Na Mwandishi Wetu
SHERIA ya ushahidi ya Zanzibar ya mwaka 2016 iliyoanza kutumika Januari 18, 2017, imeanzisha utaratibu maalum wa kisheria wa kupokea ushahidi wa kielektroniki. Sheria inatoa uhakika katika kupokea na kukubali ushahidi wa kielektroniki.
Kifungu cha 71 hadi 73 vya sheria vinaeleza jinsi ushahidi wa kielektroniki unavyoweza kukusanywa na kushughulikiwa.
Uwepo wa sheria hii ni dhahiri kwamba ushahidi wa kielektroniki unaweza kutumika wakati wa uchunguzi wa kesi za udhalilishaji wa kijinsia.
Hata hivyo, utekelezaji unafanywa kwa kiwango kisichoridhisha sana, hali inayosababisha waathirika kutopata haki kwa wakati.
Aidha, wakati sheria inaruhusu wapelelezi kukusanya ushahidi wa kielektroniki, polisi bado hawana ujuzi wa kutosha wa jinsi ya kukusanya ushahidi wa kielektroniki.
Ofisa wa makosa ya mtandao kutoka Jeshi la Polisi Zanzibar, Issa Mohamed Salum, "Hatujapewa mafunzo ya kukusanya ushahidi wa kielektroniki. Bado tunaandika maelezo ya waathiriwa kwenye karatasi.
Lakini ikiwa waendesha mashtaka wanataka ushahidi wa sauti na picha, tunaweza kukusanya, lakini bado hakuna miongozo.”anasema.
Sara Omar Hafidh, Hakimu wa mahakama ya mkoa wa Vuga anayesimamia kesi za udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, anakiri kwamba sheria ya kukubali ushahidi wa kielektroni, lakini ushahidi wa kielektroniki una mapungufu.
"Inaweza kuwa sauti ya mwathirika, lakini vipi ikiwa mwathirika atasema sauti si yake. Katika hali kama hiyo, hakimu bado asingeweza kutoa uamuzi.”anasema.
Hata hivyo, anakiri kwamba mahakama inaendelea kupokea ushahidi wa kielektroniki ingawa sio kwa kiasi kikubwa lakini kutakuwa na maboresheo kadri changamoto zitakapoibuka.
Wadau wa kupinga udhalilishaji Zanzibar wanaishauri Serikali kukarabati na kuboresha miundombinu ya Mahakama maalum ya kushughulikia kesi za udhalilishaji Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwezesha matumizi ya ushahidi wa kielektroniki ili kuwa rafiki kwa wanaotumia mahakama hizo na kuwezesha upatikanaji wa haki katika mazingira bora.
Wanasema licha ya mahakama hiyo kuonesha mafanikio makubwa ya usikilizaji wa kesi tangu kuanzishwa kwake lakini bado miundombinu yake haitoshi kutokana na kukosekana kwa vyombo vya kisasa vya usikilizaji wa kesi, ikiwemo mifumo ya kidigitali (video conference) na ukosefu wa vyumba maalum vya kuwaweka watoto walioathirika na vitendo hivyo.
Hawra Shamte, anansema TAMWA Zanzibar hivi karibuni ilifanya utafiti Unguja na Pemba ambapo ilibaini ukosefu wa vifaa katika mahakama na miundombinu duni bado ni changamoto, mfano majengo ya Mahakama ya Vuga, Mahonda, Mkoani na Wete Pemba ni ya zamani na karibu kupitwa na wakati wakati jambo linalopelekea ugumu katika uendeshaji wa kesi za udhalilishaji.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdallah, anasema kuwa ushahidi wa kieletroniki unatumika Mahakamani lakini kunachangamoto ikiwemo weledi kwa watendaji katika ushahidi wa kieletroniki.
“Kinachokosekana ni weledi wa kufanya upelelezi wa kiushahidi wa kieletroniki, lakini kukosekana uweledi kwa Polisi ambao ndio wanaosimamia shauri, kwa waendesha mashtaka wanaokuja mahakamani kuja kuthibitisha kosa lakini pia kwa mahakimu na majaji ambao ambao shauri wanalitolea mamauzi”anasema.
Aidha anasema wote hao wanajisomea wenyewe kujiendeleza na hazani kuwa wote hao kama wanaelimu nzuri jinsi ya kuutumia ushahidi wa kieletroniki na mara nyingi wahalifu huwa wapo vizuri.
Anasema kuna haja kusimamia vizuri hilo kuendeleza mafunzo kwa watendaji wote kwa sababu huo ndio uhalifu wa kisasa wa kieletroniki.
Anasema makosa ya udhalilishaji wa kijinsia ni muhanga wa makosa ya kieletroniki na mahakama imejipanga kuwa na vifaa vya kusikiliza ushahidi wa kieletroniki.
“Serikali hii mahakama tumejipanga kuwa na vifaa vya kieletroniki katika usikilizaji wa mashauri, na sisi tukiwa mbele wezetu DPP, ZAECA, POLISI na taasisi zingine ziwezeshwe katika kupata vifaa hivyo”anasema.
Kwa mujibu wa Ofisi ya mtakwimu mkuu wa Serikali Zanzibar kwa mwezi wa Oktoba mwaka huu jumla ya matukio 199 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa, yakiwa na idadi ya waathirika 199 wa matukio hayo, ambapo waathirika wengi wakiwa ni Watoto kwa asilimia 78.9, wanawake 16.1 na wanaume asilimia 5.0.
Mwisho
Comments
Post a Comment