NA
HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MKATABA wa kimataifa
wa haki za watu wenye ulemavu, ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania iliusaini Machi mwaka 2007 na kuthibithisha mwaka 2009, unalazimisha
huduma za afya kwa watu wenye ulemavu.
Ibara ya 25, inasisitiza nchi wanawachama, watumbue kuwa, watu wenye ulemavu wanayo haki ya kunufaika kwa kiwango cha
juu, huduma za afya tena bila ya ubaguzi wowote.
Mkataba
ukafafanua kuwa, nchi husika zitachukua hatua zinazostahiki, kuhakikisha watu
wenye ulemavu wanapata huduma bora za afya.
‘’Nchi
wanachama zitatoa huduma za afya, zinazohitajika kwa watu wenye ulemavu, hasa
kutokana na aina ya ulemavu wao, yakiwemo maeneo ya vijijini,’’umefafanua
Mkataba huo.
Ukaongeza kuwa,
nchi hizo zitawataka wataalamu wa afya, kutoa huduma za kiwango sawa kama watu
wenye ulemavu, kama zinavyotolewa kwa watu wengine, ikiwa ni pamoja na misingi
ya kutoa ridhaa kwa uhuru na ufahamu wa kutosha.
Mwaka 1983 hadi 1992 hatua mbali mbali
zilichukuliwa, ikiwani pamoja na maamuzi ya mwisho ya Umoja wa Mataifa, kuitangaza
Disemba 3 ya kila mwaka kuwa ni siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu duniani.
Ambapo siku hiyo pamoja na mambo mengine, kundi
la watu wenye ulemavu hujadili, mafanikio na changamoto zao mbali mbali,
zikiwemo na huduma za afya.
Kwa mfano katika sherehe za mwaka jana, Mkuu wa
mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, alipendekeza kuwepo kwa madirisha
maalum ya kutolea dawa kwa watu wenye ulemavu kwa hospitali za serikali.
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nayo, iliunda Mkakati wa Kitaifa wa
Ujumuishi wa mwaka 2010 hadi 2015 na sera ya taifa ya watu wenye ulemavu ya
mwaka 2004, ukitaja uhitaji wa lazima wa huduma za afya wa watu wenye ulemavu.
Ipo
sera ya kitaifa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2018 kwa upande wa Zanzibar, ambayo
nayo kwenye Ibara ya 20, ikasisitiza uimarishwaji wa upatikanaji huduma bora na
endelevu kwa watu hao.
Kuhusiana
na hatua za kisheria, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilitunga
sheria ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2010, ambapo ilikuja kuharakisha pia
suala la huduma bora za afya.
Zanzibar,
ambayo ilikuwa na Sheria ya Watu wenye Ulemavu, nambari 9 ya mwaka 2006, ambayo
sasa imefutwa na kuwa na sheria mpya nambari 8 ya mwaka 2022.
Kifungu cha 28 (1) (c) cha sheria hiyo, kimeanisha
haki ya kupata huduma za afya kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo matibabu,
matengenezo au marekebisho yanayohusiana na aina ya ulemavu wao.
Tanzania
bara pia iliunda Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya ambao unatoa mwongozo wa ufikiaji
wa huduma za afya kwa makundi yote yakiwemo ya watu wenye ulemavu kama viziwi.
Kwa
upande wa Zanzibar, kulikuwa na Mpango Mkakati wa sekta ya afya wa miaka tisa,
ambao uliishia mwaka 2019, wenyewe ulitaja hatua za kuchukuliwa, ili kuwakinga
na utapia mlo wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
UGONJWA WA CORONA NA
CHANJO YAKE
Wakati
hayo yakifanyika, Machi 11, 2020, Shirika la Afya Ulimwenguni ‘WHO’
iliiratibisha rasmi ugonjwa COVID-19 kama janga la dunia.
Hii baada ya ugonjwa huo wa mlipuko wa kuenea
kwa kasi duniani kote, ambao huenea kwa haraka katika mataifa na mabara mbali mbali.
Aidha WHO iligundua kuwa, watu 4,291 walikuwa wameshaaga
dunia na maelfu zaidi walikuwa wamelazwa hospitalini kwa muda mfupi.
Baada ya janga hilo, wataalamu wa afya waliibuka na
chanjo za aina mbali mbali, ambazo baada ya majaribio zikabainika kuwa,
zinaweza kuwa kinga.
Na hapo sasa wizara ya Afya Zanzibar kwa upande nwake, ilidhamiria
hadi ikiingia mwaka 2023 iwe wazanzibari 70 kila 100 wameshapa chanjo za
Corona.
Huku hayo
yakipangwa, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema Julai 27, mwaka 2022 kuwa
hadi kufikia Julai 25, 2022 jumla ya dozi bilioni 12.24 za chanjo ya Covid-19
zilitolewa duniani kote.
Utoaji wa chanjo dhidi ya Covid-19 hapa
nchini ulizinduliwa Julai 28, mwaka 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambapo chanjo aina ya Pfizer, Moderna, Sinopharm,
Sinovac na Jansen ziliidhinishwa kutumika.
VIZIWI WANASEMAJE?
Kassim Issa Khamis mkaazi wa Kisiwa cha
Makoongwe wilaya ya Mkoani akizungumza na wandishi wa habari hii, chini ya mkalimani
wake, anasema hajapata elimu ya ugonjwa wa Uviko 19.
Anasema, hana taarifa rasmi za kujikinga
na janga hilo, bali amekuwa akipewa taarifa za juu juu na familia yake.
‘’Kwa kuitwa na wizara ya Afya, sisi watu
wenye uziwi hapa wilaya ya Mkoani bado, bali wengine wanakwenda wakirudi
wanatueleza japo juu juu,’’anasema.
Mayasa Mkombe Mgando nae wa Kisiwani humo,
anasema wao wamesahauliwa kwenye elimu ya Uviko 19, hivyo wameshindwa kufanya
uamuzi kuhusu kuchanjo.
Idrissa Khamis Khamis wa Kisiwa Panza, wilaya
ya Mkoani, anasema amekuwa akishiriki kwenye shughuli kadhaa za kijamii, ingawa
kwenye elimu ya Uviko 19, wameachwa.
‘’Mimi ni kiongozi wa wenzangu wenye uziwi
katika shehia tatu, ikiwemo ya Kisiwa Panza, lakini wizara ya Afya ilitusahau
kutupa elimu ya moja kwa moja,’’anasema.
‘’Natamani hasa nipate elimu ya umuhimu wa
chanjo, ili kisha nifanye uamuzi wa kuchanja ama laa, lakini sasa elimu
niliyonayo ni kupitia kwenye baraza zetu za mazungumzo,’’anasema.
Maryam Ali Kombo wa kisiwa cha Makoongwe,
anasema hana elimu ya kutosha juu ya namna ya kujikinga na Uviko 19, kwani
hajawahi kuitwa na watendaji wa wizara kumpa elimu.
‘’Sisi ni wanachama wa chama cha viziwi
Zanzibar ‘CHAVIZA’ lakini hatujawahi kualikwa, chini ya mkalimani wetu,’’anasema.
Mama mmoja mwenye vijana wawili wote
viziwi mkaazi wa Kisiwa cha Shamiani wilaya ya Mkoani, anasema sio elimu ya
Uviko19, ambayo wamekuwa wakisauliwa, lakini hata shughuli nyingine za kijamii.
‘’Hata ukiona na sisi tumeshirikishwa
kikamilifu, basi iwe CHAVIZA, wamepata mradi, lakini vyenginevyo huwa vigumu
kupata taarifa rasmi,’’anasema.
Sheha wa shehia ya Kisiwa Panza Haji Ali
Shaali, anasema anaowahudumu wa afya shehiani mwake, lakini hawana utaalamu wa
kuzungumza na viziwi.
‘’Ninao viziwi wastani 15 kwenye shehia
yangu, lakini wote hawajafikiwa na elimu ya Uviko19, na kuachwa nyuma katika
vita dhidi ya ungonjwa huu,’’ anasema.
Muhudumu wa afya shehiani humo ‘CHV’
Haroub Makame Bakar, anasema ilikuwa vigumu kuwafikishia elimu viziwi, kutokana
na wao kukosa mafunzo ya lugha ya alama.
‘’Sisi ‘CHV’ tupo watano kwenye shehia,
lakini hakuna hata mmoja ambae anaelimu japo ndogo ya lugha ya alama, hivyo
basi elimu ya Uviko19 haikuwafikia viziwi,’’anasema.
Mkalimani pekee wa lugha ya alama Pemba Asha
Suleiman, anasema hajawahi kualikwa na wizara ya Afya au wahudumu wa afya, ili
kuwa makalimani wakati elimu ya kujikinga na Uviko19, ikietolewa.
‘’Tume za uchaguzi huwa wananialika au
Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, kwamba viziwi washiriki, lakini kwa hilo
la elimu ya Uviko19 bado,’’anasema.
Mwenyeikiti wa Chama cha Viziwi wilaya ya
Chake chake Mohamed Khamis Shehe, anasema hakuna hata mkutano mmoja, waliowahi
kualikwa wa utoaji elimu ya Uviko19.
Mjumbe wa Umoja wa Watu wenye Ulemavu
Zanzibar, Hidaya Mjaka Ali, anakiri kuwa, elimu ya Uviko19 kwa watu wenye uziwi,
haikuwepo moja kwa moja kwao.
‘’Ni kweli wizara ya Afya hasa Pemba,
imeyafikia makundi yote, lakini kwa wenzetu wenye uziwi kwa mkutano wao peke
yao, hilo halijafanyika,’’anasema.
Mratibu wa Baraza la Taifa la watu wenye
Ulemavu Mashavu Juma Mabrouk, anakiri kuwa wizara ya Afya haikuwahi kuliita
kundi la watu wenye uziwi, kuwapa elimu hiyo.
‘’Mbinu tulioitumia kwa watu wenye uziwi, ili
wafikiwe na elimu ya Uviko19, ni kuwatumia maafisa wa Baraza, ambao wameshapata
elimu na kukutana na viziwi,’’anasema.
Changamoto inayojitokeza kuwa ni uwepo wa
viziwi zaidi ya 400 kisiwani Pemba, ingawa kuwepo kwa mkalimani mmoja
anayetambulika.
Anakiri kuwa ile elimu rasmi ya Uviko19 na
hasa inayoambatana chanjo kutoka kwa wataalamu wa afya, watu wenye uziwi
imefika kwa kundi dogo mno.
WIZARA YA AFYA
Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis
Bilali Ali, anasema walichokifanya ni kukutana na wakuu wa Jumuiya za watu
wenye ulemavu, ili kuwapa elimu.
‘’Naamini katika elimu ya kujikinga na
Uviko19, hakuna mtu aliyeachwa nyuma, na hasa wenzetu wa makundi maalum,
tulikuwa na mkakati malum,’’anasema.
Eneo jingine, hadi leo hii wameweka
utamaduni wa kuyataka makundi yote, yawaalike wataalamu wa afya popote walipo
ili wapatiwe elimu ya Uviko19.
‘’Inawezekana kwa mfano wenye uziwi wapo
kisiwani na kufika mjini ni shida, kwa mujibu wa mazingira yao, sasa wawasiliane
na maafisa wetu wa afya wa wilaya na watafuatwa walipo,’’anasema.
Ingawa upande mmoja, Mratibu wa kitengo
cha elimu ya Chanjo cha wizaara hiyo Pemba Bakar Hamad, anasema utaratibu wao
ulikuwa ni kuyaenda makundi kuyapa elimu.
''Kwa mfano tulikwenda kwa vikosi vya ulinzi na usalama, wanafunzi wa skuli, vyuo vikuu, waandishi wa habari, wakulima, watumishi wa umma na viongozi wa dini,’’anasema.
Hivyo anasema hakumbuki kuwa na mpango
maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa uziwi peke yao, bali walikuwa na
mikutano ya elimu kwa makundi mchanganyiko.
NINI ATHARI YAKE?
Himid Mcha Khamis kiziwi mkaazi wa kisiwa
kidogo cha Fundo wilaya ya Wete, anasema ni kuwa rahisi wao kushambuliwa na
uogonjwa wa Corona au mengine ya mfumo wa hewa.
Aisha Haji Makame wa kisiwa cha Makoongwe,
anasema wamevunjiwa haki zao ambazo zimeainisha kwenye mikataba na sheria mbali
mbali.
Afisa Mdhamini wizara ya Afya Khamis
Bilali Ali, anasema moja ni kukumbuwa na maambukizo kwa wepesi, kama hawakuwa
na elimu ya kujikinga.
Afisa wa Chama cha Viziwi wilaya ya Chake
chake Mohamed Khamis Shehe, anasema ni kuwaweka wao katika msingi wa kukumbwa
na magonjwa.
NINI KIFANYIKE?
Mratibu wa Baraza la Taifa la watu wenye
uleavu Zanzibar Mashavu Juma Mabrouk, anasema ni wizara ya Afya kurudi kwa
kundi la watu wenye ulemavu, ili kuliemisha.
Mwashamba Haji Mrisho mwenye uziwi mkaazi
wa Chake chake, anasema nguvu ya elimu sasa ielekezwe kwa wenzao waliko
vijijini.
Mkalimani wa lugha ya alama Pemba Asha
Suleiman, anashauri vipindi na taarifa zote za kwenye tv zinapoendeshwa, kuwepo
kwa mkalimani maalum.
Jengine ni jamii na hata watu wenye
ulemavu wenyewe, kusomea lugha ya alama na ukalimani, kuwasaidia wananchi
wenzao wenye uziwi.
Mzazi mweye kijana mwenye uziwi, anasema
ni kutekelezwa kwa sheria kama zilivyo, ili kundi hilo lipate haki zao.
TAKWIMU YA WALIOCHANJA
Katika kipindi cha tarehe 29 Oktoba hadi 02 Disemba,
2022, jumla ya visa vipya 442 vimethibitika kuwa na maambukizi ya Uviko19.
Imebainika kuwa, idadi hii ni kubwa ukilinganisha na
takwimu za mwezi uliopita ambapo kulikuwa na visa vipya 272, sawa na ongezeko
la asilimia 62.5.
Hadi kufikia tarehe 02 Desemba 2022, jumla ya watu milioni
29,123,387 kati ya walengwa 30,740,928 ambao ni sawa na asilimia 94.7 wamepata
dozi kamili ya chanjo ya UVIKO- 19.
Mwisho
Comments
Post a Comment