi na mume wangu kila mmoja ana chama chake, lakini hajawahi kunidharau. Hunitia moyo na kunijenga zaidi. Hata mama yangu ameridhia hatua zangu na ananiombea kila siku,” anabainisha kwa furaha.
Laila amejijengea uwezo kupitia mafunzo ya uongozi na siasa kutoka taasisi mbalimbali za kimataifa. “Nafarijika kuwa katika chama ambacho kimewapa wanawake nafasi kubwa. Viongozi wanawake tupo sita, wanaume watatu. Hii imenitia nguvu zaidi,” anaongeza kwa kujiamini.
Mbali na siasa, Laila amekuwa mstari wa mbele kusaidia wajasiriamali wa ushonaji na vijana wa michezo. Hata hivyo, anakiri changamoto kubwa ni dhihaka kutoka kwa baadhi ya wananchi.
“Wengine hunikejeli kwa kugombea nafasi hii, lakini sijakata tamaa. Nitaendelea kupambana kwa sababu najua wapo wanaoniunga mkono,” anasisitiza. Matarajio yake sasa ni kushika nafasi ya urais na kutumia sera zake kuleta mabadiliko. “Nimejipanga kuwasaidia wanawake, vijana na watoto kwenye masuala ya kijamii na kiuchumi.
Vijana wanakabiliwa na tatizo kubwa la ajira, nami nimeweka mkazo mkubwa katika hilo,” anasema. Hata hivyo, Laila anakiri iwapo hatashinda hatakata tamaa, bali ataendelea kushiriki kwenye kinyang’anyiro kingine na kushirikiana na washindi kuhakikisha maendeleo ya Wazanzibari yanapatikana.
WANAOMFAHAMU LAILA
Mtumwa Ame Khamis, mkazi wa Fuoni, anaeleza: “Laila ni mwanamke aliyebeba ujasiri wa kugombea nafasi ya urais bila woga. Amejibika na hakuogopa kuingia kwenye kinyang’anyiro hiki na kuandika historia ya Zanzibar.”
Sheha wa Jimbo la Fuoni, Juma Mussa Juma, naye anaeleza: “Ninampongeza Laila kwa kujiamini na kujitoa kwake.
Hii itachochea wanawake wengine kuingia kwenye siasa na kugombea nafasi za uongozi. Laila ni mwanamke mchapakazi na hodari, na naamini anaweza kuleta maendeleo Zanzibar. Hata hivyo, Sheha huyu aliongeza kuwa kwa majukumu yake hana takwimu za wagombea wa uchaguzi, wawe wanawake au wanaume, kwa kuwa si jukumu la Sheha kujiweka mbele katika mchakato huo.
Pia, wagombea wenyewe hawana utaratibu wa kwenda kujitambulisha kwake, jambo linalomfanya abaki kando na masuala ya ushindani wa kisiasa.
Kwa upande wa chama chake, viongozi wameeleza kuwa kuibuka kwa mgombea mwanamke katika kinyang’anyiro cha urais ni hamasa kubwa kwa wanawake wengine. Wamefafanua changamoto kubwa kwa wanawake ni ukosefu wa elimu ya uongozi na hofu ya kujiamini, jambo linalozuia wengi kuingia kwenye siasa.
Naibu Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Ameir Mshindani Ameir, anaona ni muhimu serikali kurejesha ruzuku kwa wagombea kama ilivyokuwa mwaka 1995 ili kusaidia kampeni. “Katika kipindi hiki cha kampeni, ruzuku ingesaidia wagombea kupata nguvu ya kuendelea na harakati zao. Bila rasilimali za kifedha, mgombea anakosa nguvu ya kushindana kikamilifu,” anabainisha.
Licha ya changamoto zote, Laila ameapa kutokata tamaa. Ndoto yake kuu ni kushika nafasi ya juu ya uongozi na kuwa sehemu ya historia ya wanawake waliopigania maendeleo ya Zanzibar. Ujasiri wake, kujitolea na kujiamini kwake ni mfano wa kuigwa kwa kizazi cha wanawake wanaotaka kuandika historia zao za kisiasa.
Kwa kumbukumbu, katika uchaguzi wa mwaka 2020, wagombea wa nafasi ya uwakilishi walikuwa 251, ambapo wanawake walikuwa 61 na wanaume 190. Kwa upande wa madiwani walijitokeza wagombea 350, wanawake 74 na wanaume 276. Kwa mwaka 2025, Tume ya Uchaguzi Zanzibar bado haijatoa takwimu rasmi zinazoonesha jumla ya wagombea wa nafasi za uwakilishi, ubunge pamoja na udiwani.
Kwa sasa, jina la Laila Rajab Khamis limechukuliwa kama alama ya mabadiliko, uthubutu na uwekaji wa historia ya mwanamke katika siasa za Zanzibar. Changamoto zinaweza kujitokeza, lakini dhamira yake ya kupigania nafasi ya urais na kuwatetea wanawake, vijana na watoto inaendelea kumpa nguvu ya kusonga mbele.
MWISHO
Comments
Post a Comment