Skip to main content

LFS YAKUNWA UTOAJIA MSAADA WA KISHERIA ZANZIBAR

 

NA HAJI NASSOR, ZANZIBAR@@@@

MWAKILISHI wa taasisi ya LFS, Wakili Alphonce Gura, amesema kwa sasa Zanzibar, imekuwa sehemu ya kujifunzia katika utoaji wa msaada wa kisheria kwa nchi za Afrika Mashariki.

Alisema, hayo yamejitokeza tokea lilipomalizika jukwaa la pili la Msaada wa kisheria mwezi Disemba mwaka 2022, lililofanyika Zanzibar, na kuibuliwa maazimio ambayo yalilenga kutekelezwa.

Wakili huyo, aliyasema hayo Novemba 20, 2023, wakati akitoa salamu za LSF, kwenye jukwaa la tatu la Msaada wa kisheria, lililofanyika ukumbi wa mikutano Chuo cha Utalii Maruhubi mjini Zanzibar.

Alisema, kwa nchi za Ruwanda, Burundi, Unganda, Kenya na hata Tanzania bara, Zanzibar kwa sasa, imekuwa kinara na sehemu ya kujifunzia, kwa upekee na ubora wa utoaji wa msaada wa kisheria.

‘’Sisi LSF, tunaridhishwa na tunapongeza mno kazi inayofanywa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, kwa kuongeza wigo na kusababisha kuchukua nafasi ya kwanza, kwa utoaji wa msaada wa kisheria,’’alieleza.



Katika hatua nyingine, Wakili huyo na Mwakilishi wa LSF Alphonce Gura, alieleza kuwa, amevutiwa mno na kaulimbiu ya mwaka huu, juu ya ‘kuimarisha huduma za msaada wa kisheria zenye ubora na zinazozingatia matokeo’, kwamba inakwenda na wakati.

Akizungumzia kanzi data, ambayo imeanzishwa na LSF kwa muda mrefu, alisema inaangalia na kuzichakat kazi, zinazofanywa na wasaidizi wa sheria mmoja moja kwa Tanzania nzima.

Alieleza kuwa, kupitia kanzi data hiyo, imedhihirisha uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria na kufikia watu 200,000 kila mwaka na kufikia watu milioni 7 kwa mwaka wanaohitaji elimu ya sheria.

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, akiwasilisha yatokanayo na jukwaa la pili la msaada wa kisheria Zanzibar, alisema ni pamoja na azimio la kuifanyia marekebisho sheria ya Msaada wa kisheria.



Jingine alisema, ni azimio la kuanzishwa kwa mfuko wa msaada wa kisheria, jambo ambalo tayari Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar, wameshawasilisha andikoni la kwanza wizarani.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo, ameupongeza uongozi wa taasisi za LSF na UNDP, kwa kuendelea kuinga mkono Idara hiyo, ili kuona jamii inaendelea kupata elimu, ushauri na msaada wa kisheria.

‘’Kwa hakika, wenzetu hawa wamekuwa wakitubeba kila siku, katika shughuli zetu mbali mbali, na hata kuadhimisha majukwaa kama haya, na sasa tunajivunia kwa jamii,’’alieleza.

Akifungua Jukwaa hilo, Naibu Mwanasheria mkuu wa Zanzibar Shaaban Ramadhan Abdalla, alisema majukwaa kama hayo, husababisha watoa msaada wa kisheria, kupata nafasi ya kujadili mafanikio na changamoto zao.




Alieleza kuwa, kazi inayofanywa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria na hadi kupelekea kutekeleza majukwaa matatu kwa sasa, imekuwa ndio jambo pana na lenye kutoa wigo, na kujipima kwa watoa msaada wa kisheria.

‘’Kwa hakika majukwaa haya ya msaada wa kisheria, yanatoa dira na mwelekeo kwa watoa msaada wa kisheria, ambao wanakwenda moja kwa moja kuwahudumia wananchi, tena bila ya malipo,’’alifafanua.

Hata hivyo Nibu Mwanasheria mkuu huyo mkuu wa Zanzibar, alielezea kuvutiwa na kusikia kuwa yametekelezwa kwa vitendo maazimio yatokanayo na jukwaa la pili la msaada wa kisheria.

‘’Kwa hakika ni jambo jema, kusikia kuwa rasimu ya msaada ya kisheria imeshapita katika baadhi ya ngazi, kwa ajili ya kuifanyiwa  marekebisho sheria hiyo,’’alifafanua.

Mwakilishi wa kutoka wizara ya Katiba na sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Edith Shekidele, alisema amekuwa akivutiwa mno na kazi inayofanywa na wizara kama hiyo Zanzibar, hasa katika kuwafikia wananchi.




‘’Wananchi wamekuwa wakitutegemea mno katika kuwafikia, hasa eneo la utoaji wa msaada wa kisheria, ingawa kwa hapa Zanzibar kazi inafanywa kubwa mno,’’alifafanua.

Akiwasilisha mada ya bajeti ya msaada wa kisheria, Mkuu wa skuli ya sheria Zanzibar Dk. Ali Uki, alisema bado changamoto ni kuendelea kuwategemea wafadhili, kwa asilimia kubwa kuendeshea asasi.



Akichangia mada hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la Msaada wa kisheria na haki za binaadamu Zanzibar ‘ZALHO’ Harusi Miraji Mpatani, alisema juhudi inayohitajika ni wanaasasi, ili kuwa na vyanzo mbadala vya mapato.




Mahafoudhi Shaaban Haji, alisema vikwazo kwa asasi na hasa zile za watoa msaada wa kisheria, ni kukosekana taaluma ya kuibua njia za kupata mapato.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu Tawala za Mikoa na serikali za mitaa, Zainab Khamis Kibwana, alisema lazima matumizi ya rasilimali fedha zitumike, kwa mujibu wa vipaumbele.

Hili ni jukwaa la tatu la msaada wa kisheria, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘kuimarisha huduma za msaada wa kisheria zenye ubora na zinazozingatia matokeo’.

Mwisho



Comments