NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MWANASHERIA
Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi asubuhi
hii, katika Jukwaa la tatu la mwaka la msaada wa kisheria Zanzibar.
Jukwaa hilo,
linatarajiwa kufanyika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi mjini Zanzibar,
ambapo tayari washiriki mbali mbali kutoka kisiwani Pemba na Tanzania bara,
wameshawasili kisiwani Unguja.
Kwa mujibu
wa taarifa iliyopatikana na blog ya Pemba today, inaeleza kuwa, katika Jukwaa
hilo, pamoja na kuwepo kwa Mwanasheria mkuu, aidha viongozi mbali mbali watawakuwepo.
Mmoja wa
viongozi wanaotarajiwa kuwepo ni Waziri wa nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria,
Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman.
Viongozi
wengine ni Katibu mkuu wa wizara hiyo Mansura M. Kassim, wakurugenzi mbali mbali
wa wizara hiyo, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na msaada wa Kisheria
Hanifa Ramadhan Said ambae ndie mwenyeji wa shughuli hiyo.
Aidha taarifa
zinaeleza kuwa, washiriki wengine ni kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Tume ya Kurekebisha sheria, wadau wa
haki wa jinai.
Wengine ni
watoa msaada wa kisheria, wasaidizi wa sheria, taasisi za watu wenye ulemavu,
masheha, wanufaika wa msaada wa kisheria na makundi mengine ya jamii.
Kabla ya
hutuba ya mgeni rasmi, taasisi mbali mbali kama za LSF, UNDP, wasaidizi wa
sheria, Katibu mkuu na Wizara husika watatoa hutuba zao, ambazo zitalenga kuongeza
ari na kasi, kwa wasaidizi na watoa msaada wa kisheria Zanzibar.
Ambapo kwa
upande wa UNDP salamu katika jukwaa hilo la tatu, zinatarajiwa kutolewa na
Mwakilishi wao aliyepo Zanzibar Godfrey Nyamrunda, wakati zile za LSF
zinatarajiwa kutolewa na Wakili Alphonce Gura.
Kisha kwa
siku ya kwanza, na baada ya mgeni rasmi kuondoka ukumbini, watoa mada akiwemo Mkuu
wa skuli ya sheria Zanzibar Dk. Ali Uki na Katibu wa Tume ya Kurekebisha sheria
Zanzibar Mussa Kombo Bakari watachukua nafasi yao.
Akizungumza hivi
punde, Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake
Pemba, CHAPO Nassor Bilali Ali, alisema majukwaa kama hayo, yanawaamsha wale
wasaidizi wa sheria waliolala kikazi.
Alisema, jambo
linalofanywa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar chini ya
Mkurugenzi Hanifa Ramadhan Said, kwa kushirikiana na taasisi za LSF na UNDP, linawapa
moyo wao kwenye kazi zao.
Afisa sheria
wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar ofisi ya Pemba Bakar Omar
Ali, alisema kwa upande wake juu ya kuwafikisha washiriki Unguja, limekaa sawa.
Sheha wa
shehia ya Wawi Sharif Abdalla Waziri, alisema kwake hii ni mara ya kwanza
kushiriki, lakini limemtia moyo, juu ya kazi inayofanywa na wasaidizi wa sheria,
shehiani mwake.
Katika jukwaa
hili la tatu, ambalo litaanza asubuhi ya leo Novemba 20 na kumalizika kesho, kauli
mbiu ya mwaka huu ni ‘kuimarisha huduma za msaada wa kisheria zenye ubora
na zinazozingatia matokeo’
Mwisho
Comments
Post a Comment