|
|
|
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
RIPOTI ya uhalifu na makosa ya usalama barabarani ya Jeshi la Polisi
Tanzania ya mwaka 2020, inaonesha kuwa, wapo wananchi 124 wameshauawa, kutokana
na watu kujichukulia sheria mikononi visiwani Zanzibar.
Uchunguzi umebainika, hao ni wa
kipindi cha miaka 10, kati ya mwaka 2011 hadi mwaka 2020, kwa mikoa mitano
pekee ya Zanzibar.
Kwa idadi ya wananchi hao
waliouawa, kwa tuhuma za kufanya uhalifu, ni sawa na kila mwaka, wastani wa
watu 13 kuuawa visiwani humo katika kipindi hicho.
Kwa idadi hiyo, ilisababisha
punguzo la watu kutoka milioni 1,303,569 waliohesabiwa kwenye sensa ya mwaka
2012, hadi kufikia watu milioni 1,303,445.
Watuo hao waliouawa kwa Zanzibar,
Mkoa wa Mjini Mgharibi Unguja, ulioongozwa kwa miaka yote hiyo na takwimu hizo
haijwahi kushuka.
Imebainika kuwa, mwaka 2011,
Zanzibar kuliripotiwa matukio manne (4), mkoa wa Mjini Magharibi pekee, uliripoti
matukio matatu (3).
Uchunguzi ukabaini kuwa, mwaka
2015 ambayo Zanzibar ilifanya uchaguzi wake mkuu wa tatu wa vyama vingi,
ilikusanya matukio nane (8), mkoa wa Mjini Magharibi uliripoti matukio matatu,
ingawa mwaka 2016 kati ya matukio 21, mkoa huo uliripoti matukio 16.
Hali hiyo, iliripotiwa kutisha
zaidi katika mwaka 2017, kulikoripotiwa wananchi 26 waliouawa, ambapo kati yao,
18 walikuwa wa mkoa wa Mjini Magharibi.
Kwa mwaka huo mikoa mingine ya
iliyoripoti matukio mengi zaidi, ni mkoa wa kusini Unguja kwa matano (5),
kusini Pemba matatu (3) na mikoa mengine kukiwa hakuna vifo vilivyoripotiwa.
Mwaka 2019 ulibeba matukio 17, uchunguzi
ukaonesha matukio 12 yalikuwa mkoa wa Mjini magharibi pekee, kusini Pemba
matukio mawili (2) na mikoa mengine kukiwa na idadi sawa na tukio moja moja.
Hata mwaka 2020, mkoa wa Mjini
magharibi, ulikusanya matukio 10, ya mauwaji kwa wananchi kujichukulia sheria
mikononi, kati ya matukio yote 15 yaliyoripotiwa.
NINI CHANZO CHA WANANCHI KUJICHUKULIA SHERIA
MIKONONI?
Hafsa
Issa Khamis Ali wa Mwanakwerekwe mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambae mwaka
2018 kijana wake wa miaka 18, aliauwa kwa tuhuma za wizi wa ndizi nne zenye
thamani ya shilingi 200,000 katika soko la Mwanakwerekwe anasema, chanzo ni
jamii kukosa maadili.
‘’Wanaotuhumiwa kwa mauwaji
wakiwa na hasira ikiwa hawafungwi, lakini wanaotuhumiwa kwa wizi, wanafikishwa
mahakamani na wakati mwengine wanafungwa, tabia hiyo itaendelea,’’anasema.
Khadija Mansour Haji wa Kikwajuni
wilaya ya Mjini Unguja, ambae mwaka 2019 mume wake alipoteza uhai kwa
kushambuliwa na wananchi wakati wa usiku, anasema chanzo ni sheria kuwa lege
lege za wanaoua.
‘’Kama sheria za anaeua
hazitafanyiwa kazi, basi makosa haya ya wananchi kujichukulia sheria mikononi hayatopungua’’,
anasema.
Mohamed Kassim Othman wa Gulioni
wilaya ya Mjini Unguja, anasema chanzo ni jamii kukosa uwelewa, juu ya
kumfikisha katika vyombo vya sheria mtuhumiwa wa aina yoyote.
Kheir Makame Haji wa Chake chake
Pemba, anasema bado jamii haijapata elimu ya athari ya kujichukulia sheria
mikononi na ndio maana visa hivyo mkaoni humo viko juu.
Mwanakhamis Muhidin Juma wa
Mzingani Mkoani Pemba, anasema mifumo ya haki jinai, kuanzia siku ya kwanza ya
kuripotiwa kwa tukio hadi siku ya hukumu ni shida.
VYOMBO VYA ULINZI VINASEMAJE?
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kaskazini
Pemba, Kamishna wa Msaidizi wa Polisi Juma Saadi Khamis anasema, chanzo ni ukosefu
wa elimu ya sheria husika, kwa wananchi walio wengi.
Jingine anasema inaweza kuwa ni
urasimu wa kisheria, uliopo katika vyombo vya sheria, ambao huchukua muda mrefu,
bila ya mtuhumiwa kesi yake kumalizika.
‘’Kwa kule wananchi kutokujua
sheria, ndio maana mwaka 2021 ndani ya mkoa wangu, kulikuwa na matukio manne (4)
ya mauwaji, ingawa kwa mwaka 2022, kulikuwa na tukio moja,’’anafafanua.
Mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashtaka Ali Amour Makame, anasema wananchi wanadhani
kujichukulia sheria mikononi, kama vile wanavisaidia vyombo vya ulinzia na
usalama kukomesha, jambo ambalo sio sahihi.
‘’Kama jamii inataka kutusaidia,
wawafikishe katika vyombo sheria, ambako huko ndio haki ya mtuhumiwa
inapatikana na sio kujichukulia sheria mkononi,’’anashauri.
Kamishna wa Polisi Zanzibar ‘CP’
Hamad Khamis Hamad, anasema chanzo ni inawezekana ni mifumo ya haki jinai ilivyo,
ikiwemo haki za mtuhumiwa, hasa dhamana.
Chanzo chingine ni mtuhumiwa
kuwa anarejea makosa na anapofikishwa mahakamani anashinda kesi, inayochangiwa
na wananchi wakati mwengine kutotoa ushahidi.
‘’Kama kuna mtu amefanya uhalifu
na kushuhudiwa, lakini baada ya kufikishwa mahakamani wananchi wakishindwa
kutoa ushahidi ataachiwa huru,’’anasema.
WANAHARAKATI WA HAKI BINAADAMU
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi
wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali anasema, kasi
ndogo katika vyombo vya sheria, kuyashughulikia makosa ya jinai, ndiko
kunakozaa fikra chafu ya kujichukulia sheria.
‘’Elimu ya athari ya
kujichukulia sheria mikononi, bado iko chini na ndio maana imekuwa jambo la
kawaida, hata mtu akituhumiwa kuchungulia kwenye jengo la jirani
anauawa,’’anafafanua.
Aliyekuwa Mratibu wa Kituo cha
Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ Pemba Safia Saleh Sultan, anaona chanzo ni
urasimu wa uliopo katika vyombo vya sheria.
Jengine ni ufinyu wa ufahamu kwa
jamii, juu ya haki za mathumiwa, jambo ambalo wanadhani kila anayetuhumiwa ana
haki ya kuuawa ama kufungwa.
Mratibu wa Tume ya Haki za
Binaadamu na Utawala Bora Tanzania ofisi ya Pemba Suleiman Salim, anasema hata
tafiti mbali mbali zinaonesha wavunjifu wakubwa wa haki za binadamu, ni
wananchi wenyewe.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona
Pemba ‘ZANAB’ Suleiman Manssour anasema, haki inayofikiwa mahakamani ya
watuhumiwa kuachiwa huru, ndio chanzo cha wananachi kujichukulia sheria
mikononi.
Mjumbe wa Baraza la Wazee mkoa
wa Mjini magharibi Haraoub Shein Hassan, anasema uhuru wa kufanya kila mmoja
apendavyo bila ya kuchukuliwa hatua, ndio chanzo cha mauwaji hayo.
VIONGOZI
WA DINI
Sheikh Said Ahmad Mohamed,
anasema chanzo ni waumini kukosa hofu ya Muumba wao, ambae ameshaahidi adhabu
kwa atakayeondoa uhai wa mwengine, kinyume na sheria.
‘’Uislamu unakataza na
hautambui, kumuondolea uhai mwengine kwa sababu ya tuhuma ya wizi, kwani sheria
ya dini ya kiislamu, imeweka wazi kwa mwizi, ikiwemo kukatwa mkono pindi
ushahidi ukikaa vyema.
Mchungaji Samuel Eliyas Maganga
ambae ni Mwangalizi wa Makanisa ya Pemba Tanzania Assembles of God ‘TAG’,
anasema Kanisa linakataza kujitoa muhanga, kulipiza kisasi na kuua.
‘’Kitabu cha ‘Kutoka’ kwenye
milango yake mbali mbali, inakataza moja kwa moja, mtu mmoja kuchukua kazi ya
Muumba ya kuondoa roho ya mwengine, kwani huko hakuondoi tatizo,’’alieleza.
KISAIKOLOGIA SABABU ZA WANANCHI KUJICHUKULIA SHERIA MIKONONI
Dokta Ali Yussuf, mtaalam wa
saikolojia ya binaadamu, anasema wananchi hufikia uamuzi huo, kutokana na
kujirerejea reje kwa makosa kwa mtu mmoja husika, katika maeneo yao.
Jengine ni wananchi kukata tamaa
na vyombo vilivyowekwa kwa ajili ya kuwashughulikia wahalifu, hivyo akili zao
hukosa imani na kufanya uamuzi wa kuua, ambao sio sahihi.
Daktari wa saikolojia Mtumwa
Hija Mzale anasema, uwezo wa akili ya mwanadamu ni kuvumilia kosa la mwanzo,
hivyo la pili likitokezea hupenda kujichukulia sheria mwenyewe, ili kukomesha.
‘’Kisaikolojia mwanadamu haridhishwi
na kukosewa yeye kisha adabu akaitoa mtu au mamlaka nyingine na ndio maana
hasira za wananchi hupenda kujichukulia sheria mikononi,’’anafafanua.
NYARAKA MBALI MBALI
Katiba ya Zanzibar yam waka 1984,
kifungu cha 13 kimebainisha kuwa ‘kila mtu anayo haki ya kuwa na hifadhi ya
maisha yake kwa mujibu wa sheria’.
Kifungu hicho kifafanua kuwa, ‘kila
mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi na ni marufuku kuteswa, kuadhibiwa
kinyama au adhabu zinazomdhalilisha’.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 15 ikafafanua kuwa, ‘kila mtu anayo haki ya kuwa huru
na kuishi kama mtu huru’.
Mkataba wa haki za binadamu wa
mwaka 1948 kuanzia ibara yake ya 3 hadi ya 8, imekataza kwa mtu kuteswa,
kuadhibiwa, kwani yuko huru kulindiwa.
Mkataba wa kimataifa wa haki za
kiraia na kisiasa wa mwaka 1966, ambao Tanzania uliuridhia mwaka 1976, Ibara ya
1, umeanisha haki ya kuishi, ukamilifu na usalama wa mtu.
ATHARI
YAKE
Ussi Khamis Haji wa mkoa wa Mjini Magharibi, anasema ni kuendeleza
visasi, kati ya familia ya waliouliwa kijana wao na familia ya watuhumiwa wa
mauwaji.
Mtumwa Saadi Ibrahim Mwinyi wa
Mtambile Mkoani, anasema athari nyingine ni wananchi kupoteza imani na vyombo
vya ulinzi na usalama, ambavyo ndio kimbilio lao.
Kamada wa Polisi mkoa wa kusini
Pemba Msaidizi wa Kamishna Abdalla Hussein Mussa anasema, ni kuvunjwa Katiba
ambazo zinakataza kuondoa uhai wa mtu.
Mratibu wa Tume ya Haki za
binadamu na Utawala bora Tanzania ofisi ya Pemba Suleiman Salim, anasema ni kuyachukua
mamlaka kisheria ya mahakama, kumpa mtu mwengine kuhukumu.
Mwenyekiti wa Jumuiya mwemvuli
wa asasi za kiraia Pemba ‘PACSO’ Sifuni Ali Haji, athari inayojitokeza ni
kujenga hofu miongoni mwa vijana katika shughuli zao za kila siku.
Sheikh Mohamed Juma Issa,
anasema athari nyingine ni kujitia katika makosa ambayo wakati mwengine adhabu
yake inaweza kuanza hapa ulimwenguni.
Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, athari ni vyombo
vinavyosimamia haki jinai, kukasimiwa madaraka yake kimakosa ikiwemo mahakama.
‘’Kisheria mahakama ndiyo ambayo
inaweza kutoa hukumu ya kifo, kama sheria zilivyo, lakini badala yake sasa,
wananchi ndio wamechukua nafasi hiyo jambo ambalo ni kosa,’’anasema.
NINI KIFANYIKE
Kamanda wa Polisi mkoa wa
kaskazini Pemba, Kamishna Msaidizi Juma Saad Khamis, anashauri elimu itolewa ya
athari ya kujichukulia sheria mikononi.
Wananchi Juma Seif Khamis na
Mayasa Himid Kassim, wanasema kinga ya kuwa na hasira, baada ya mmoja kumuua mwenzake,
iondolewe na badala yake ikibainika watiwe hatiani.
Afisa Sheria kutoka Idara ya
Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar ofisi ya Pemba Bakar Omar Ali, anasema wananchi
waelimishwe athari ya matokeo ya kujichukulia sheria mikononi.
Sheha wa shehia ya Wawi Sharifa
Waziri Abdalla, anasema vyombo vya ulinzi na usalama, viharakishe upelelezi wa
makosa mbali mbali, ili kupunguza hasira kwa wananchi waliotendewa kosa.
Afisa kutoka baraza la vijana
wilaya ya Chake chake, Sara Khamis Juma anasema vijana ndio waathirika wakubwa,
waanzishiwe mpango maalum, ambao unaweza kuzaa ajira.
Mwanamke ambae muume wake
alipoteza uhai kwa tuhma za kuvunja na kuiba eneo la Wete Pemba mwaka 2022,
anasema anaeuwa, nae mahakama iondowe uhaki wake.
Hidaya Mjaka Ali mwenye ulemvu
wa viungo, anasema lazima sheria ziwekwe ambazo zitaharakisha uendeshaji wa
kesi za jinai kwa haraka.
Mwisho
Comments
Post a Comment