Skip to main content

HUU HAPA UTAMADUNI WA WATU WA MICHEWENI ULIODUMU HADI LEO


 

NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

 ‘’TUMESHAWAHI kusimamisha shughuli ya harusi kwa dakika 10, mke asichukuliwe na mume wake, baada ya kugundua hatujamtia pambo la kipini cha pua,’’anasema Rehema Faki Shehe (60) wa Kwale Micheweni Pemba.

Ilishazoelekea kuwa, kuwa mapambo ni aina ya mafuta, podari, pete, mkufu, udi, wanja na hina, ingawa kwa wanawake wilaya ya Micheweni, kipaumbele ni utoboaji wa pua kwa ajili ya utiaji wa kipini cha pua.

Utamaduni wa uboboaji (utomoaji) wa pua tena ya upande wa kushoto, wenyewe wanawake wa Micheweni waliurithi zaidi ya miaka 200 iliyopita.

Kwa mfano, Rehema Faki Shehe (60) alimkuta bibi yake wakati akiwa huo akiwa na miaka 50, akiwa ametobolewa tundu la upande wa kushoto ya pua, akiwa na kipini.

KINA MAAGA GANI KIPINI CHA PUA?

Sharifu Massoud Hamad (60) wa Kwale Micheweni mkoa wa kaskazini Pemba, anasema moja ni tofauti kati ya mwanamke na mwanamme.

Anaona hata unapokuta wamevaa mavazi yenye kufanana, lakini dalili kubwa ya tofauti hiyo, ni kumuangalia kwenye mlango wa tundu ya pua ya upande wa kushoto, atakuwa na sehemu ya kuwekea kipini.

‘’Ukifika miaka kati ya mitano hadi minane, lazima kwa mtoto wa wilaya ya Micheweni apelekwe kwa mtoboaji na afanye hivyo, ili ajitayarishe kwa baade kuweka kpini,’’anasema.

Saada Said Kombo (58) anasema, kwa umri wake huo hakukuwa na dada yake wala mdogo wake wa kike ambae hakutobolewa pua kwa ajili ya kuweka kipini.

Anasema kila familia imekuwa na mtoboaji wake maalum, tena huwa bila ta malipo, kwa kila mmoja.

NANI ANAVA AKIPINI?

Kumbe uvaaji wa kipini ni kwa ajili ya mwanamke ambae tayari ameshaolewa pekee na sio mwengine, ambae bado hajafunda ndoa.

Hii wanasema, utamaduni unasindikiza kwa namna ya kumtofautisha kati ya mwari ‘kigori’ na mtu aliyekwishaolewa au mjane.

Aisha Hamad Shamata (65) anasema, tena ilishamtokezea mara mbili katika maisha yake, bibi harusi kumzuia kwa dakika 10 baada ya kusahau kumtia kipini.



Anasema, hakuna hata pambo moja ambalo ni muhimu na la lazima kwa harusi wa kike wa Micheweni, kama sio kipini cha pua.

Fatma Hamad Ali (40) anasema, hata yeye alipoolewa alilazimika wiki tatu kabla ya harusi yake, kutobolewa pua, kwa vile hakulelewa eneo hilo na alikosa huduma hiyo awali.

‘’Kwa mfano mimi sikulelewa eneo la Micheweni, ingawa ndio kwetu lakini nililazimika kutobolewa, ili kuiheshimisha ndoa na familia yangu,’’anasema.

Kweli anasema, mwanamke alimpenda mno baada ya kumkuta akiwa na kipini cha pua, na hayo anasema aliyabaini siku waliokwenda kuwasalimu wazazi, wiki mbili baada ya harusi yao.

Aisha Hashim Said (25) anasema wao ni utamaduni waliourithi na imekuwa vigumu hasa ikiwa utalelewa Micheweni kuuacha.

Halima Ibrahim Khamis (30) na mwenzake Hadia Ramadhan Himid (22) wanasema, ingawa siku ya kutobolewa hupata maumivu, lakini haiwi kikwazo kwa wengine kutobolewa.

‘’Maumivu yake kama sindano ya kawaida, lakini ninachoamini kama unataka uzuri, lazima kwanza uzurike,’’anasema Halima Ibrahim Khamis.



Maryam Issa Khamis anasema yeye alikataa kutobolewa pua akiwa na miaka 20, na aliolewa hadi sasa ana watoto watano akiwa kwenye ndoa.

‘’Kama hutaki kutobolewa, wenzako wengine wanakucheka wengine wanakuunga mkono na unaolewa bila ya shida nyingine,’’anasema.

WANAUME WA MICHEWENI WANASEMAJE?

 Wanasema, kama watawakuta wanawake waliowaoa hawakuwakuta na utamaduni huo, huwa na maswali yanayokosa majibu vichwani mwao.

Kwa mfano Faki Khamis Kai (60) anasema, moja ya pambo ambalo haliishi hamu, ni uwepo kwa pua yenye kipini kwa mke wake.

Kwao suala la udi, hina, piko, podari na asumini yapo kama mapambo ya ujumla, ingawa utamaduni wa utoboaji wa pua na kuweka kipini huwa ndio kipaumbele.

‘’Hata sisi kwenye vikao vyetu, huwa tunataniana na kuelezena kuwa, ikiwa mwanamke hana kipini cha pua hana tofauti na mwanamme,’’anasema.

Khamis Juma Khamis (73) anasema kipini cha pua ndio mpango mzima kwa mke, na mapambo mengine kama udi, hina na piko ni vitu vya kuondoka.

‘’Hata kama mwanamke anaumwa, au wewe mwanamme unaumwa, bado mke anakuwa anakupendezesha kwa kule kuwa na mng’ara pua kwa kipini,’’anasema.

Kwao hawajali na wala hawashughuliki aina ya kipini, kiwe cha dhahabu, almasi, silva hata cha kutengeneza kwa mali ghafi zinazotoka Micheweni kwao, huvutiwa.

Issa Hamad Shehe (25) anasema hata vijana wa leo utamaduni wa utoboaji pua, wanaupenda kwa wake zao, maana ndio pambo lisilo na gharama.

‘’Udi mpaka uwe na shilingi 1,000 kila baada ya muda, piko na hina zinawakati huchakaa kama ilivyo kwa udi, lakini kipini mpaka mtu afariki,’’anasema.

Kombo Haji Simba (35), anasema ni aibu kubwa kwao kuoa mke ambae mmetakana na familia yake, kukosekana kwa pambo la kipini cha pua.

HISTORIA YA UTOBOAJI WA PUA

Kwa zaidi ya karne tatu (miaka 300), hapo zamani wanawake wa jamii ya Kihindi na wale wa mwambao wa pwani hasa Tanga, walinza kutoboa sehemu ya miili yao katika pua.

Pia kwa wakati huo, halikuwa jambo la ajabu kuweka jino la dhahabu na hata kutoboa masikio yote mawili.



Ingawa historia inaonesha, unapotoboa pua, lazima kisha uweke kipini cha dhahabu, baada ya maumivu kuponya, na sio kweka jambo jingine lolote.

Kutoboa pua kumekuwepo kwa miaka mingi, katika ustaarabu tofauti ambao umetumia kurejelea vitu tofauti.

Ukubwa wa mapambo ya kujitia puani yalikuwa na maana ya utajiri wa kifamilia kwa makabila katika Afrika na Mashariki ya Kati.

Na mithili ya pete za pua zinadaiwa kutolewa kwa marafiki wa kike wapya na waume zao, kama hatua ya usalama.

Vivyo hivyo, ustaarabu wa Amerika ya Kati na Kusini umetumia kutoboa kwa septamu na mapambo yao kama alama za hadhi.

Katika jamii ya kisasa ya Magharibi, kutoboa pua kunahusishwa na tamaduni anuwai kama punk, tamaduni mbadala, na tamaduni ya bohemia.

Kutoboa pua hakuhitaji tu tahadhari na uvumilivu wa maumivu, lakini muhimu zaidi kuliko inavyosikika.



Kutoboa ncha ya pua ya wima ni kutoboa pua ya kipekee na nadra ambayo hutembea wima, kama jina linavyopendekeza, kutoka juu tu ya ncha ya pua hadi chini tu ya ncha ya pua.

Kwa sababu ya muundo wa pua yako, baa iliyopindika kwa kweli ni mapambo pekee yanayokubalika kwa aina hii ya kutoboa. 

 

ATHARI ZA UTOBAJI PUA USIOZINGATIA UTAALAMU

Maumivu ya pua, yanaweza kusumbua na kuumiza, na wakati mwengine yanaweza kusababishwa na homa, yenye kuambatana na mvutano wa misuli kwenye taya.

 

Daktari Issa Khamis Ali anasema lakini hata kwa mtobolewaji anaweza kukumbwa na shinda kwenye sehemu ya shingo, muoteo wa meno, muwasho usio wa kawaida kwenye pua ndani na nje.

               Mwisho

Comments