NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
Katika majimbo
mengi Unguja na Pemba ni kawaida kusikia malalamiko ya waliochaguliwa
kuingia Baraza la Wawakilishi, Bunge na Udiwani nadra kuonekana, tafauti na
walipohangaika kuchaguliwa.
Hii ilipelekea majimbo mengi kuzorota kimaendeleo kwa vile hapakuwepo
watu waliohangaikia shida zao na kilichosikika ni wananchi kulalamika kwamba
waliowachagua kupeleka mbele madai yao hawaifanyi kazi kama walivyotarajia.
Hali ilianza kubadilika hivi karibuni kutokana na kuibuka wanawake
majasiri na wanaojituma kuhangaikia kero hizi baada ya kushika hatamu za
uongozi katika ngazi mbali mbali.
Wapo watu
waliodiriki kusema laiti zamani kungekuwa na wawakilishi wanawake kama hawa
waliopo sasa, matatizo ya majimbo mengi yangepatiwa ufumbuzi na
yangepungua.
Licha ya kuwepo
viongozi wanawake wachache, lakini kazi waliyoifanya wengi wao ni kubwa na
inathibitisha maelezo ya kwamba siku zote mama huwa na huruma na ndio maana
wawakilishi wanawake wanatumia vizuri fedha za mfuko wa Jimbo na wakati
mwengine wanatoa mifukoni mwao ili kusukuma gurudumu la maendeleo katika
majimbo yao.
Uchache wao haukuwa
sababu wasitekeleze walichowaahidi wananchi na wamejitokeza kusimama kidete
kuhakikisha wanatimiza ndoto za wananchi waliowapa nafasi za uongozi.
Zanzbar inayo wawakilishi
wanawake 29, wakiwemo wanane waliochaguliwa, 18 viti maalumu 18 na watatu
wateule wa Rais.
Wote wanafanya kazi
vizuri kwa kila siku kuibua matatizo ya wananchi na kufanya juhudi za kuyapatia
ufumbuzi.
"Kila
nilipoiangalia jamii niliona imeelemewa na mzigo wa changamoto na
walioumia zaidi ni wanawake na watoto na walikosa watetezi.
Nilikuwa naumia na
ndio maana siku moja nikaamua kujitokeza kutaka kuwatetea kwa kuingia jimboni
kugombea,” anasema Zawadi Amour Nassor, mwakilishi wa Jimbo la Konde Pemba.
Alikwenda jimboni
kuchukua fomu ya kugombea akiwa hana tamaa ya kupata kutokana na baadhi ya watu
kumbeza kwa kile walichodai hakuwa na pesa za kuwagaia.
"Nilikuwa
nasikia lazima uwe na pesa ndipo ufanikiwe, lakini niliamua kutafuta mzee mmoja
kupata ushauri, lakini aliniangusha kwa kuniambia niende viti maalumu, lakini
sikuridhia," anaeleza Zawadi.
Alimtafuta mzee
mwengine mwaka 2019 na kumshauri kuchukua fomu ambapo kufanikiwa na sasa
anaendelea kutatua changamoto za wananchi.
Katika kipindi
kifupi cha kuwa mwakilishi ametatua changamoto mbali mbali, ikiwa pamoja na
kuchimba visima vinane.
Anasema, visima
saba kati ya hivyo viligharimu shilingi milioni 14 kila kimoja na kimoja
ambacho ni kikubwa kiligharimu shilingi milioni 21.
Mwakilishi huyu
anahimiza malezi mazuri ya watoto kwa kutoa elimu na kulizungumzia suala hilo
katika Baraza la Wawakilishi.
Mambo mengine
ambayo anajihusisha nayo ni mpambano dhidi ya dawa za kulevya na udhalilishaji
wa wanawake na watoto.
Vile vile, ameweka
gari ya kubebea wagonjwa na huwasaidia sana akinamama na watoto ambao hupelekwa
hospitali bila ya malipo.
Kwa kutumia fedha
za mfuko wa Jimbo alizijengea uzio skuli mbili na kununua eneo la kiwanja
katika kijiji cha Kipange ambacho Wizara ya Elimu inawajengea skuli, ili
kuwapunguzia watoto masafa marefu ya kwenda skuli.
Pamoja na hayo
yote, mwakilishi huyo ametengeneza uwanja wa michezo na kwa sasa wapo katika
hatua ya mwisho.
"Tumezipatia
jezi timu 26 za mpira na nimezisajili kwa kutumia zaidi ya shilingi milioni nne,
kwa sasa timu hizi zinashiriki ligi kuu, vile vile nimewapatia mafunzo
waendesha bodaboda 43 kwa gharama zangu, ili kuwasaidia kujiepusha na ajali’’,
aliongeza.
Mafanikio yake
mengine ni pamoja na kuitengeneza skuli ya
maandalizi ya
Makangale, ili kutimiza ahadi aliyitoa wakati akiomba kura.
Maryam Thani Juma,
mwakilishi wa Jimbo la Gando, anasema alichukuwa fomu ya kugombea katika
uchaguzi wa mwaka 2015.
Anaeleza,
alishawishiwa na mumewe kugombea uongozi baada ya kuona nafasi nyingi
zinachukuliwa na wanaume, huku utetezi ukiwa mdogo katika kushughulikia masuala
ya maendeleo katika Jimbo.
Wakati akiwa
barazani amekuwa akitetea mambo mengi na mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na
kujengwa kwa skuli ya ghorofa iliyopo Kizimbani, hospitali ya Wilaya Kinyasini,
ujenzi wa tangi la maji Raha, uchimbaji wa visima Junguni na barabara za ndani.
Alizitumia fedha za
mfuko wa jimbo kukarabati madarasa na vyoo vya skuli mbali mbali, kujenga
mabanda mawili ya skuli ya maandalizi Kwale Mpona.
Vile vile alichimba
visima vinne katika Jimbo lake, ambapo vitatu ni kupitia fedha za wahisani na
kimoja kwa kutumia fedha zake mwenyewe.
Alivipatia vikundi
nane vya wanawake wajasiriamali zana za kufanyia kazi na fedha kwa kila kikundi
laki mbili, ambapo wengine aliwadhamini kuchukua mkopo benki ya CRDB na mwisho
wa siku kulipa yeye.
Alifanya kombe kwa
wanamichezo na kutumia zaidi ya shilingi milioni nne katika kuziendeleza timu
za mpira na pia alichezesha ligi ya mbuzi kwa gharama zake mwenyewe.
Baadhi ya
mambo aliyoyafanya Mwakilishi wa Jimbo la Chambani Bahati Khamis Kombo katika
kuling’arisha jimbo lake ni, kujenga skuli za maandalizi Chumbageni, Pujini na
Chambani.
‘’Pia
nimejenga madarasa na kuezeka skuli za msingi Wambaa, Ukutini na Dodo ambapo
katika skuli ya Dodo pia nimekarabati vyumba vyengine vinne na stoo kwa kutia
saruji na plasta,’’ anasema.
Mwakilishi
huyo aliweka kifusi kwenye barabara za Wambaa- Kwaazani sokoni, alichimba
kisima kwa ajili ya wananchi na wanafunzi wa skuli ya Ukutini, kulaza mipira ya
kusambazia huduma ya maji safi na salama, pamoja na kufikisha huduma ya umeme
kijiji cha Kwaazani.
Alijenga
barabara ya kijiji cha Kumvini- Kibaridi kwa kiwango cha lami, kusimamia ujenzi
wa barabara kuu ya Ole –Kengeja na vituo vya mama na mtoto, ambapo hutumia
fedha za mfuko wa jimbo na fedha zake kuhakikisha maendeleo yanapatikana.
CHANGAMOTO WALIZOKUMBANA NAZO WAKATI WA KUGOMBEA
Ni baadhi ya watu
kuwatia hofu na woga kwani wao walichukulia kuwa ni kitu kikubwa na
hakiwezekani kufanywa na wanawake.
Kuvunjwa moyo na
kuambiwa kuwa hawawezi kufanya chochote kutokana na maumbile yao ya kike, jambo
ambalo sio sahihi kwani wameweza na wanaendelea kuwatumikia wananchi wao.
Mwakilishi wa Jimbo
la Konde yeye alikerwa na baadhi ya marafiki na vipenzi vyake walivyobadilika
nyoyo zao na kuwa zaidi ya nyoka, kutokana na tamaa ya pesa zaidi kuliko utu na
ihsan.
Mwakilishi wa Jimbo
la Gando anahadithia wanaume walitumia kigezo cha dini kuwakataza wanawake kuwa
viongozi, ingawa yeye alikuwa anawatolea mifano hai ya wanawake wa kiislamu
walioongoza enzi za manabii.
NINI KIFANYIKE
Wanawashirikisha
wananchi katika kuibua na kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili na ndio
maana wanafanikiwa katika kutekeleza yale waliyojipangia kuyafanya.
"Unaposikiliza
kero za wananchi na kuzitatua basi unapungukiwa kubezwa na kuonekana huna
thamani, hivyo tunajivunia kuaminiwa katika majimbo yetu," anasema
mwakilishi Zawadi Amour Nassor.
Ili kuondosha
migogoro kwa wananchi ni vyema wachukue juhudi ya kuwasikiliza na kuwaondolea
matatizo katika vijiji vyao, watumie fedha za mfuko wa Jimbo kupeleka maendeleo
kwani uwezo wa kusaidia wanao.
ASASI ZA KIRAIA
Mratibu wa TAMWA
Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema, wana mpango mkubwa wa kuwajengea uwezo
wanawake na jamii, ili wawe na muelekeo chanya kushiriki kwenye vyombo vya
maamuzi.
“Na tumeona kwamba
wanawake wengi waligombea katika chaguzi zilizopita, ingawa hawakushinda wote
lakini walionesha moyo mzuri na walioshinda wanaendelea kufanya vizuri katika
majimbo yao,” anaeleza.
Kwa Pemba, TAMWA
imeshawapatia mafunzo wanawake 70 wenye nia ya kugombea na wamewaunganisha na
wanawake mashujaa ambao tayari wameshagombea nafasi mbali mbali, ili kuwajengea
uzoefu na kuwatoa hofu.
Hafidh Abdi Said
ambae ni Mkurugenzi wa PEGAO anaeleza, wanawake wachache wanaokaa katika nafasi
za uongozi, wanaonekana juhudi kubwa wanazozifanya katika kutekeleza majukumu
yao.
‘’Tulipofanya
utafiti kwenye vyama, tulituambia kwamba wanapochaguliwa viongozi wanawake hata
chama kinaimarika zaidi kwani wanachangia kwa kiasi kikubwa,’’, anasema.
WANANCHI
Wanasema kuwa, wapo
tayari majimbo yote yachukuliwe na wanawake kutokana na utendaji wao wa kazi
pamoja na kuwatatulia shida zao.
"Kwa vyovyote
vile mwanamke ana huruma, hivyo wanajitahidi kutekeleza zile ahadi
walizozichukua kwa vitendo, hilo limetufanya tuwapende," wanaeleza
wananchi hao.
Hassan Salim Ali
mkaazi wa Kizimbani Wete anasema, wawakilishi wanawake wamekuwa mstari wa mbele
katika kuisaidia jamii kuwa na maendeleo, hivyo ni muhimu kuwepo hata katika
majimbo yote.
"Mimi naona
tulichelewa sana kutambua hili, lakini tungejua mapema naona majimbo yote
tungechukua sisi, mwakilishi wetu anajitutumua kwa kweli kutatua matatizo yetu,
anahitaji pongezi," Asha Suleiman mkaazi wa Kiuyu kwa Manda.
Wingi wa wanawake
waliopo nchini haujawawezesha usawa wa jinsia katika nafasi za uongozi
zinazotokana na uchaguzi ili kufikia 50 kwa 50.
Kwani mwaka 2020
wanawake walioingia katika Baraza la Wawakilishi ni 29 kati ya 75 ya
wawakilishi wote huku wanaume wakiwa 46.
Ambapo wanawake
waliogombea ni 61 na walioshinda ni nane (8), huku wanaume waliogombea wakiwa
190 na walioshinda ni 42
Kwa mujibu wa tume
ya uchaguzi Zanzibar, wanawake walioingia Baraza la Wawakilishi mwaka 2015 ni
28 sawa na asilimia 36, kati ya wawakilishi wote 84.
Kutokana na idadi
hiyo inaonesha dhahiri kwamba elimu imewafikia ipasavyo wanajamii na wanawake
katika ushiriki wa wanawake kwenye uongozi na ndio maana idadi inaongezeka.
Kwa kutambua umuhimu wa mwanamke,
sera na sheria mbali mbali za Zanzibar zimeeleza kuhusu haki ya wanawake
kushiriki katika demokrasia na uongozi.
Kifungu cha 21 (2) cha Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 64 kimeeleza kwamba, kila mzanzibari anayo haki na uhuru wa
kushiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu mwanamke
na taifa lake.
Katiba ya Zanzibar mwaka 1964
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 imeeleza wazi katika kifungu nambari 67 (1)
kuwa, kutakuwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanawake kwa idadi ya
asilimia 40 ya wajumbe wote wa kuchaguliwa katika majimbo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment