NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@
MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar Othman
Massoud Othman, amesema Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ndio yaliotengeneza
mwanga, na kisha kufungua milango ya fursa sawa kwa wote, ikiwemo elimu bila ya
ubaguzi.
Alisema, Mapinduzi hayo ndio yaliyojenga ngome ya uhakika
kwa kila mzanzibari, katika kupata elimu, matibabu na huduma nyingine za kijamii
bila ya ubaguzi wowote.
Makamu huyo wa Kwanza, aliyasema hayo leo Disemba 30, 2023 Kisiwa cha
Kojani wilaya ya Wete Pemba, mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la skuli
ya ghorofa ya msingi ya Kojani, ikiwa ni shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi
ya Zanzibar.
Alisema, ujenzi wa skuli hiyo pamoja na nyingine, ni
mkakati endelevu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wa kuhakikisha inawapatia
wananchi wake haki ya elimu, waliyoikosa kabla ya Mapinduzi.
Alieleza kuwa, elimu ndio msingi wa uhakika wa maendeleo ya
mwanadamu, na ndio maana hata Muumba katika kuwaumba wanaadamu, kuliambatana na
tendo la kupewa elimu.
Alisema msingi wa elimu, kama inavyofanya serikali kwa
kuwekeza miundombinu ya kisasa, ndio inayomtofautisha mwanaadamu na viumbe vyingine
duniani.
‘’Kuimarika kwa sekta ya elimu na miundombinu yake,
kumekuwa kukishuhudia kukua mwaka hadi mwaka, na haya hasa ndio azma na malengo
ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964,’’alieleza.
Aidha Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman
Massoud Othman, alisema kuwa, kwa kule serikali kutambua umuhimu wa haki ya elimu,
imeweka kwenye dira yake ya 2050, ikiwa na dhima ya kujenga nguvu kazi, yenye
ujuzi, ubunifu na uwezo wa kuchangia katika uchumi wa taifa.
Alifahamisha kuwa, moja ya vipaumbele vya kwanza ndani ya
serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni elimu na ndio maana, imemshapitisha
mpango mkubwa wa mageuzi ya elimu, hapa visiwani.
‘’Mpango huo unazo nguzo kadhaa, ikiwemo kuimarishwa kwa
miundombinu ya elimu, ambayo yatamuwezesha mwanafunzi kusoma kwa mujibu wa
mahitaji ya kisasa,’’alifafanua.
Hivyo Makamu huyo wa Kwanza, alifahamisha kuwa, ujenzi wa
skuli hiyo, unakwenda samba mba na mipango na mikakati ya muda mrefu ya
serikali, katika mageuzi ya elimu.
‘’Uwekaji wa jiwe la msingi la skuli hii, ni kielelezo tosha,
cha dhamira thabiti ya serikali, kupitia wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,
katika kutekeleza kwa vitendo, mageuzi ya elimu,’’alieleza.
Aidha alisema skuli hiyo ya Kojani ni moja,
lakini tayari serikali kupitia wizara husika, inaendelea na ujenzi wa skuli
nyingine 25, katika mwaka huu, tano kati ya hizo zikiwa mkoa wa kaskazini
Pemba.
Alieleza kuwa skuli hizo ambazo ni za kisasa ni pamoja na
Kojani, Konde, Kifundi, Utaani pamoja na ile ya Maziwang’ombe , ambazo
zinatarajiwa kuanza kutumiwa, kuanzia mwakani.
‘’Kumbukeni kuwa, ujenzi wa skuli hizi za kisasa kwa
Unguja na Pemba, serikali imeshajiwekea shabaha, ili kuona kila darasa halizidi
wanafunzi 45, pamoja na kuwa na mkondo mmoja wa wanafunzi,’’alisema.
Alisema, licha ya ongezeko la idadi ya watu wa Zanzibar kutoka
milioni 1.3 hadi kufikia watu milioni 1.8, sawa na ongezeko la wananchi wa Kojani,
waliokuwa 4,536 kwenye sensa ya mwaka 2012 hadi kufikia 8, 475 kwa sensa ya mwaka
2022.
Wakati huo huo Makamu huyo wa Kwanza, amewataka wazazi na
walezi, kuhakikisha hakuna mtoto, ambae amefikia umri wa kuandikishwa masomo na
kubakia nyumbani.
Mapema Katibu mkuu wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar, Khamis Abdalla Said, alisema skuli hiyo inajengwa kwa fedha za serikali
na hadi kukamilika kwake, itagharimu shilingi bilioni 3.382.
Alieleza kuwa, skuli hiyo itakuwa na madarasa ya chini ‘ground floor’ kisha ghorofa mbili za juu, pamoja na kuwekewa miundombinu yote ya kisasa, kwa ajili ya wanafunzi.
Katibu mkuu huyo alifafanua kuwa, ndani ya skuli hiyo
kutakuwa na vyumba 34, ofisi tatu za waalimu, ukumbi wa mitihani, maabara, ofisi
ya TEHAMA, maktaba na stoo.
‘’Shabaha ya ujenzi wa skuli kama hizi za ghorofa, kwanza
ni kuongeza kiwango cha elimu, kuondoa mikondo miwili pamoja na wanafunzi
kuwepo 45 kwa darasa moja,’’alieleza.
Alifamisha kuwa, skuli ya sasa ya Kojani inayotumika,
inavyo vyumba 19, yenye wanafunzi 2,802 ambapo kati ya hivyo, vyumba vitano
vinatumiwa na wanafunzi 430, wastani wa wanafunzi 86 kwa darasa moja.
‘’Vyumba vya msingi ni 14 vinavyotumiwa na wanafunzi 1,942
sawa na wanafunzi 139 kwa darasa moja, jambo linalosababisha kuingia mikondo
miwili,’’alieleza.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Salama
Mbarouk Khatib, amewataka wananchi wa Kojani, kuthamini juhudi za serikali, katika
kuitunza miundombini ya elimu.
Hata hivyo, amepongeza Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali
Mwinyi, kwa kueteleza kwa vitendo, ahadi yake kwa wananchi wa Kojani, juu ya ufinyu
wa nafasi za kusomea kwa watoto wao.
Mwisho
Comments
Post a Comment