WANANCHI kisiwani Pemba wametakiwa kuacha tabia ya kuchimba mashimo ya vyoo na makaro karibu na vianzio vya maji, ili kuepusha uchafuzi wa maji ambayo yanaweza kusababisha maradhi ya kuharisha.
Akizungumza na masheikh, maimamu na walimu wa madrasa katika shehia ya Mjananza wilaya ya Wete Pemba, Inspekta wa Jeshi la Polisi Khalfan Ali Ussi alisema kuwa, kipindi hiki ni cha mvua hivyo wananchi wachukue tahadhari kujiepusha na madhara mbali mbali ikiwemo maradhi ya mripuko na maafa.
Alisema kuwa, ni vyema viongozi wa dini wakachukua juhudi ya kuwaelimisha wananchi waache kuchimba mashimo ya vyoo na makaro kwenye vianzio vya maji, kwani ndiyo wanayotumia kwa kunywa na kupikia, hivyo yanaweza kuchafuka na kuwasababishia maradhi.
"Lengo la mkutano wetu huu ni kuelezea juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, tunajua kuwa kuna mvua nyingi, hivyo tuwaelimishe wanajamii kuchukua tahadhari kutokana na madhara yanayoweza kujitokeza," alisema.
Alieleza kuwa, pia wanatakiwa kufunika makaro yao ili yasiweze kusababisha madhara ikiwemo vifo, kwani wakati wa mvua watoto wanacheza sehemu wasizozijua na hatimae wanaweza kutumbukia.
Aidha, aliwashauri viongozi hao kuwakumbusha wananchi kutambua athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa kama vile mafuriko, maradhi ya kuambukiza, maradhi ya matumbo ambayo yanasababishwa na maji yasio salama.
"Tunatakiwa kuchemsha maji ya kunywa hasa katika kipindi hiki cha mvua, ili kuepukana na magonjwa," alisema Inspekta huyo.
Aliwataka viongozi hao wa dini, kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe ujumbe huo unawafikia wananchi kabla ya kutokea madhara, kwani wao wanakaa na watu wengi kwa wakati mmoja na wanaaminiwa sana na jamii
Inspekta huyo pia aliitaka jamii kuchukua tahadhari ya kutosha juu ya uwezekano wa kutokea vitendo vya kihalifu hasa nyakati za usiku, kwani wahalifu hutumia fursa hiyo ya kunyesha mvua kutekeleza azam yao ya kuiba.
"Tuweke taa za nje zenye mwanga mkali na taa za ndani tuzizime ili muhalifu asione mazingira ya ndani, hii itatusaidia kuepusha uwezekano wa kuvunjwa na kuiba," alifahamisha.
Sambamba na hayo aliitaka jamii kushirikiana pamoja na kuimarisha ulinzi maneno yote sambamba na kuendelea kumtumia vikundi vya ulinzi shirikishi kuimarisha doria hasa nyakati za usiku.
Vile vile aliwaasa wananchi kusikiliza, kufuatilia na kutekeleza taarifa na maelekezo ya wataalamu wa hali ya hewa ili kuepuka maafa masiyo ya lazima.
Kwa upande wao viongozi wa dini walisema kuwa, elimu waliyopewa wataifanyia kazi kwa maslahi ya jamii na taifa, huku wakiahidi kuwafikishia wananchi ili waweze kujikinga na madhara mbali mbali yanayoweza kujitokeza wakati mvua zikiandelea.
MWISHO.
Comments
Post a Comment