NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar
Zubeir Ali Maulid, amewataka wananchi wa Mwambe wilaya ya Mkoani, kuyaenzi na
kuyalinda mapinduzi ya Zanzibar, kwani ndio mkombozi wa upatikanaji wa huduma
mbali mbali, ikiwemo elimu.
Spika Zubeir, aliyasema hayo leo Disemba 28, 2023 Mwambe wilaya ya
Mkoani, mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la skuli ya ghorofa mbili iliyopo
Chanjaani, ikiwa ni shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kabla ya Mapinduzi hayo, watawala walitoa huduma
hizo kwa matabaka na kuwafanya watoto wa wanyonge, kukosa huduma mbali mbali
ikiwemo elimu na matibabu.
Alieleza kuwa, madhila hayo na mingine ndio yaliyowafanya
waasisi wa Mapinduzi hayo, kuamua kufanya kila juhudi ili kuhakikisha
wanauondoa utawala uliokuwepo, ili kuwarejeshea heshima wazalendo.
‘’Leo tukiwa ndani ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar
wananchi wa Mwambe na maeneo mingine, tunayokila sababu ya kuyalinda, kuyaenzi
mapinduzi hayo, maana ndio ambayo sasa matunda yake tunayatumia,’’alieleza.
Akizungumza uwepo wa skuli hiyo ya ghorofa mbili,
aliwataka wananchi na waalimu, kushirikiana ili itowe wataalamu wa fani mbali
mbali, kwa ajili ya taifa lao.
Alieleza kuwa, serikali imetumia fedha nyingi katika ujenzi
wa skuli hiyo, sasa ili matunda yake yarudi serikali ni kuongeza ufaulu ambao
utasababisha upatikanaji wa wataalamu hapo baadae.
Alieleza kuwa, kumalizika kwa ujenzi wa skuli hiyo
mwanzoni mwa mwaka ujao, utakwenda kuondoa moja kwa moja mikondo mitatu, ambayo
hapo awali ilikuwa katika maeneo hayo ya Mwambe.
‘’Naelezwa kuwa, ndani ya miaka hii mitatu ya uongozi wa
Dk. Mwinyi, samba mba na miaka 60 ya mapinduzi, ndani ya jimbo hili la Kiwani, tumeshajenga
skuli tatu za ghorofa, ikiwemo za Mwambe na ile ya Kiwani,’’alieleza.
Hata hivyo, Spika huyo wa Baraza la Wawakilishi,
aliwataka wananchi wa Mwambe, kuitunza skuli hiyo mara itakapomalizika, ili
iweze kutumiwa na vizazi vijavyo.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wizara ya Elim una Mafunzo ya
Amali Zanzibar, Mwanakhamis Adam Ameir, alisema ujenzi wa skuli hiyo, ni miongoni
mwa mikakati ya serikali, katika kuweka elimu kipaumbele cha pekee.
Alisema, serikali ya awamu na nane, tokea ilipoingia madarakani
imeweka mikakati ya kuimarisha miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa skuli za
ghorofa, ili kupunguza msongamano wa wanafunzi
Naibu Katibu mkuu huyo alieleza kuwa, ujenzi wa skuli
kama hizo unamawanda mapana ya kuondoa mikondo mwili kwa skuli zote za Unguja
na Pemba, ili kuwapa waalimu nafasi nzuri zaidi za kufundisha.
‘’Kwa mfano hapa Mwambe, tulikuwa na mikondo mitatu,
lakini mwanzoni mwaka huu, tulishafungua skuli moja ya ghorofa na leo, tunaweka
jiwe la msingi skuli hii, iliyopo Chanjaani, haya yote ni kuona wanafunzi wanapata
muda wa kujifunza,’’alieleza.
Aliongeza kuwa, eneo la Mwambe kwa sasa lina skuli tatu
za msingi, ambazo zinajumla ya wawanafunzi wa msingi na maandalizi 4,658,
wakiwa na vyumba 68 vya kusomea.
“Lengo la serikali ni kuongeza vyumba zaidi vya kusomea,
ili kufikia lengo la serikali, la kuwa na wanafunzi 45 kwa kila darasa moja,’’alifafanua.
Kwa upande wake Naibu Waziri wizara ya Elim na Mafunzo ya
Amali, Ali Abdull-ghulam Hussein alisema ujenzi wa skuli hiyo, ni utekelezaji
wa vitendo, wa maana ya mapinduzi daima.
Alieleza kuwa, Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi
wakati akilihutubia Baraza la Wawakilishi, alieleza kutotaka hadithi ya
Mapinduzi, bali sasa ni kuwaonesha wananchi matunda yake.
‘’Ujenzi wa skuli kama hii ya Mwambe, tayari sisi wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Amali, wakati tukiadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi ya
Zanzibar, tumeshazijenga 21 kwa Unguja na Pemba, lengo ni kuondoa msongamano mdarasani,’’alifafanua.
Mapema Mkuu wa wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja,
alisema Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, yalifanyika ili kuwakomboa
wananchi na kupata haki zao.
Alieleza kuwa, sasa ndani ya miaka 60, watoto wa kinyonge
wanapata haki ya elimu, matibabu, maji safi na salama na hata miundombinu ya
barabara.
Ujenzi wa skuli hiyo ya ghorofa, ulianza Mei, 2023 na
unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwezi Januari 2024, ambapo inajengwa na
kampuni ya Mwinyi Bulding na kusimamiwa na wakala wa majengo Zanzibar ‘ZBA’ na
sasa umefikia asilimia 60.
Skuli hiyo yenye vyumba vya kusomea 29, vyoo 25, ofisi
nne za waalimu, ukumbi mmoja wa mitihani, maabara, chumba cha kompyuta na
maktba moja, hadi kukamilika kwake itagharimu shilingi bilioni 4.6.
Mwisho
Comments
Post a Comment