Skip to main content

MIKATABA YA KUWAINUA WANAWAKE IMEACHWA NYUMA

 



NA ASIA MWALIM, ZANZIBAR@@@@
                                      
NCHI nyingi zimeridhia mikataba na matamko ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kwenye uongozi na nafasi za maamuzi kama ilivyoainishwa katika Tamko la Haki za Binadamu la 1948.
 
Zanzibar imesaini mikataba ya kikanda na kimataifa, lakini safari ya utekelezaji ni ndefu kwa sababu hadhi sawa  kwa wanawake na wanaunme katika uongozi haipo na hii inaonekana katika shehia, wadi, majimbo, wadi hata taifa kutokana na kutokuwepo fursa sawa katika kugombea uongozi.
 
Mara nyingi unapofanyika uteuzi nafasi wanazopewa wanawake huwa hazina hadhi sawa na zile wanazokabidhiwa wanaume na hii inapelekea wanawake kuwa na wakati mgumu kufikia malengo yao na ndio maana upo umuhimu wanawake kupaza sauti zao kutaka mabadiliko.
 
Vyama vya siasa navyo vinawaacha nyuma wanawake katika kuwapa nafasi za kugombe kama, inavofanyika kwa wanaume na jina la mwanamke likipita huwa kama bahati. Matokeo yake ni  kuwa zaidi ya robo tatu ya viongozi ni wanaume.
 
Katika uchaguzi wa 2020, wanaume walioteuliwa na vyama kugombea kuingia katika Baraza la Wawakilishi (BLW) walikua 190 na walioshinda ni 42 wakati wanawake walikuwa  61 na walioshinda ni wanane.
 
Kutokuepo sheria inayowataka wanaume na wanawake kupata fursa sawa ya kugombea uongozi wa kuchaguliwa katika majimbo kumechangia kuwepo wanawake wachache.
 
Taarifa za Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN Women) na Umoja wa Mabunge (IPU) za 2017 zimeonesha kuwepo ongezeko dogo la viongozi wanawake katika serikali na mabunge katika nchi nyingi.
 
Katika mahojiano maalum viongozi na wanachama wa vyama vya siasa Zanzibar  walisema  sababu zinazochangia ni kuwepo mfumo dume na mitazamo  ya kibaguzi na mgawanyo wa kijinsia wa majukumu katika vyama.
 
Uwakilishi wa wanawake kwa udiwani, uwakilishi na ngazi za juu ni changamoto, licha ya juhudi  za kutafuta mabadiliko na kuelezwa dhamira ya kufikia nusu kwa nusu ya wanawake na wanaume.
 
 
Katika majimbo 50 wanawake katika BLW ni wanane (asilimia16), wabunge ni  wannne (asilimia 8), mawaziri ni sita (asilimia 33) na Makatibu Wakuu ni saba (asilimia 39).
 
Kati ya wakuu wa mikoa watano Unguja na Pemba, mwanamke ni mmoja tu na kati ya wakuu wa wilaya ni wanawake wanne na masheha wanawake ni 81 kati ya 388.
 
 MTAZAMO WA VYAMA VYA SIASA
 
Mwakilishi wa Dimani, Mwanaasha Khamis Juma, alisema hali sio mbaya kwa viongozi wa chama chake cha CCM na serikali katika kuteua wanawake kuwa viongozi, lakini bado haitoshelezi kwani ongezeko la Wawakilishi wanawake ni kuwa wanane hivi sasa kutoka saba mwaka 2015.
 
Alisema wanaume waliogombea wakilishi walikuwa 190 na walioshinda 42 na wanawake waliojitokeza  walikuwa 61 na walioshinda ni wanane na kwahivyo  haja kwa wanawake kujiandaa vyema kwa uchaguzi wa mwaka 2025 ili idadi yao iongezeke katika BLW.
 
Mbunge wa Kiembesamaki, Muhammed Maulid, alisema sera ya CCM na katiba yake zinazingatia jinsia na muda chama kinahamasisha wanawake kugombea uongozi katika, Bunge, BLW na nafasi nyengine katika serikali ya Zanzibar na ya Muungano.
 
 
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, alisema chama hicho kinafuata sheria na mikataba iliyoridhiwa na kusistiza hakina mfumo dume na kutoa mfano wa sekretieti ambayo ni chombo kikubwa kuwekewa uwiano wa wajumbe, wanaume 10 na wanawake 10.
 
Naibu Mkurugenzi kutoka ADC, Mtumwa Faiz Sadik, alisema ili kuzipatia ufumbuzi changamoto wanazopitia wanawake ni lazima kuwepo mipango mizuri ya kutekeleza mikataba na maazimio ya kimataifa.
 
Mchakato wa kuwania uongozi kwa uchaguzi wa mwaka 2020 kwenye majimbo wanawake walihamasika na kufikia takriban 400  kutoka katika  vyama  vya siasa na hasa CCM, CHADEMA,  NCCR mageuzi, na ACT Wazalendo.
 
WIZARA YA MAENDELEO, JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO
 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar, Abeda Rashid alisema, licha ya changamoto ziliopo, wanawake wamenufaika na fursa za uongozi ndani na nje ya vyama vya siasa na zipo nafasi muhimu katika taasisi za serikali zinazoshikiliwa na wanawake.
 
Kwa mara ya kwanza nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuongozwa na yeye akiwa mwanamke mwenye ulemavu.
 
Alisema pia wapo walioteuliwa kushika nafasi muhimu, akiwemo Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee wanawake na Watoto, Anna Atunas.



 
 “Kwa sisi watu wenye ulemavu tunashukuru serikali haijatuacha nyuma na tunampongeza Rais, Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuwaona wenye ulemavu na kuwaamini katika nafasi kama hizo za uongozizao” alisema.
 
Aliwapongeza wadau maendeleo na taasisi mbali mbali kwa kuwa mstari wa mbele kuwashirikisha wanawake kwenye mafunzo ya kuwezesha kuwa viongozi.
 
TAKWIMU ZA UCHAGUZI 2020. 
Katika uchaguzi mkuu wa 2020 watu walioteuliwa na vyama kugombea ubunge kwa upande wa Zanzibar ni  wanaume ni 257 na walioshinda 46 na  wanawake walikua 81na walioshinda wanne.
 
Kwa BLW walioteuliwa walikua wanaume 190 na walioshinda 42 ambapo wanawake walikuwa  61 na walioshinda ni wanane na wanaume walioteuliwa na vyama kugombea udiwani ilikua 276 na walioshinda 85 ambapo wanawake walikua 74 na walioshinda ni 25.
 
KINACHOKWAMISHA USAWA
Kiongozi mmoja wa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa upande wa Zanzibar, Tunu Juma Kondo, alisema ipo haja ya kuzingatia usawa kwenye uongozi kati ya wanawake na wanaume na kusisitiza kwamba hivi sasa wanawake wameelimika, wanafahamu mambo ya siasa, uchumi na maendeleo, pia wanaendelea kujifunza kutoka kwa viongozi wa ndani na nje ya nchi na wale walioshika nafasi za uongozi wameonesha uwezo mkubwa wa kutumikia wananchi.


 
Mfano mzuri ni wa Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye anaifanya kazi yake kwa bidii kuimudu nyadhifa hioo kuu nchini kwa uadilifu mkubwa,
 
Kutokana na kutouwepo sheria inayotaka kuwepo ursa zenye hadhi sawa kwa wanawake na wanaume kunaifanya nchi kutotekeleza kwa ufanisi baadhi ya  mikataba iliyoridhia inayohusu usawa katika uongozi.
 
 
NINI KIFANYIKE.
Daktari Ananilea Nkya, mwanaharakati maarufu wa haki za wanawake, ameishauri serikali kupitia sheria  za uchaguzi na kuweka kipengele kinachovitaka vyama vya siasa kuteua idadi sawa ya wanawake na wanaume kugombea katika kata, majimbo, uwakilishi na ngazi nyengine za uongozi.
 
Alitaka nafasi za viti maalumu kwa wanawake ziondolewe na wapewe watu wenye mahitaji maalumu kwani katika zama hizi wanawaeke wa Tanzania wameshathibitisha kwa vitendo wanaweza kugombea majimboni na kushinda na kuongoza kwa ubora wa kiwango cha juu.
 
 
Hata hivyo Dk. Nkya alishauri wanawake  kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa mwaka 2025 na sio kusubiri nafasi za uteuzi ili waweze kuwa viongozi kwani viti maalumu kwa wanawake havina hadhi sawa na vile vya kuteuliwa majimboni.
 
Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) kwaa Zanzibar, Dk Mzuri Issa Ali, alisema umefika wakati kuondoa vikwazo vinavyokwamisha hadhi sawa kwa wanawake na kuwataka viongozi wa vyama vya siasa kuweka sheria rafiki zitakazotoa muongozo wa nafasi za uongozi na sio kugawa nafasi za uteuzi kama zawadi. 
 
Alisema kutokana na hali ilivyo katika vyama vya siasa ipo haja ya vyamao kulazimishwa kuwa na usawa wa 50 kwa 50 kwenye vyombo vyao vyote vya maamuzi ili wanawake wapate nafasi za majimbo.

 


"Bado vyama vya siasa havijazingatia usawai, kuanzia kwenye sheria, uchaguzi ndani ya vyama na majimboni, mbali ya kupokelewa vizuri na sio kwa uadui" aliongeza.
 
Alisema TAMWA, kwa kushirikiana na wadau wengine, kama Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na PEGAO ) imekua ikitoa mafunzo ya uongozi mara kwa mara kwa wanawake ili kuhakikisha wanapata haki sawa katika nafasi za uongozi wa kuchaguliwa. 
 
Tanzania, kwa mara ya kwanza ilipata Rais mwanamke, Mama Samia, miaka miwili iliopita na kwa mara ya kwanza katika historia  Bunge la 10 la Jamhuri Muungano lilipta Spika mwanamke, Anna Makinda kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 na kufuatiwa na Dk. Tulia Akson Mwansasu ambaye ndiye Spika  wa sasa na Spika wa Bunge na kuchaguliwa mwezi Oktoba, mwaka huu kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge ya Dunia (IPU).
 
Zanzibar kwa mara ya kwanza imepata muhandisi mwanamke, Zena Ahmed Said,  ambae ni Katibu Mkuu kiongozi Katibu wa Baraza la Mapinduzi kupitia serikali ya awamu ya nane.
 
KATIBA YA ZANZIBAR
 
Katiba ya Zanzibar ya 1984, imeweka wazi kuwa kila Mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu na yanayohusu taifa lake na katika marekebisho ya 2010 imeeleza kutakuwa na wajumbe BLW kwa idadi ya asilimia 40 wa wajumbe kwa kila jinsia.
 
TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR (ZEC)
Katika kuhakikisha wanawake na makundi yaliyo pembezoni haki zao zinazingatiwa katika michakato ya demokrasia na uchaguzi wa mwaka 2015 ZEC ilitengeneza sera ya jinsia ili uhakikisha kuwepo ushiriki na uwakilishi sawa wa raia wote, lakini  haikuzingatiwa ipasavyo utekelezaji wake katika vyama vya siasa.
 
DIRA NA SERA ZA ZANZIBAR
Aidha Dira ya Zanzibar ya 2050 imeelezea jinsi gani masuala ya usawa wa jinsia juu ya kuondoa unyanyasaji na kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wanawake, ikiwa pamoja na kuinua na kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake.
Vile vile imelenga kuongeza fursa na kuwawezesha katika vyombo vya kutoa maamuzi na kwenye shughuli za uchumi, kijamii, siasa, ngazi za utawala na huduma za sheria.
 
Sera ya jinsia inaeleza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya utoaji maamuzi katika ngazi zote ni mdogo na kwahivyo serikali, kwa kushirikiana na wadau wengine, itafanya juhudi kuona makundi yote na yaliyopembezoni yanapata fursa hiyo.
 
MIKATABA NA ITIFAKI
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC)  ambayo mkataba wake ulitiwa saini mwaka 2008 inaeleza kutaka kuondoa utafauti na kuwatenga wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo na kusaidia kuwepo usawa wa kijinsia katika nchi wanachama na kufikia asilimia 50/50 kwenye  maamuzi, serikali na taasisi binafsi.
Vile vile yapo makubaliano yanayojulikana kama Itifaki ya Maputo ambayo yalifanyika kule Msumbiji mwaka 2003 ambayo inacho kipengele kinachoonyesha haki ya wanawake kushiriki katika siasa na  mchakato wa vyombo vinayofanya maamuzi.
 
Mkataba mwengine ni ule wa kimataifa unaojulikana kama (CEDAW) wa 1979 ambao unapinga aina zote za udhalilishaji na kusisitiza ushiriki wa wanawake katika siasa na maisha ya kijamii.
 Mengine yalyoelezwa kuwepo usawa  wa kushiriki kwa wanawake wanaume katika uchaguzi, mchakato  wa upigaji kura na kushika madaraka.
, kwa mantiki hiyo basi CEDAW ni mkombozi kwa wanawake katika Nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
 
MIKATABA KWA NJIA HII
 
Kwa mfano itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) mkataba wake wa kikanda uliotiwa saini  mwaka 2008 na nchi wanachama wake ikiwemo Tanzania, wenye vifungu 43 unaelekeza nchi hizo kuzingatia suala la haki na usawa kati ya wanaume na wanawake katika suala la uongozi.
 
Kifungu cha nambari 12 kinasisitiza ushiriki sawa wanawake na wanaume kufikia asilimia 50/50 kwenye Nyanja za maamuzi, serikalini na taasisi binafsi.
 
Katika Itifaki ya Maputo ambayo makubaliano yake yalifanyika tarehe 11, Julai 2003 nchini Msumbiji, kipengele nambari 9 kinahimiza ushiriki sawa wa wanawake na wanaume katika siasa na vyombo vya kutoa maamuzi.
 
Aidha jukwaa la Mpango wa Utekelezaji wa Beijing mwaka 1995 kifungu nambari 7 kinataka ushiriki katika vyombo vya maamuzi kwa kuzingatia uwiano wa kijinsia kwenye ngazi zote za uongozi.
 
Pia mkataba wa Kimataifa unaopinga aina zote za udhalilishaji (CEDAW) wa mwaka 1979, kifungu chake cha 7 kinaeleza umuhimu umuhimu wa wanawake kushiriki katika siasa na kuwa na haki sawa ya kushika madaraka.
  
Kwa mukhtadha niliouleelezea kwa urefu i ni wazi kuwa mikataba ya kikanda na kimataifa haijazingatiwa vyema hapa nchini katika kutoa fursa sawa ya uongozi kati ya wanaume na wanawake. 
 
mwisho
 

Comments

BLOG'S VISITORS

DAKTARI MWENGINE CHAKE CHAKE KULA SIKUKUU POLISI, NI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MGONJWA WAKE

NA WAANDISHI WETU, PEMBA::: DAKTARI anaetoa huduma kwa wagonjwa kituo cha afya cha serikali cha  Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, Is-haka Rashid Hadid, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16, mkaazi wa Gombani. Daktari huyo miaka 35 ni mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani. Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa, April 21 mwaka huu alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu. Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms) kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo alizikosa hospitalini hapo. "Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele katika sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje da

'MKAPA' NA WENZAKE PEMBA WALAZWA RUMANDE

  NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@ MAHKAMA kuu Zanzibar kisiwani Pemba, chini ya Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, imewapeleka rumande watumuhimwa wanne wanaokabiliwa na tuhuma za kuua kwa makusudi, akiwemo Ali Mussa Omar ‘ Mkapa’ mkaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake Pemba. Watuhumiwa wengine walioanza maisha mapya ya rumande ni mtuhumiwa Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari Mussa Omar miaka 30 pamoja na mtuhumiwa Yassir Mussa Omar ‘ Makababu ’ miaka 29, wote wakaazi wa shehia ya Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba. Awali watuhumiwa hao waliwasili mahakamani hapo, kwa mara ya kwanza, kwa ajili ya kusomewa tuhma zinazowakabili za kumuua kwa maksudi Said Seif Kombo. Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Seif Mohamed Khamis akiambatana na mwenzake Mussa Khamis Ali kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaia kufanya mauwaji hayo kwa maksudi. Ilidai kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo Oktoba 16, mwaka huu, baina ya saa 7:00 mchan

HII KALI MBUNGE ASIYA AMKOGESHA MWANANCHI HADHARANI KISA HICHI HAPA......

  NA HAJI NASSOR, PEMBA MBUNGE wa viti maalum nafasi za wanawake mkoa wa kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka wananchi wa kijiji cha taifu, shehia ya Kinyasini jimbo la Gando wilaya ya Wete Pemba, kuyalinda miundombinu ya maji safi na salama, ili yawe endelevu kwao. Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kuwasili kijijini humo, na kumkogesha mwananchi mmoja kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama, ulioasisiwa na mbunge wa Jimbo la Gando. Alisema, hawana mbadala kwa sasa bali ni kuilinda miundombinu ya huduma hiyo, hasa baada ya mbunge wa wao Salim Mussa Omar, kuwarejeshea huduma hiyo. Alieleza kuwa, inafahamika kuwa kwa miaka 14 waliikosa huduma hiyo hasa kwa vile viongozi waliokuwepo hawakujali kuwatatulia tatizo hilo, hadi juzi ilipofanywa na mbunge wao. “Baada ya huduma hii sasa kurejeshwa na mbunge wa jimbo la Gando, kazi iliyobakia kwenu wananchi ni kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii,’’ali

TUHMA ZA DAKTARI PEMBA KUCHIWA HURU: POLISI KASKAZINI KUTOA TAARIFA RASMI LEO

  NA HAJI NASSOR, PEMBA KAMANDA wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, amesema leo Mei 9, mwaka huu atatoa taarifa rasmi, juu ya kuendelea kumshikilia au kumpa dhamana ya Polisi, daktari wa Kituo cha Afya Gombani Is-haka Rashid Hadid, anayetuhumiwa kwa ubakaji. Alisema, kwa vile alikuwa katika mapumziko mafupi, haelewi jambo lolote linaloendelea kwa mtuhumiwa huyo, juu ya kuendelea kushikiliwa kwake kituoni hapo. Alieleza kuwa, leo Mei 6 (jana), hajapata taarifa za ndani za mtuhumiwa, huyo na kuwataka wananchi na wanaharakati, wasubirie hadi Jumatatu ijayo. Akizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Kamanda huyo, alisema hana taarifa zozote za kupewa dhamana mtuhumiwa ndani ya kituo chake cha Polisi au kuendelea kuwepo. ‘’Ilikuwa mimi sipo kazini kwa muda, kuanzia anakamatwa hadi anafikishwa Polisi, kwa sasa siwezi kueleza jambo lolote kwa mtuhumiwa huyo, hadi Jumatatu,’’alieleza. Aidha Kamanda huyo alieleza kuwa, kwa sasa hawezi kutoa ufafan

MADAKTARI KUTOKA CHINA WAOKOA MAISHA YA MTOTO PEMBA

  HABIBA ZARALI, PEMBA TIMU ya 32 ya madaktari wa kichina katika hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani wamefanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa mtoto mwenye umri wa miaka 15 mkaazi wa Chole Kengeja, baada ya kuchomwa na jiti sehemu ya njia zake za mfumo wa uzazi. Mtoto huyo ambae alianguka hivi karibuni katika mti na baadae kuchomwa na jiti hilo na kumsababishia kutokwa na damu nyingi katika sehemu ya nyonga, alifanyiwa upasuaji uliodumu kwa muda wa saa tatu na   kuokolewa maisha yake. Akizungumza mara baada ya operesheni huo kiongozi wa timu hiyo Dr Jiang Jinhua, alisema mara baada ya mtoto huyo kufikishwa hospitalini hapo na kufanyiwa vipimo na kuonekana   ilibidi apatiwe rufaa ya kwenda katika hospitali nzuri yenye kutibu tatizo lake huko nchini Kuwado ambapo haikuwezekana kutokana na hali ya umaskini wa f amilia ya mtoto huyo . Alisema timu ya madaktari hao itaendelea kutowa huduma za matibabu   kwa wananchi kisiwani humo,   ili kuwaondolea gharama ya kutafuta matibabu nje ya nch