NA HAJI NASSOR, PEMBA @@@@
WANANCHI wa kijiji cha Mtega, shehia
ya Wawi wilaya ya Chake chake Pemba, wameamua kuikarabati barabara yao yenye
urefu wa kilomita 2.5, kwa kutumia matofali ya fuuwe na mawe, baada ya
kuharibika kwa mvua, inayoendelea kunyesha.
Mwandishi wa
habari hizi, aliwashuhudia wananchi hao, wakiwa kwenye eneo la barabara hiyo, wakiikarabati
barabara hiyo, kwa kutumia vipande vya matofali na mawe, ili iweze kupitika.
Wananchi hao
walisema, uamuzi huo umekuja kufuatia kukosa misaada kutoka mamla husika, hali
iliyopekea mvua kuathiri barabara yao.
Mwenyekiti
wa kamati ya maendeleo ya kijiji hicho, Khamis Haji, alisema barabara hiyo
imeharibika mno, kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini kote.
Alieleza
kuwa, juzi Mei 4, kamati iliikagua barabara hiyo, na kufikia uamuzi wa kutafuta
matofali na mawe, ili kuikarabati katika maeneo, yalioathiriwa zaidi na mvua.
‘’Hivi sasa,
kama atatokezea mgonjwa ama mzazi anataka kwenda hospitali, inabidi tutumie
gari za Ng’ombe au tutumie magunia hadi njia kuu,’’alieleza.
Mwenyekiti
huyo alieleza kuwa, kwa sasa kwenye kijiji chao cha Mtega hakufika, gari wala
chombo chochote cha maringi mawili, kutokana na kukatika na kuchimbika kwa
barabara yao.
Wakati huo
huo, Mwenyekiti huyo amepiga marufuku tabia ya baadhi ya wananchi kuchota
mchanga kwenye barabara hiyo, na kusema, atakaepatikana atafikishwa mbele ya
vyombo vya sheria.
‘’Wapo
baadhi ya wananchi wenzetu, kwa maksudi huchimba mchanga kwenye barabara hii,
hivyo tunawataka kila mmoja awe mlinzi kwa mwenzake,’’alifafanua.
Katika hatua
nyingine, amemtaka Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, kuzitekeleza ahadi
walizoziweka za kuwapatia kifusi kwenye bara bara hiyo.
Mshika fedha
wa Kamati hiyo, Mwalimu Juma Yahya, alisema kusita kwa mchango wa shilingi
50,000 kwa kila nyumba, ambazo ilikuwa ni kwa ajili ya ununuzi wa kifusi,
kumesababisha uchakavu wa barabara hiyo.
‘’Kama lile
zoezi la uchangiaji wa fedha, kwa ajili ya ununuzi wa kifusi twengelikamilisha
kabla ya mvua, leo barabara yetu isingeharibika sana,’’alieleza.
Hata hivyo,
amewakumbusha wananchi wa kijiji cha Mtega na wengine, kuendelea kutoa michango
yao, ili kufanikisha ununuzi wa kifusi, mara mvua zitakapomalizika.
Mjumbe wa
kamati hiyo Rashid Ali Mussa, alisema lazima katika kipindi hichi cha mvua, mkazo
wa kuifanyia ukarabati barabara hiyo uwekwe, na wananchi wenyewe bila ya
kutegemea ufadhili.
Nao Ibrahim
Mohamed Ali, Hassan Abdalla na Khamis Khatib walisema, lazima kila mmoja, awe
mlinzi kwa mwenzake, juu ya suala la uchimbaji wa mchanga kwenye barabara yao.
Bara bara ya
kijiji cha Mtega, shehia ya Wawi wilaya ya Chake chake, iliyoanzia Wawi kwa
Gerei, yenye urefu wa kilomita 2.5 kupitia mtega uwanja wa mpira, hadi mwanzo
wa kambi za Jeshi la wananchi, iliasisiwa mwaka 2016 na wananchi wenyewe.
Mwisho
Comments
Post a Comment