NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
ABRAHMAN Juma Abdalla miaka 70,
mkaazi wa kijiji cha Kuyuni wilaya ya Mkoani, ameanguka ghafla na kufariki
dunia papo hapo, akiwa kwenye foleni ya kuchukua maji ya kiimani katika bahari
ya Msuka, wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba.
Itakumbukuwa
kua, eneo hilo lilishafukiwa na kupigwa marufuku na serikali, kuwataka wananchi
wasiyatumie maji hayo, kwa kutokuwa salama kiafya.
Pamoja na
marufuku hiyo, imeabainika kuwa wapo baadhi ya wananchi, wamekuwa wakilitumia
eneo hilo na kuchota maji ya kiimani, yanayodaiwa kuponyesha magonjwa na
maradhi sugu.
Kwa mujibu
wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema mpatwa na mauti, alifika shehia ya Msuka
mashariki leo Mei 6, mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi, akitokea kijijini kwao
Kuyuni wilaya ya Mkoani.
Walisema,
mzee huyo alifika eneo hilo, akikabiliwa na magonjwa sugu, ili kuchukua maji
hayo, ambayo alikuwa anaamini, yanaweza kumponyesha magonjwa yake.
Mmoja kati
ya mashuda hao Omar Kije Omar alisema, mzee huyo alimpita njiani, akiwa na dumu
la lita 20, akielekea kwenye eneo la uchukuaji maji hayo.
‘’Mimi
nilikuwa na safari zangu za kwenda kwenye kilimo, lakini alinipita na kuniuliza
ikiwa kuna walinzi ama laa katika eneo hilo, na kuelekea kwenye chem chem
hiyo,’’alieleza.
Alifafanua
kuwa, ghafla akiwa kwenye shughuli zake karibu na eneo hilo, aliona kundi la
watu, likiwa limejikusanya eneo karibu na chem chem hiyo, na aliposogea aliona
mwili ukiwa umefunikwa.
Sheha wa
shehia ya Msuka Mashariki Bakar Ali Bakar, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho,
na kusema kuwa, alipokea taarifa hizo majira ya saa 5:00 asubuhi ya Mei 6,
mwaka huu.
Alisema,
baada ya kupokea taarifa hiyo, alifika eneo la tukio na kuukuta mwili wa
marehemu, ukiwa umefunikwa na tayari ameshafariki dunia.
‘’Taarifa
nilizozipata ni kuwa, marehemu hakufariki wakati wa kuchota maji, bali alikuwa
kwenye foleni ya kuelekea kuchota maji hayo, licha ya kuzuiwa na
serikali,’’alieleza.
Alieleza
kuwa, pamoja na marufuku ya serikali na kufukiwa, lakini bado wastani wa watu
kati ya 10 hadi 15 kutoka maeneo mbali mbali, hufika na kuchukua maji hayo.
Kamanda wa
Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Juma Saad Khamis, alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo, na kusema baada ya uchunguzi marehemu, ameshakabidhiwa kwa jamaa
zake.
Alisema,
marehemu aligundulika kuwa na maradhi ya presha na sukari, na ndio ambayo
kutokana na machofu iliyosababisha kifo chake.
‘’Marehemu
hakufariki kwenye chem chem ya maji ya kiimani, kama wengine wanavyoeleza, bali
alianguka akiwa kwenye foleni ya kwenda kuchukua maji hayo,’’alieleza.
Kamanda huyo
aliwataka wananchi, kuheshimu amri halali ya serikali ya kutolitumia eneo hilo la
Msuka wilaya ya Micheweni, kutokana na maji hayo, kutokuwa salama.
April 5, mwaka huu Wizara ya Afya Zanzibar, ilipinga
kutumika kwa maji hayo, ikisema sio salama kwa matumizi ya bindamu kwa kule
kuwa na vimelea kati ya 220 hadi 1800 kwa kila lita moja ya maji hayo.
Waziri wa
wziara hiyo Nassor Ahmed Mazurui, alisema uchunguuzi umebaini kuwa, maji hayo
yamebeba kloraida kiasi cha miligramu 149 hadi 2059 kwa kila lita moja ya maji
hayo ya chem chem.
Ambapo
alisema ,kwa kwaida ya maji ya kunywa, hutakiwa kuwa na kiwango cha chumvi
sifuri (0), ingawa hayo yanayodaiwa kuwa ni tiba yamebaba chumvi 2.8 hadi 3.8
ambayo ni hatari kwa binadamu.
Hata hivyo
Waziri huyo aliwataka wananchi wote, ambao wameshawahi kuyatumia maji hayo,
kufika vituo vya afya mbali mbali kwa ajili ya uchunguuzi wa afya zao.
Mwisho
Comments
Post a Comment