CFP YAANZA KUMALIZA KIU YA UKOSEFU WA MAJI KWA WAKULIMA KILIMO MSITU PEMBA, FATMA BAKAR AANZA KUUAGA UMASKINI
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@
….nilianza na shamba moja la ekari moja, na sasa nimeongeza mawaili yenye ukubwa na nusu nusu eka kila moja, ndio maneno ya mkulima kilimo msitu Fatma Bakari wa Chato.
Chato hiyo, sio ile ya Mkoani Dodoma Tanzania bara, hapana ipo kijiji cha Gombeume, shehia ya Mchanga mdogo wilaya ya Wete Pemba.
Hapo ndio anapoishi mkulima huyo, ambae kwa sasa anajiita mtaalamu wa kilimo msitu, ama kilimo mchanganyiko wa miti ya biashara na chakula.
ALIANZAJE KILIMO MSITU
Alianza kuwataja Jumuiya ya Uhifadhi yaw a Misutu Pemba ‘CFP’ na Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar, kwamba ndio waliomzua yeye na sasa kuwa mkulima mtaalam wa kilimo msitu.
Alijifunza nini maana ya kilimo hicho, kinalimwaje na faida zake za muda mfupi na mrefu, katika maisha ya kila siku.
Baada ya mafunzo, huku na muume, akiwa ameshafariki, ndipo mwaka 2024 mwezi wa August, alipoanza kilimo hicho ndani ya shamba la urithi la aliyekuwa muume wake.
Hapo akiwa na utaalamu, aliza kupanda minansi 1,000, miembe ya mbegu ndogo sita, mipapai sita, mitondoo 24 na mashina 30 ya muhogo.
‘’Nilianza kulilea shamba hilo, katika mazingira ya ukosefu wa huduma ya maji, jua likawa linakausha miti yangu, na nilianza kukata tamaa,’’anakumbuka.
Kumbe sio jua kali pekee, kwa wakati huo lililomkatisha tamaa, bali wizi, wafugaji kumlishia na baadhi ya miti ya biashara na matunda kufa, nazo zilimkwaza.
Fatma ambae anaumri wa miaka 49, anasema siku zilisonga hadi alipoanza kuvuna ndizi 20 na muhogo, na kujiingiizia shilingi 100,000.
Mkulima huyu sasa akawa kila baada ya muda anavuna ndizi, muhogo na mananasi na alianza kujiwekea akiba taratibu, kwa ajili ya kauendeleza ujenzi wa nyumba ya kisasa.
‘’Nilipoanza kuvuna mazazo kama ndizi na nanasi, hata watoto wangu wanne mayataima, niliwamudu kuwanunulia vifaa kamili vya skuli na kutumia shilingi 60,000,’’anasimulia.
Mbinu za kuongeza mashamba mingine, alikuwa anaranda nazo kichwani, maana utamu wa mavuno kwa shamba lake la kwanza lenye ekari moja, ulimuiingia gegoni.
Aliafanikiwa kuanzisha shamba jingine mwishoni mwa mwaka jana, yote mawili kila moja, likiwa na nusu ekari, na sasa kuwa na ekari mbili, kwa mashamba yake matatu.
Kwenye mashamba hayo, kama nyongeza amepanda minanasi 2,000, mitondoo 1,000, migomba 80 ikiwemo ya mkono mmoja, michungwa 30 na mihogo mashina 30.
Hapa mkulima huyo, anasema sasa ni mwendo wa kuukimbia umaskini kwa vitendo, kwani ameshajiwekea malengo, pindi akifanikiwa kuvuna kwa wakati.
MATARAJIO YAKE
Hapa kwa hesabu za madole, mkulia huyo atajiingizia shilingi milioni 22,070,000 ikiwa katika kilimo hicho, kwanza atavuna kwa wakati na hatokumbana na changamoto yoyote kwenye kilimo chake mchanganyiko.
Maana kwenye mitondo yake, 1,000 anasema anatarajia kuuza mfano wa boriti ambapo kila moja ni shilingi kati 20,000 na kujiingizia shilingi milioni 20, ikiwa haitapambana na changamoto, ikiwemo wizi.
Kwenye minanasi, anasema matarajio yake ni kujiingizia shilingi mlioni 1, kwa kuyauza manansi 1,000, kwa bei ya shilingi 1,000 kila mmoja.
Kwa sasa akiendelea kuvuna ndani ya shamba lake la awali, ameshaanza ujenzi wa nyumba ya kisasa yenye vyumba vinne, kwa ajili ya familia yake.
‘’Ijapokuwa sio fedha zote zinatokana na manufaa ya kilimo msitu, lakini wastani wa shilingi milioni 5 ni mkusanyiko wa fedha za kilimo hicho,’’anabainisha.
Nyumba yake hiyo, ameshatumia zaidi ya shilingi milioni 12, na imefikia hatua ya kuezeka akikwama hapo, licha ya kuwa na mapau kwa kazi hiyo.
CHANGAMOTO ZA KILIMO CHAKE
Moja anasema ni ukosefu wa huduma ya maji ya kumwagilia, ambayo humpa kigugumizi ya kupata mavuno aliyoyakusudia, wakati anaipanda.
Eneo jingine anasema ni wizi wa kupindukia, kuanzia mazao kama mananasi, mihogo na ndizi huku wakiendelea kuwalalamikia wafugaji kwa daharau zao.
‘’Naandamwa na ukosefu wa huduma ya maji, maana kipindi cha jua ipo miti husinyaa, wizi na wafugaji kwa hakika wananikatisha tamaa,’’anasema.
Mkulima huyo anasema, walishawahi kumlalamikia Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo na kuwaahidi, ingawa sasa imeshapita miezi minne, bila ya mafanikio.
‘’Tulisikia hata Mbunge wetu wa Kojani, alidai kukisikia kilio chetu na kuahidi kutusaidia, ingawa hadi sasa tunaendelea kuwasubiria,’’anaeleza.
MALENGO YAKE YA BAADAE
Mkulima huyo anasema, anatarajia kuhakikisha amemaliza ujenzi wa nyumba yake kikamilifu, ili kuhakikisha anaishi na familia kwa furaha.
Jingine anatarajia, ikiwa kilimo hicho kitakwenda bila ya changamoto za kumrejesha nyuma, ni kuwaajiri wanawake wenzake, iwe kwenye upaliliajia na hata uvunaji.
WANAOMFAHAMU MKULIMA HUYO
Asiya Abeid Salum wa Kiuyu, anasema mkulima huyo amekuwa mfano kwao, kwa kule kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo waliopewa na ‘CFP’ kwa kushirikiana na TAMWA.
Hidaya Khatib Hamad mkulima wa kilimo msitu Mchangamdogo, anasema wamekuwa wakijifunza mingi kupitia mkulima huyo, ikiwemo kutokata tamaa.
Anaeleza kuwa, wakati anaaza waliona kama vile amekosea njia ya kusaka maisha, ingawa kwa sasa baada ya miti yake ya biashara kunawiri, wanaomuona ni mtu anaeuchungulia utajiri miaka michache ijayo.
Kombo Khatib Bakari mkulima kilimo mseto shehia ya Mjini kiuyu, anakiri kilimo hicho kimeanza kumuinua mkulima huyo kiuchumi taratibu.
‘’Kwa sasa ni wanawake wachache hapa kijijini, ambao wameanzisha ujenzi kwa nguvu zao, lakini Fatma ameweza akisaidiwa na fedha anayoipata kwenye kilimo msitu,’’anasema.
VIONGOZI WA SERIKALI
Afisa Mdhamini wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Idrissa Hassan Abdulla, anasema kilimo msitu kitawapa faida kubwa wanawake, kwani kitaifanya ardhi kuwa na rutba na kupatikana mazao kwa wingi.
‘’Unapolima kilimo mchanganyiko kutasaidia kupatikana kwa mvua, na kusaidia kupatikana kwa mazao kwa wingi,’’anaeleza.
Kama wizara wamekua wakitoa elimu kwa vikundi mbalimbali ya utunzaji mazingira, ili kuona wanawake wanapiga hatua kupitia kilimo hicho.
Kuhusu ahadi ya wizara juu ya huduma ya maji, alisema ilitolewa na uongozi wa CFP mbele ya wakulima hao, wakati Waziri alipowatembelea na kulalamikia.
‘’Ni kweli mwanzoni mwa mwaka huu, Waziri wa wizara hii alifika Mchanga mdogo, na wakulima waliomba kupatiwa huduma ya maji, kupitia CFP na sio ahadi ya wizara moja kw amoja,’’anafafanua.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mgeni Khatib Yahya, amasema, kilimo msitu kitawainua kwa kiasi kikubwa wanawake kiuchumi, kwani watapata mazao ambayo yatawasaidia katika familia zao.
‘’Ukilima tambarare utapata mboga, ukipanda miembe utavuna embe utauza utapata pesa za kununua mahitaji mingine ya nyumbani,’’anafahamisha.
WANAHARAKATI
Juma Bakar Alawi mdau wa mazingira, anasema wanawake ndio wathirika wakubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo lazima mkazo wa kuwezeshwa uwekwe.
Akaleza kuwa, kupitia mradi huo wa uhifadhi mazingira utawasaidia, kwanza kujikwamua na umasikini sambamba uhifadhi wa mazingira.
‘’Kwakweli jambo wanalolifanya wenzezetu wa Jumuiya ya uhifadhi wa misitu Pemba ‘CFP’ kwa kushirikiana na wenzao wa kimataifa ‘CFI’ la kuleta mradi huu wa mabadiliko ya tabianchi ni jambo jema,’’anafafanua.
Rehema Abrahman Alawi ni Afisa misitu kutoka CFP, anasema mradi wao umelenga zaidi kwa wanawake, kwani ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi.
Wamekuwa wakiwapatia elimu pamoja na miche, ili waweze kulima kilimo msitu, kwa ajili ya kujiinua kiuchumi.
‘’Unapomwambia mama apande miti ya misitu katika shamba lake, atajipatia mahitaji muhimu kama vile kuni, miti ya kujengea, na kufahamu athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi,’’anafafanua.
Mkurugenzi wa ‘CFP’ Pemba Mbarouk Mussa Omar anasema, endapo hakutochukuliwa jitihada za makusudi, kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu ya utunzaji wa mazingira, itasababisha baadhi ya vijiji kuhamwa kutokana na maji ya bahari kupanda juu.
KAULI YA CFP KUHUSU HUDUMA YA MAJI YA UMWAGILIAJI
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Misitu Pemba ‘CFP’ Mbaroku Mussa Omar, anasema wameanza na uchimbaji wa kisima, eneo la…kwa ajili ya wakulima hao.
Anasema visima hivyo, vitakuwa vinane, kwa awamu ya kwanza, vikichimbwa kwenye eneo la mradi wa shehia nane, ambapo Unguja na Pemba kila kisiwa ni shehia nne.
Visima hivyo, kwa awamu ya kwanza kitachimbwa kimoja kimoja kila shehia, na baadae vitachimbwa vitatu vitatu, ili kuwanufaisha wakulima wa kilimo msitu.
‘’Kwa sasa tumeanza na uchimbaji eneo la Kiuyu Minungwini, na pale tumeshajenga mnara wa mita nne, kwa ajili ya matenki manne yenye ujazo wa lita 5000 kila moja kwa ajili ya wakulima hao wa maeneo ya karibu,’’anasema.
Anafafanua kuwa, shehia nyingine za Mchanga mdogo, Kambini, Chwale kwa Pemba na Uzi, Ng’ambwa, Unguja Ukuu na Bungi kwa Unguja.
‘’Katika uchimbaji hatokwenda moja kwa moja, kila tunapomaliza kimoja, tunaangalia changamoto, faida ya kujifunza kabla ya kwenda shehia nyingine,’’anafafanua.
Hapa anasifia taasisi za Mamlaka ya Maji Zanzibar ‘ZAWA’ Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji na Shirika la Umeme Zanzibar ‘ZECO’ kwa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hilo.
Mwisho

Comments
Post a Comment