NA MARYAM NASSOR, ZANZIBAR
MAHKAMA maalum ya kupinga makosa ya udhalilishaji mkoa wa Mahonda Unguja, imemuhukumu kijana Sharif Juma Hamad (33) maarufu ‘MAYELE’wa Mzambarau mbata Unguja, kutumikia kifungo cha miaka 14, kwa kukutwa na hatia ya makosa mawili ya udhalilishaji.
Akisomewa hukumu hiyo, Hakimu Luciano Makoe Nyengo, alisema kuwa mshitakiwa huyo amekutwa na hatia hiyo, baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliyoletwa na upande wa Mashtaka, ulioongozwa na Mwendesha Mashtaka Hariri Yeshau Ali, na vielelezo vilivyowasilishwa.
Hakimu Luciano, alisema kuwa Mshitakiwa huyo anatiwa hatiani kwa makosa mawili aliyoshitakiwa likiwmo la kulawiti mtoto wa kiume mwenye miaka 12, kwa kosa hilo atatumikia kifungo cha maiaka 14 chuo cha mafunzo.
Kosa la pili, ni kutorosha mtoto wa kiume alie chini wa uwangalizi wa wazazi wake, ambapo ni kinyume na kifungu cha 113 (1) (b) cha sheria nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar na kosa hilo atatumikia kifungo cha miaka 10.
Aidha, Hakimu Luciano alisema kuwa, adhabu zote hizo ziende sambamba, hivyo mshitakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka 14 chuo cha mafunzo.
Kesi hiyo nambari, 18 ilifunguliwa tarehe Juni 11, mwaka huu na kusikilizwa mashahidi sita na upande wa utetezi kulikuwa na shahidi mmoja ambae ni mshtakiwa mwenyewe.
Awali mshtakiwa huyo, alishtakiwa kwa makosa mawili kosa la kwanza likiwa ni kulawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12 kinyume na kifungu cha 115 (1) vya sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
Kosa la pili ni kumtorosha mtoto wa kiume, aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake, kutoka nyumbani kwao Mgambo na kumpeleka nyumbani kwake, eneo hilo la Mgambo bila ya ridhaa ya wazazi wake.
Ambapo kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 113 (1) (b) cha sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.
MWISHO
Comments
Post a Comment