NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda
Zanzibar Omar Said Shaaban, amesema tayari serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
imeshatekeleza mambo makubwa kwa wananchi, ikiwemo miradi mbali mbali, yenye
tija ya moja kwa moja.
Alisema, ndani ya shamra shamra hizi za kuelekea miaka 60
ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni wakati kwa viongozi na wananchi kuyatangaaza mema
yaliokwishafanywa, ikiwemo ujenzi wa miundo mbinu ya barabara, afya elimu na
huduma za maji safi na salama.
Waziri Shaaban, aliyasema hayo leo Disemba 24, 2023 kwenye hafla ya uwekaji
wa jiwe la msingi la mradi wa utotoleshaji wa vifanga vya matango bahari, ikiwa
ni sehemu ya shamra shamra, za kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliyofanyika
shehia ya Dodo Pujini, wilaya ya Mkoani Pemba.
Alisema, kwa mfano ndani ya wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi,
wametafsiri kwa vitendo, maana ya Mapinduzi pamoja na yale maono ya Rais wa
Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, la kuweka mkakati maalum katika uwekezaji wa
bahari.
Alieleza kuwa, hivyo kila mmoja na kwa nafasi yake, anaowajibu
wa kusherehekea mafanikio ya Mapinduzi ya Zanzibar, ya mwaka 1964, kwani yapo
mafanikio ya wazi wazi, kwenye sekta mbali mbali ikiwemo uchumi na kijamii.
‘’Leo tukisherehekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar,
moja ya wizara iliyofanya vizuri kwa muda mfupi, ni hii iliyokuja kuanzishwa na
Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu, ambao sasa
wananchi wananeemeka,’’alieleza.
Alifafanua kuwa, Mapinduzi hayo ndio msingi wa utu, heshima,
mafanikio na maendeleo ya kila mmoja, hivyo ni wajibu wa kila mmoja, kuyalinda
na kuyaenzi, ili yazidi kuwakomboa wananchi.
Akizungumzia mikakati ya serikali, katika kuwandeleza
wananchi kupitia uchumi wa buluu na uvuvi, alisema ni pamoja na ufugaji wa mazao
ya baharini kama vile kaa, samaki na matango bahari.
‘’Ndio maana, ushirikiano wa serikali na wawekezaji wa
kituo hichi cha kutotoleshea vifaranga vya matango bahari wanaoitwa Mwambao MCC,
ni hatua kubwa na inahitajika kuendelezwa, kwa maslahi mapana zaidi,’’alifafanua.
Alisema serikali imejidhatiti kuendeleza wananchi kupitia
dira yake ya maendeleo ya mwaka 2050, pamoja na mipango ya maendeleo, ambapo
vituo kama hivyo, ni sehemu ndogo katika hilo.
Alifafanua kuwa, tayari serikali katika kutekeleza dira
hiyo kwa vitendo, imechimba mabwawa 100 ya ufugaji wa mtango bahari (majongoo
bahari), kwa idadi sawa, kati ya Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa, sasa ndio mwisho kwa wafugaji wa matango
bahari waliopo Pemba, kuagizishia vifaranga hivyo kutoka Unguja, baada ya
kuzinduliwa kwa kituo cha Pujini Dodo, wilaya ya Mkoani.
‘’Unguja kipo Bet-elrass ambacho kilikuwa kikihudumia
Unguja na Pemba, kwa kuzalisha vifaranga vya matango bahari, lakini kilichopo
Pujini, sasa kitasidia wakulima zaidi ya 500 walipo Pemba,’’alifafanua.
Mapema Katibu mkuu wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi
Zanzibar Aboud Suleiman Jumbe, alisema vitango baharini, ni bidhaa adimu na
dhahabu ya bahari, kwani soko lake ni katika nchi za China, Japan na Korea.
Hivyo aliwataka wananchi wa Zanzibar, kuchangamkia kilimo hicho, kwani kwa sasa, thamani ya soko kwa bidhaa hiyo duniani, inafikia dola za Marekani bilioni 10, ambapo kwa nchi za Afrika, 80 kila 100 zinazopakana na ukanda wa pwani, zinajishughulisha na kilimo, uuzaji usafirishaji wa matango bahari.
‘’Theluthi moja ya zao la matango bahari, kutoka nchi za
Afrika kwenda masoko ya nchi za China, Japan, Hong kong, Taiwan na Korea inatoka
magharibi wa ukanda wa hari ya hindi, inapopatikana pia Zanzibar,’’alifafanua.
Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa, mara baada ya Zanzibar kujenga
kituo cha kwanza cha kuzalishia vifaranga vya matango bahari mwaka 2017, na
kuanza ufugaji, uzalishaji na usafirishaji nje ya nchi, kisha mwaka 2019 kulisafirishwa
na tani 30 pekee.
‘’Usafirishaji huo, ulisita kwa ujio wa janga la Covid
19, mwaka 2020 hadi 2021 na kufikia tani 5.58, ingawa mwaka 2022 usafishaji
uliongezeka na kufikia tani 15, zenye thamani ya shilingi milioni 492.4,’’alieleza.
Aliongeza kuwa, uwepo wa mashamba 100 ya matango bahari
kwa Unguja na Pemba, kunatarajiwa kuongeza usafirishaji tani 45 hadi kufikia
mwishoni mwa mwaka 2024.
Nae Mkurugenzi Mtandaji wa shirika la MCC-Mwambao Said
Khalifa, alisema, wanatamani kuona jamii ya pwani, wanakuwa wasimamizi wazuri
wa rasilimali bahari, kwa maendeleo endelevu.
‘’Lengo la mradi huu ni kuisadia serikali kuu, katika
uchumi wa buluu, kwani ndio ambao kwa sasa, umepewa kipaumbela kama sekta
kiongozi,’’alifafanua.
Alieleza kuwa, kituo hicho kina mpango wa kuzalisha vifaranga
zaidi ya 5,000 kwa mwezi, sawa na mashamba matano, ambapo tayari kwa awamu ya
kwanza, walizalisha mayai milioni 1, na kukuza vifaranga 4,000, na kisha kupata
1,035 na 1,1500 ndio wamefakiwa kuviuza.
‘’Kwa awamu ya pili, tunavyo vului lui wastani wa milioni
2.1, vilivyozalishwa, ambavyo kwa sasa viko hatua ya kulelewa, na kisha vitawekwa
kwenye eneo maalum, kabla ya kuwa vifaranga kamili kwa ajili ya kuuzwa,’’alifafanua.
Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud,
alisema uwepo wa kituo hicho, ni ishara ya utekelezwaji wa kwa vitendo, maana halisi
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ujenzi wa kituo wa kutotolea matango bahari, umeanza
mwezi Machi mwaka huu na kumalika mwaka huu, ambapo jumla shilingi milioni 55,
kutoka shirika la moja lililoko Marekani, ndio zilizotumika.
Kisha uwekaji mitambo maalum na ya kisasa ulifuatia, na
kugharimu shilingi milioni 90, uwepo wa
mashine za kuvutia maji baharini, ujenzi wa barabara ya kuingia kituoni hapo
kwa njia ya kifusi.
Ufunguzi wa miradi ya Mapinduzi ya Zanzibar, utasita kwa siku mbili na kuendelea tena Disemba 27, kwa ufunguzi wa miradi miwili ukiwemo wa soko la samaki na mboga Machonne Chake chake na Ufunguzi wa ghala la la chakula na vifaa vya ujenzi Kinyasini wilaya ya Wete.
Mwisho
Comments
Post a Comment