JUKWAA LA TATU LA MSAADA WA KISHERIA ZANZIBAR, WAZIRI HAROUN AAMSHA SHANGWE UKUMBINI 'SOMA HIYOOO'.....LSF WASEMA JAMBO
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
NOVEMBA
20 na 21 mwaka huu, ilikuwa siku nyingine adhimu na adimu, kwa wadau wa haki
jinai Zanzibar.
Siku hii,
ambayo kila mwaka hujitokeza mara moja, ni kwa ajili ya kuwakutanisha wadau wa
haki jinai na washirika wao, kujadili mafanikio, changamoto za utoaji wa msaada
wa kisheria.
Kwa jukwaa
hili la tatu la mwaka huu, ambalo lililfanyika Chuo cha Utalii Maruhubi Unguja,
kama kawaida wadau wa haki jinai, kutoka kuona zote Tanzania, walihudhuria.
Hapa Idara
ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, iliyochini ya Ofisi ya Rais, Katiba,
Sheria na Utawala Bora ikishirikiana kwa karibu na wadau wake LSF na UNDP,
iliwavuta washiriki kutoka Pemba na Tanzania bara.
Wenyeji
waliopo Unguja, ndio waliokuwa na kazi ya kuwakaribisha wageni wao, kutoka
maeneo mbali mbali, na si haba jukwaa, lilifana.
YALIOJIRIA
KATIKA JUKWAA LA TATU LA MSAADA WA KISHERIA 2023
Jukwaa hili,
lilifunguliwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Shaaban Ramadhan Abdalla,
ingawa kabla ya hutuba yake, iliyowavutiwa wengi kulitanguliwa na yatokanayo na
jukwaa la mwaka 2022.
Mkurugenzi
wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Abdalla,
ambae kiprotokoli ndie mwenye jambo lake, aliyasoma maazimio hayo.
Kwanza
akaeleza kuwa, majukwaa hayo yamekuwa na tija mno katika kuweka mazingira
rafiki, kwa watoa msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa sheria.
Akisema
kuwa, kinachoaahidiwa kupitia majukwaa hayo, yamekuwa yakitejelezwa, akitolea mfano
yale yalioahidiwa mwaka 2022, kwenye jukwaa la pili la msaada wa kisheria.
Lakini kwanza
Mkurugenzi huyo, akaelezea malengo ya jukwaa la tatu la Msaada wa kisheria,
akisema moja ni kuimarisha ufanisi na uweledi wa utendaji wa majukwaa ya
watoaji wa msaada wa kisheria.
‘’Kuwezesha
upatikanaji wa sera na sheria mpya, zinazokidhi mahitaji ya jamii, katika
upatikanaji wa huduma za kisheria, kuanzisha upatikanaji wa sahihi wa taarifa
za utoaji wa huduma za msaada wa kisheria,’’alitaja maazimio.
Akafafanua
kuwa, lengo jingine ni kukuza ubunifu na kuimarisha uwezo wa watoaji wa msaada
wa kisheria, katika kuendeleza majukumu yao ya kazi za kila siku.
Mkurugenzi
Hanifa akaweka wazi kuwa, lengo jingine ni kuwaunganisha watoa msaada wa
kisheria na taasisi nyingine, ili kuwawezesha kufanyakazi kwa ufanisi.
Baada ya
kueleza dhamira ya jukwaa la tatu, sasa Mkurugenzi huyo, akawakumbusha
washiriki hao kuwa, kwa yale maazimio ya Disemba 13 na 14, 2022, nayo
yameshatekelezwa.
Hapa akatoa
mfano wa machache, ni pamoja na kutakiwa kuifanyia marekebisho sheria ya Msaada
wa kisheria ya mwaka namba 13 ya mwaka 2018 pamoja na sera yake, sambamba na
kuweka mfuko wa msaada wa kisheria.
Akisema
kuwa, kazi hiyo ilipewa Idara yake pamoja na Tume ya Kurekebisha sheria
Zanzibara, na tayari andiko la kwanza limeshapelekwa wizarani.
‘’Kwa hili,
tayari rasimu ya sera ya msaada wa kisheria imeshaandaliwa, na hili ni baada ya
kukukusanywa maoni, ya wadau wa Unguja na Pemba na uanzishwaji mfuko limezingatiwa,’’akafafanua.
Azaimio
jingine ambalo limseshatekelezwa ni kuitaka Mahkama na Idara ya Katiba na
Msaada wa kisheria, kushirikiana na wasaidizi wa sheria katika utoaji wa elimu
ya kisheria.
‘’Na hili tayari
Mahkama ililitekeleza, maana ilishirikiana nao, katika shehia za Kidombo,
Gamba, Mcheza shauri na Tumbatu kwa Unguja kutoa elimu ya sheria,’’anafafanua.
Serikali
kuzingatia nafasi za ajira kwa watu wa wenye mahitaji maalum, limeshatekeleza
kwani wapo watumishi watatu, wameshaajiriwa.
Suala la
kuweka wakalimani wa lugha ya alama, katika vituo vya Polisi, kwa sasa tayari
watendaji kadhaa wa Jeshi la Polisi, wako masomoni, kusomea lugha ya alama.
LSF
Kisha zamu
ikawa ni ya mwakilishi kutoka taasisi za LSF Wakili Alphonce Gura, akisema kwa
sasa Zanzibar, imekuwa sehemu ya kujifunzia katika utoaji wa msaada wa kisheria,
kwa nchi za Afrika Mashariki.
Anasema hayo
yamejitokeza tokea lilipomalizika jukwaa la pili la Msaada wa kisheria mwaka 2022,
lililofanyika Zanzibar, na kuibuliwa maazimio, 13 yaliyotekelezwa.
Wakili huyo,
anasema kwa nchi za Ruwanda, Burundi, Uganda, Kenya na hata Tanzania bara,
Zanzibar imekuwa kinara na sehemu ya kujifunzia, utoaji wa msaada wa kisheria.
‘’LSF,
tunaridhishwa na tunapongeza mno, kazi inayofanywa Idara ya Katiba na Msaada wa
kisheria Zanzibar, kwa kuongeza wigo na kusababisha kuchukua nafasi ya kwanza,
kwa utoaji wa msaada wa kisheria,’’anafafanua.
Gura, amevutiwa
mno na kaulimbiu ya mwaka huu, juu ya ‘kuimarisha huduma za msaada wa
kisheria, zenye ubora na zinazozingatia matokeo’, kwamba inakwenda na
wakati.
Akizungumzia
kanzidata, ambayo imeanzishwa na LSF mwaka 2013, inayoangalia na kuzichakata
kazi, zinazofanywa na wasaidizi wa sheria, mmoja mmoja kwa Tanzania.
Kupitia
kanzidata hiyo, imedhihirisha uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria na kufikia
watu 200,000 kila mwaka na kufikia watu milioni 7 kwa mwaka, wanaohitaji elimu
ya sheria Tanzania.
Jukwaa hilo la
tatu la mwaka 2023, lilifunguliwa na Naibu Mwanasheria mkuu wa Zanzibar Shaaban
Ramadhan Abdalla, akasema majukwaa hayo, husababisha watoa msaada wa kisheria,
kupata nafasi ya kujadili mafanikio na changamoto zao.
Kazi
inayofanywa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria na hadi kupelekea
kutekeleza majukwaa matatu kwa sasa, imekuwa ndio jambo pana na lenye kutoa
wigo, na kujipima kwa watoa msaada wa kisheria.
‘’Kwa hakika
majukwaa haya, yanatoa dira na mwelekeo kwa watoa msaada wa kisheria, ambao
wanakwenda moja kwa moja kuwahudumia wananchi,’’anafafanua.
Alielezea kuvutiwa
mno kusikia kuwa, yametekelezwa kwa vitendo maazimio yatokanayo na jukwaa la
pili la msaada wa kisheria.
‘’Ni jambo
jema, kusikia kuwa rasimu ya msaada ya kisheria imeshapita katika baadhi ya
ngazi, kwa ajili ya kuifanyia
marekebisho sheria hiyo,’’anafafanua.
Mwalika kutoka
wizara ya Katiba na Sheria ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Edith
Shekidele, nae akavutiwa mno na kazi inayofanywa na wizara kama hiyo Zanzibar,
hasa katika kuwafikia wananchi.
‘’Wananchi
wamekuwa wakitutegemea mno katika kuwafikia, hasa eneo la utoaji wa msaada wa
kisheria, ingawa kwa hapa Zanzibar kazi inafanywa kubwa mno,’’anafafanua.
Mmoja wa
wawasilisha mada kwenye jukwaa hilo, Mkuu wa skuli ya sheria Zanzibar Ali Uki,
kwenye mada yake ya bajeti ya msaada wa kisheria, akasema bado changamoto ni
kuendelea kuwategemea wafadhili, kwa asilimia kubwa kuendeshea asasi.
‘’Lazima
asasi ziangalie uwezekano wa kuibua njia mbadala za vyanzo vyengine vipya vya
mapato, badala ya kutegemea wafadhili wa nje pekee,’’anafafanua.
Akichangia
mada hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la Msaada wa kisheria na haki za binaadamu
Zanzibar ‘ZALHO’ Harusi Miraji Mpatani, anasema juhudi inayohitajika ni
wanaasasi, kuwa na vyanzo mbadala vya mapato.
Hata Mahafoudhi
Shaaban Haji mwakilishi wa asasi za kiraia Zanzibar, anasema vikwazo kwa asasi
na hasa zile za watoa msaada wa kisheria, ni kukosekana taaluma ya kuibua njia
za mapato.
Mkurugenzi
wa Idara ya Uratibu Tawala za Mikoa na serikali za mitaa, Zainab Khamis
Kibwana, anasema lazima matumizi ya rasilimali fedha zitumike, kwa mujibu wa
vipaumbele.
Kwa siku ya
pili, katika jukwaa hilo kulikuwa na mada mbili, moja wapo ni mifumo ya
ufuatiliaji na tathmini na matokea, katika sekta ya sheria, iliyotolewa na
Saada Mkwangwa.
Ni Afisa
ufuatiliaji na tathmini kutoka taasisi ya LFS, ambae anasema ufuatiliaji mzuri
ni ule ambao utakuwa na takwimu na kuonesha uhitaji wa wateja.
Mada
nyingine ambayo iliwasilishwa ni uunganishaji wa mifumo ya ufuatiliaji na
tathmini, iliyotolewa na Rukaiya Khamis Othman, Mkuu wa Divisheni ya Ufanisi na
uchambuzi wa mifumo.
Kisha Waziri
wa Nchi, Ofisi yaa Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali
Suleiman, alilighairisha jukwaa hilo na kutamka rasmi kufuta ada ya usajili kwa
wasaidizi wa sheria.
‘’Naelewa
vyema kuwa, wasiaidizi wa sheria, mnalipa ada ya shilingi 20,000 ingawa kila
baada ya miaka miwili, lakini kuanzia sasa natangaaza kuifuta ada hiyo,’’alibainisha
huku akishangiliwa.
Waziri Haroun
akasema, ufutaji huo kwa sasa unawahusu wale watoa msaada wa kisheria wanaojisajili
mmoja mmoja, akiwemo msaidizi wa sheria, mavakili, wanasheria na hata mawakili
wanaojisajili kama watoa msaada wa sheria.
Upande mwingine,
akaweka wazi kuwa hapo baadae, wizara itangaalia uwezekano kuondoa ada hiyo na
hata kwa tasisi zinazotoa msaada wa kisheria.
Jingine
alilopendekeza Waziri huyo ni kuangalia uwezekano wa kubadilisha neno ‘jukwaa’
na kuangalia jina jingine kama vile baraza la watoa msaada wa kisheria.
‘’Mkurugenzi
wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, tafuteni jina mwafaka la
kuita lakini sio ‘jukwaa’ nahisi linaleta tafsiri ya kujibagua,
ili mwakani tuwe na jina jingine,’’alipendekeza.
Alienda mbali
zaidi Waziri Haroun akaishauri kuwa, Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria,
kuwapeleka ziara za kujifunza wasaidizi wa sheria, ili kuongeza wigo mpana wa
kazi zao.
Lakini kabla
ya hutuba hiyo, Mkurugenzi wa Idara hiyo Hanifa Ramadhan Said, alisoma maazimio
tisa (9) ya jukwaa la tatu, likiwemo kuhakikisha katika jukwaa lijalo,
kuwashirikisha washiriki kutoka nje ya Tanzania.
Jingine ni wahusika
wa sekta ya sheria kuundwa kikosa kazi na kufanya ushawishi katika uidhinishaji
wa bajeti na uingizaji wa fedha, ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya
msaada wa kisheria kwa ufanisi zaidi.
Azimio namba
tatu ni wizara inayohusika na msaada wa kisheria, kusimamia uandaaji na utekelezaji
wa mpango kazi wa pamoja wa watoa huduma msaada za kisheria.
‘’Wahusika
wa msaada wa kisheria watahamasisha baadhi ya taasisi kama vyama vya
wafanyakazi kuwa na utaratibu wa kutoa huduma za msaada wa kisheria, kwa
wanachama wake, na kuweka wataalamu wa sheria katika maeneo yao,’’anafafanua.
Mkurugenzi
huyo alitaja azimio jingine kuwa ni, vyama vya Wanasheria na Mawakili, wakishirikiana
na wahusika wa msaada wa kisheria watawahamasisha mawakili katika uwakilishi
mahakamani.
Skuli ya
sheria Zanzibar, itaweka ulazima kwa wanafunzi wanaosomea uwakili, kuvitumia vituo
vya msaada wa kisheria, kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo.
‘’Wizara
husika ya Katiba na Sheria itaanzisha kanzidata ya kitaifa na mfumo jumuishi wa
kidigitali wa ukusanyaji taarifa za msaada wa kisheria, kwa kushirikiana na
wahusika wa msaada wa kisheria,’’anaongeza.
Hili ni
jukwaa la tatu la msaada wa kisheria, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘kuimarisha
huduma za msaada wa kisheria zenye ubora na zinazozingatia matokeo’.
Mwisho
Comments
Post a Comment