IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
KHADIJA Anwar Mohamed mwenye umri wa miaka 40 mkaazi wa Wawi Mgogoni ni mwanamke shupavu mwenye ndoto ya kuwa kiongozi tangu akiwa mdogo.
Aliamua kujiunga na chama cha CUF wakati huo ili kusudi apate nafasi ya kuwa kiongozi kwa lengo la kutatua kero za wananchi kwenye jamii iliyomzunguka.
Mwaka 2000 Khadija alianza kupata nafasi za uongozi katika chama chake, ambapo alijiona tayari anaenda kutimiza ndoto zake alizokuwa akiziwaza mara kwa mara.
Alianza kushika nafasi ya Mshikafedha wa tawi katika Jumuiya ya vijana na baada ya hapo ulifanyika uchaguzi kwenye chama na kufanikiwa tena kushika nyadhifa hiyo ya Mshikafedha lakini wa Jumuiya ya vijana kwenye jimbo.
"Kwa vile lengo langu ni kuwa kiongozi na kuwatetea wananchi maendeleo, sikufikia hapo bali niliendelea kushika nyadhifa mbali mbali ndani ya chama changu mpaka nimefikia pale ninapopataka," anaeleza Khadija.
Aliwahi kuwa Makamo Mwenyekiti mteule wa Kanda ya Pemba ambapo alikuwa anasimamia majimbo 18, hali ambayo iliendelea kumjengea ujasiri na kujiamini, huku akiamini wazi kwamba ipo siku ataingia kwenye vyombo vya maamuzi kuwatetea wananchi na kuwafikishia maendeleo.
Ilipofika mwaka 2019, wanachama wa CUF pamoja na viongozi wao walijiunga na chama cha ACT Wazalendo na baada ya kufanya uchaguzi, akabahatika kuwa Katibu wa Ngome ya Vijana Kusini Pemba na alikuwa anasimamia majimbo tisa (9).
"Baadae nikashika nafasi ya Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa ingawa baada ya hapo kutokana na umri wangu kutoka kwenye ujana, ilinibidi nigombee nafasi nyengine ambazo zinaniruhusu," anafafanua Khadija.
Alifanikiwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama Taifa, pia Naibu Waziri kivuli wa Mambo ya Ndani sambamba na Waziri kivuli wa Ulinzi.
Mama huyo alishikilia nafasi mbali mbali ndani ya chama, ndio alipoona sasa kuna haja ya kuingia kwenye vyombo vya maamuzi ili lengo lake la kuwatumikia wananchi aweze kulifikia.
"Nilijiona kuna nafasi nyingi nimeshikilia ndani ya chama changu, lakini nilisema kuwa bado lengo langu sijalifikia, hivyo lazima nipambane na ndipo nilipochukua fomu ya ubunge viti maalumu na kugombea," anasema.
Anaeleza kuwa, kura hazikutosha kwa upande wake kwa sababu kwenye majimbo wanawake wana tabia ya kusokotana sana, hivyo akatokea mshindi wa tatu, ingawa hakukata tamaa kwani kimpindi kilichofuata aligombea nafasi ya uwakilishi kwa upande wa Jimbo.
Ameshawahi kugombea nafasi hiyo mara mbili na zote kuibuka mshindi wa pili, ambapo mwaka huu kwa mara ya tatu amefanikiwa kuchaguliwa kugombea nafasi hiyo.
"Nilisema ni mwiko kukata tamaa, nikagombea tena uwakilishi mwaka huu wa 2025 na nashkuru sana wajumbe walinichagua kwa kura 82 huku wa pili yangu akiibuka na kura 52," anaeleza.
Alikuwa mwanamke pekee kati ya wagombea watano waliokuwa wakitafuta nafasi hiyo, ambapo aliwashinda wanaume wanne na ndipo alipopata nafasi ya kugombea ili kuishikilia nafasi hiyo kwenye Jimbo lake.
Khadija anahadithia kuwa, ilikuwa ni ngumu kuingia jimboni kugombea kutokana na wanaume kumkwaza kwa kile wanachodai kuwa, nafasi za wanawake ni viti maalumu pekee na za majimboni ni za wanaume tu.
"Kwa kweli walinishika nisigombee lakini niliwaambia kuwa nimeshaweka nia ya kugombea na nimeamua, kwa hiyo sipindishi kauli yangu na hasa kwa vile chama chetu kinazingatia jinsia, ndipo nilipopata nguvu zaidi ya kujiamini," anaeleza.
Ingawa alikosa mara mbili lakini hakukata tamaa ambapo mara ya tatu amefanikiwa kuingia kwenye mchakato wa kugombea na sasa anaendelea kuwaomba wananchi kura za ndio, ili aweze kuwaletea maendeleo katika Jimbo lake la Wawi Wilaya ya Chake Chake.
Mgombea huyo wa uwakilishi kupitia chama cha ACT Wazalendo anasema, hakupambana cha changamoto sana katika kugombea, kwani tayari alikuwa ameshajiamini, hivyo hakuna mtu aliemsikiliza kwa kumvunja moyo.
"Unajua changamoto zinakuja kutokana na udhaifu wetu wanawake, kwa sababu mtu akikuona dhaifu anakutumia kukuharibia lakini ikiwa umejiamini na umesimama imara, hakuna changamoto yeyote inayoweza kukuopelekesha," anafafanua.
Changamoto nyengine alizokumbana nazo ni kupigiwa, kudhalilishwa na kutolewa maneno ya kashfa, kwani katika jamii kuna watu wa vyama tofauti, hivyo kila mmoja anajiona yeye yuko sahihi kuliko mwenzake.
Anawataka wananchi wa Jimbo hilo wategemee mazuri endapo watamchagua na kuingia kwenye chombo cha maamuzi, kwani ni lengo lake kuwatumikia na kutatua changamoto zinazowakabili.
Anasema, wananchi wa Jimbo hilo wanatambua utendaji wake wa kazi na kusimamia ipasavyo majukumu yake, hivyo anaamini kuwa watamchagua ili aweze kwenda kuwatetea.
Mgombea huyo anasema, alipochaguliwa na wajumbe alifurahi sana kwani aliona wamemuamini na ndio maana wakamchagua kwenda kuwatetea na kuwaletea maendeleo wananchi.
"Lakini furaha ile inakatika ghafla pale unapoona kuwa kuchaguliwa kule ni kubeba dhima hapa Duniani na Akhera, hivyo akili yako yote unaipeleka kutumikia wananchi ipasavyo na sio kufurahia kwa kuwa umepitishwa kugombea nafasi hiyo," anasema.
Anaeleza kuwa, na utakapokumbuka kwamba umebeba dhima katika hilo, basi utafanya kazi kwa kuwa na hofu ya Mungu pamoja na kuwa na uadilifu, jambo ambalo utatekeleza vizuri majukumu yote waliyokutwisha wananchi wa Jimbo lako.
Khadija anasema, atapofanikiwa kuwa mwakilishi wa Jimbo hilo atajitahidi kuifikisha Wawi pale wanapoitaka wananchi kwa kuwa ya kimaendeleo zaidi.
"Kuna mwenzangu mwanamke ambae yupo Jimbo jengine, alinitaka ushuari kuhusu kugombea Jimbo au viti maalumu? nikamwambia tujitupe kwenye Jimbo, ingawa hakuwa na tamaa ya kupata lakini na yeye alifanikiwa na tayari yupo kwenye mchakato wa kugombea," anaeleza.
Anasema, wanawake wanaweza kugombea na kuleta mabadiliko makubwa endapo watafanikiwa, ingawa bado kuna baadhi yao wana hofu na ndio maana wanakimbilia viti maalumu.
Mama huo anasema, atakapochaguliwa kuwa mwakilishi, atafanya kazi zake za kuwatumikia wananchi na pia atafanya majukumu ya nyumbani bila kuathiri upande wowote.
"Majukumu ya nyumbani lazima niyafanye kama mke, mama na familia na majukumu ya kazi nitayafanya kadiri yatakavyokuwepo, nitajitahidi sitoathiri upande wowote," anaeleza.
Anaeleza kuwa, mume wake anamuunga mkono katika harakati zote za kisiasa, hivyo anapata nguvu zaidi ya kutokata tamaa.
Aliwataka wananchi wazidi kuwa na imani nae na wamchague kwa ajili ya kuongoza kwenye Jimbo hilo, ili kuwafikishia maendeleo zaidi.
Mume wa Khadija, Omar Ali Shehe anasema, anashirikiana na mke wake katika kuhakikasha anapata ushindi .
Anasema, mke wake ana uwezo mzuri wa kuongoza, ni jasiri na ana uthibutu, hivyo atakapopata nafasi ya kuongoza Jimbo, anaamini atawatimikia vyema wananchi wake.
Anasema kuwa, anamuunga mkono katika kila hatua kwani anamuamini na anajua lengo lake, hivyo anampa mashirikiano makubwa na ndio maana anafanikiwa hatua kwa hatua.
Katibu wa Habari, Mawasiliano na Uenezi katika Jimbo la Wawi Yussuf Maulid Issa anasema, Khadija ni mwanamke mpambanaji, asieyumba, asieogopa misukosuko na anaejali maslahi ya Jimbo lake.
Anamuelezea kuwa, Khadija amekuwa akisaidia mambo mbali mbali katika Jimbo lake bila kujali vyama, hivyo atapofanikiwa kushika nafasi ya uwakilishi, anaamini atatatua kero zilizomo kwenye Jimbo lake.
"Ameshawahi kuandaa kombe la kumuenzi Maalim Seif Sharif Hamad na kuzishirikisha timu zote za Jimbo na timu iliyopata ushindi ilikabidhiwa zawadi yake," anahadithia.
Mgombea huyo ameolewa na ana watoto na anapewa mashirikiano mazuri na familia yake katika harakati za kugombea nafasi za uongozi.
MWISHO
Comments
Post a Comment