BAKARI KHAMIS NA MOZA SHAABAN, PEMBA
MAKAMu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT) Zainab Khamis Shomari, amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi katika
zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbali mbali za uongozi majimboni.
Aliyasema hayo ofisi ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya Mkoa
iliyopo Chake chake kisiwani Pemba, wakati akizungumza na waandishi wa habari
kuelekea zoezi la uchukuaji wa fomu za lililoanza janaJuni 28.
Alisema ni vyema wanawake kujitokeza kwa wingi katika zoezi
hilo, kutokana na kuwepo kwa mazingira rafiki yanayowawezesha, kushiriki zoezi
hilo bila kikwazo chochote.
Alisema ushiriki wa wanawake katika kugombea nafasi za
uongozi ni miongoni mwa matakwa ya ilani ya Chama cha Mapinduzi ‘CCM’, ambacho
kipo madarakani, ambayo imeeleza kipaumbelechake cha uwepo wa wawakilishi
wanawake kwa asilimia 50 katika vyombo vya kutunga sheria.
Alieleza kwamba Umoja wa Wanawake Tanzania, umekua ukifanya
jitihada mbali mbali katika kulitimiza takwa hilo, ikiwemo kufanya hamasa kwa
wanawake kugombea nafasi hizo kwa kuwajengea uwezo na kuwaungamkono.
"Sisi ‘UWT’ tumekua tukifanya jitihada mbali mbali katika
kuhamasisha wanawake kushiriki katika kugombea nafasi za uongozi, pamoja na
kuwaungamkono wale waliohamasika ili tupate kwa vitendo ile asilimia 50 kwa 50,
tunayoitaka ya wawakilishi wanawake,"alieleza.
Alisema kwasasa wanawake wamekua wakifanya vizuri kiungozi,
pale wanapopata nafasi mbali mbali ya kutumikia taifa, kutokana na uwezo wa
kisaikolojia walionao.
Aliongeza kua kwa mara ya kwanza, Tanzania inatarajia
kuandika historia ya kua na Raisi mwanamke, atakaepatikana kwa kupigiwa kura na
wananchi, hivyo ni vyema kwa wanawake wingine, kuungamkono azimio hilo kwa
kujitokeza katika kuchukua fomu za kugombea.
Alisema UWT imejipanga kutoa ushirikiano kwa wanawake katika
kugombea nafasi hizo, huku akiwaomba wanaume kutoa ushirikiano wa kutosha kwa
wanawake, kwa kuwashajiisha na kuwapa moyo.
" Tunataka kuuthibitishia umma kwamba, dhana ya adui wa
mwanamke ni mwanamke mwenzake sio sahihi, hivyo sisi UWT tutahakikisha
tunawaungamkono wanawake watakaojitokeza kuchukua fomu za kugombea na wanaume tunaomba
muunge mkono hili,"alifafanua.
Hata hivyo Makamu huyo Mwenyekiti wa UWT, aliwataka wanawake
bila kujali itikadi za vyama vyao, waache kuwa maadui kwa wanawake wenzao.
Wakati huo huo, amevitaka vyombo vya habari kutumia vizuri
kalamu zao, juu ya kushajiisha wananchi kuhusu
umuhimu wa kutunza amani iliopo nchini.
Awali akizungumza hivi karibuni, kiongozi wa mbio za mwenge
wa uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi, amewakumbusha wananchi, kuwachagua viongozi
wenye nia ya kuwaletea maendeleo.
Zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbali mbali za
uongozi kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, limeanza jana likitarajiwa kumalizika
Julai 2, mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni.
MWISHO
Comments
Post a Comment