NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar Othman Massoud
Othman, amesema maono ya muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, mzee Abeid Amani
Karume, yanaendelea kutekelezwa kwa vitendo, ndani ya awamu ya nane, inyoongozwa
na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Makamu huyo wa Kwanza, aliyasema hayo leo Disemba 29, 2023 shehia ya Mgelema
wilaya ya Chake chake Pemba, mara baada ya uzinduzi wa barabara ya Kipapo-
Mgelema, ikiwa ni shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema, ujenzi wa barabara za kisasa, skuli, miundombinu
ya maji safi na salama na matayarisho ya ujenzi wa viwanja vya ndege na utanuzi
wa bandari, yanayotekelezwa sasa, ndio azma na maono ya wasisi wa Mapinduzi.
Aleleza kuwa, kila mmoja anayosababu ya kufurahia na
kushangilia yanayofanywa sasa, na yale yaliokuwepo kabla, kwani yanalenga moja
moja kutatua changamoto za wananchi.
Alifafanua kuwa, ujenzi wa bara bara ya Kipapo– Mgelema na
nyingine, ni mifano mizuri ya jitihada za serikali ya awamu ya nane, ambayo
yanakwenda sambamba na shabaha ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
‘’Leo tukiadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar,
kila mmoja anayofuraha, maana yapo mingi yameshatekelezwa, kwa mfano barabara
hii ya Mgelema, kila mmoja alikuwa shahidi jinsi ilivyokuwa hapo kabla’’alifafanua.
Aidha Makamu huyo wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Massoud
Othman, amewataka wananchi wanaotumia barabara hiyo, kuilinda na kuienzi, ili
itumike kwa muda mrefu ujao.
Alieleza kuwa, barabara ndio kichecheo pekee cha kukuza
na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na serikali kuu, hivyo ni wajibu, kuilinda
miundombinu yake.
Hata hivyo, amewakumbusha wananchi wa Pemba, kuwa tayari
serikali imeshasaini mikataba mbali mbali na kampuni tofauti, juu ya ujenzi wa
bara bara kuu na zile za ndani.
‘’Hapa nichukue nafasi ya kuipongeza wizara husika, kwa
juhudi zao mbali mbali, ambazo zinaonekana kwa vitendo, katika kuwakwamua
wananchi, na sio tu kwa usafiri, bali hata kwa usafirishaji wa mazao yao na
bidhaa nyingine,’’alieleza.
Wakati huo huo, Makamu huyo wa Kwanza, ameitaka jamii
kuendelea kupanda miti na kukirejeshea uasili wake, kisiwa cha Pemba, ambacho
kilikuwa kimezungumkwa na miti mikubwa.
Aidha ameitaka jamii, kutokuwa sehemu ya kuendeleza na
kukuza vitendo vya udhalilishaji na ukatili kwa wanawake na watoto, kwani nao wanahitaji
kulindwa, ili wawe viongozi wema hapo baadae.
Katibu Mkuu wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
Zanzibar Khadija Khamis Rajabu, alisema ujenzi wa barabara hiyo ya Kipapo-
Mgelema yenye urefu wa kilomita 5.3, ujenzi wake uligawika katika awamu mbili, ambapo
moja wapo ni ujenzi wa Kipapo –Mgelema na kisha Mgelema- Wambaa yenye urefu wa
kilomita 4.
Alieleza kuwa, ujenzi huo ulianza mwezi Novemba mwaka 2020,
na ukitarajiwa, kukamilika mwaka mmoja baadae, ingawa kutokana na sababu za mbali
mbali, umekamilika Disemba mwaka huu.
Aidha Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa, barabara hiyo ina upana
wa mita sita, na mabega {road shoulder} yenye upana wa 0.5 kwa
kila upande, na ujenzi wake umetumia mfumo wa lami moto.
‘’Kwa sasa bara bara hii, inazo daraja ndogo {culvert}
sita na daraja moja kubwa, na imeshawekewa alama za barabarani, kwa ajili ya vyombo
vya moto, watembea kwa miguu na ina uwezo wa kupitisha gari zenye uzito usiozidi
tani 10,’’alifafanua.
Alieleza kuwa, kama barabara hiyo ya Kipapo- Mgelema
itatunzwa inaweza kuishi kwa wastani wa miaka 10, bila ya kuharibika, wala
kufanyiwa matengenezo yoyote.
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa, ujenzi wa barabara hiyo,
hadi kukamilika kwake, umeshatumia zaidi ya shilingi bilioni 2.109, fedha
zilitolewa na serikali ya Mapinduzi, kupitia Mfuko wa Bara bara na imejengwa na
Wakala wa Barabara Zanzibar.
Akizungumzia fidia za vipando na makaazi ya wananchi,
alisema miti ya wananchi 63 na majengo ya watu 17, yalilazimika kuondolewa, na
sasa shilingi milioni mia 500.723 zimeshatumika.
‘’Kati ya fedha hizo, zaidi ya shilingi milioni 134.6 zimetumika
kulipa majengo ya makaazi na shilingi milioni 437.434 zimeshatumika kuwalipa
wananchi 63 walioharibiwa miti yao,’’alieleza.
Mapema Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar
Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema ujenzi wa barabara hiyo, umechukuwa muda
mrefu hadithi yake, bila ya kutekelezwa.
Hata hivyo Dk. Khalid alisema katika kipindi kifupi
tayari wizara inaendelea na ujenzi wa kilomita 854 kwa Zanzibar, ambapo kwa
Pemba zipo wastani wa kilomita 300 zinazoendelezwa ujenzi katika maenoe mbali mbali.
Alisema, kwa upande wa mkoa wa kaskazini Pemba, zipo
wastani wa kilomita 81.35 wakati mkoa wa kusini kukiwa na kilomita 53.6 kwa
barabara za vijijini pekee, zinazoendelea na ujenzi.
‘’Lakini kwa upande wa wilaya ya Chake chake, wizara
wakati wowote itaanza na ujenzi wa barabara ya Wesha- Mkumbuu yenye urefu wa
kilomita 10, Wawi- Mesi kupitia Mzambarau -Boko yenye urefu wa kilomita 6.4, Mkoroshoni-
Ndugu kitu hadi Machomane kilomita 2 pamoja na Mchanga wa Kwale- Kichuwani
yenye urefu wa kilomita 2.7,’’alifafanua.
Aidha Waziri huyo aliwaeleza wananchi kuwa, barabara nyingine
ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami ni Chanjaani- Pujini, Chanjamjawiri- Tundaua,
Mizingani -Wambaa, Mtambile -Kangani na Mtambile -Mwambe, ambazo awali barabara
hizo zilijengwa kwa lami baridi.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud,
amewataka wananchi wa Mgelema, kuwawalinzi na barabara hiyo, ili iweze kudumu
kwa muda mrefu.
Hata hivyo amepongeza Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali
Mwinyi, kwa usikivu wake wa vilio vya wananchi, hali inayosababisha kuimbua
miradi mkubwa na yenye tija.
Mwisho
Comments
Post a Comment