NA ZUHURA
JUMA, PEMBA@@@@
JUMUIYA
ya Maendeleo ya Wanawake wa Kiislamu Pemba (JUMAWAKIPE)imekanusha tangazo
lililosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba, Jumuiya hiyo inawataka Waomani
wanaotaka kuoa, wafike kisiwani Pemba kwani wanawake wapo kuanzia miaka 18 hadi
35.
Jumuiya hiyo imesema kwamba, tangazo hilo ni la kupuuzwa
kwani waliosambaza ujumbe huo ilijiita ni Jumuiya ya Wanawake Pemba na sio
Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake wa Kiislamu Pemba, jambo ambalo si katika
akhlak za kiislamu kumnadisha mwanamke katika mtindo huo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Amira wa Jumuiya
hiyo Asya Amour Abdulrahman alisema kuwa, wanalaani kitendo hicho kilichofanywa
na Jumuiya hiyo ya Wanawake Pemba, ambapo wao kama Jumuiya ya JUMAWAKIPE
wanakanusha kusambaza ujumbe huo.
Alisema kuwa, ujumbe uliosambaa mitandaoni ulisomeka kuwa ‘Jumuiya
ya wanawake Pemba inapenda kuwajulisha Waomani wote wanaotaka kuoa yakwamba
wapo wanawake kuanzia umri wa miaka 18 hadi 35 wakiwa bikira kwa gharama ya
mahari ya Omani riali 200 na gharama za sherehe riali 300 ambazo jumla ni riali
500’, jambo ambalo sio sahihi katika dini ya kiislamu.
‘’Kwanza jina la Jumuiya yetu ni tofauti na hiyo
iliyosambaza tangazo hilo, pili Jumuiya yetu haina malengo hayo na pia si
katika akhlak za kiislamu kumnadisha mwanamke katika mtindo huo, kwa hiyo
tunakanusha sisi kwamba hatukutoa tangazo hilo na tunalaani vikali kwa
waliohusika kusambaza ujumbe huo’’, alisema Amira huyo.
Amira huyo alisema kuwa, Jumuiya yao ya JUMAWAKIPE imelazimika
kukanusha kutokana na uvumi ulioenea na kupigiwa simu na viongozi wakuu pamoja
na watu mbali mbali kuhusiana na jambo hilo ambalo ni kinyume na utaratibu wa
dini ya kiislamu.
Waliiomba jamii na wanawake wote wa kiislamu duniani kote na
wale wote wanaoipenda Jumuiya hiyo kwa dhati ya moyo wao kuwa Jumuiya ya
JUMAWAKIPE haihusiki na tangazo hilo lililosambaa mitandaoni na kwamba Jumuiya
yao ipo salama.
MWISHO.
Comments
Post a Comment