NA ZUHURA
JUMA, PEMBA@@@@
WAZIRI
wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema, Maabara ya Afya ya Jamii Pemba
sasa ina uwezo wa kuchunguza maambukizi mapya na kufanya ufuatiliaji wa
magonjwa yenye umuhimu wa afya ya jamii kwa kutumia njia ya kisasa ya kugundua
maradhi 'Next General Sequencing (NGS).
Akizungumza mara ya kufungua maabara ya kisasa Wawi Chake
Chake Pemba Waziri huyo alisema kuwa, kuwepo maabara hiyo itasaidia kuchunguza
maradhi mbali mbali ndani ya kisiwa cha Pemba, jambo ambalo ni faraja kubwa.
Alisema kuwa, awali Wizara ya Afya ilikuwa ikisafirisha
sampuli za maradhi nje ya kisiwa cha Pemba jambo ambalo ilikuwa likiwapa
usumbufu kwani majibu yalikuwa yanachelewa na kushindwa kugundua kwa haraka maradhi
anayougua mgonjwa.
‘’Kwa kweli tupepata faraja kubwa sana kwa sababu sasa
maradhi kama Uviko 19, Ebola na magonjwa mengine yatachunguzwa katika mabara hii
ya Wawi Chake Chake Pemba, hivyo wataalamu na watendaji wazilinde na kuzitunza
mashine kwa kuweka mazingira safi na salama’’, alisema.
Alisema ni lazima Serikali ihakikishe nchi ni salama, ambapo
maabara ndizo ambazo zitawahakikishia, hivyo kwa sasa watafanya uchunguzi na
ugunduzi wa magonjwa kisiwani Pemba, jambo ambalo ni faraja kwani wameondokana
na usumbufu waliokuwa wakiupata.
Alisema kuwa ushirikiano kati ya Serikali na shirika la
shirika la kitanzania linaloboresha masuala ya Afya (MDH) kwa kuonesha
mafanikio makubwa katika kuimarisha mfumo wa huduma za maabara na afya kwa
ujumla, hivyo wataendelea kufanya kazi ili kuhakikisha ushirikiano kati yao na
wadau mbali mbali unaendelea kwa ufanisi ili kuboresha ustawi wa jamii yetu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dk.
Amour Suleiman Mohamed alisema kuwa, wamepata furaha kwa sababu mwanzo kulikuwa
na changamoto lakini anaamini kwa sasa imetatuka.
‘’Tulikuwa tunalazimika kusafirisha sampuli kwa zaidi ya
siku tano hatujapata majibu, jambo hili lilikuwa linatupa shida lakini kwa sasa
tutachunguza ndani ya masaa 24 tutapata majibu, hivyo nawaomba wataalamu
waitumie maabara ipasavyo ili kupata majibu sahihi’’, alisema Mkurugenzi huyo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Matar Zahor Massoud alieleza,
hatua iliyofikiwa ni kubwa ya kuwepo maabara ya kisasa Pemba kwani inaenda na
azma ya Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuimarisha huduma za Afya nchini.
‘’Tumefarajika sana, kwani huduma zitaimarika na uchunguzi
wa maradhi utakuwa wa haraka sana na kupata majibu ndani ya muda mfupi’’,
alieleza.
Mapema Afisa Uendeshaji Mkuu Maabara Pemba Dk. Said Mohamed
Ali alieleza kuwa, maabara hiyo ya kisasa itaisaidia Serikali katika kuboresha
huduma za utambuzi na ufuatiliaji wa maradhi mbali mbali.
Aliwashukuru wafadhili wao ambao ni Serikali ya Marekani
(CDC) kupitia shirika la kitanzania linaloboresha masuala ya Afya (MDH)
wakishirikiana na UNICEF pamoja na Serikali kwani imewarahisishia huduma za
uchunguzi na ugunduzi wa maradhi.
Meneja kutoka shirika la MDH David Sando alisema, mategemeo
yao ni kuwa uwepo wa maabara hiyo italeta matokeo chanya, hivyo watendaji wa
maabara hiyo wafanye kazi kwa ufanisi kwa maslahi ya jamii na Taifa kwa ujumla.
‘’Tulipata msaada wa fedha za Uvico 19 kutoka CDC ambazo
ndizo zilizotusaidia kuweka maabara ya kisasa hapa kisiwani Pemba ambayo
itaweza kuchunguza magonjwa yote’’, alifahamisha Sando.
Maabara hiyo iliyojengwa kwa ufadhili wa CDC umegharimu kiasi
cha shilingi bilioni 3.5.
MWISHO.
Comments
Post a Comment