NA HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@
MPIRA wa kikapu ‘basketball’ ni aina
ya mchezo unaochezwa sehemu nyingi duniani.
Kwani kama ilivyo michezo mingine, nao huimarisha afya, huleta ajira, huondosha
ubaguzi, na kuunganisha watu wa aina mbalimbali.
Mchezo huu
ni wa pili kwa umaarufu, baada ya mpira wa miguu kwa kupendwa na mashabiki wa
michezo nchini, ambao wengi walicheza skulini na kupata wafuasi wengi.
Kwa mujibu
wa umoja wa Mataifa, mchezo huu ulianzishwa na Mwalimu James Naismith, kwenye
chuo cha Springfield College huko, Massachusetts mwaka 1891.
Alibuni
mchezo huu kwa ajili ya wanafunzi wake, ili wapate mazoezi wakati wa kipupwe
waliposhindwa kucheza nje, ambapo kwa mara ya kwanza, ulichezwa Disemba 21
mwaka huo huo 1891 nchini Berlin.
Mpira wa
kikapu, ulienea haraka ndani na nje ya vyuo vya Marekani, katika karne ya 20, ambapo
mwaka 1936 mchezo huu ulikubaliwa kwenye michezo ya Olimpiki.
Shirikisho
la mpira wa kikapu duniani ‘FIBA’ na chombo cha usimamizi wa mpira huo duniani,
linakadiria kuwa takriban watu milioni 450 duniani, wanacheza mchezo huo.
Kwa vile
mchezo huu uliibuliwa kwa ajili ya wanafunzi, skuli ya Sekondari ya Uweleni
Mkoani Pemba, nayo imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha lengo linatimia.
Skuli hiyo
yenye timu mbili ya wanawake na wanaume, imekuwa ikifanya vizuri na imeshachukuwa
ushindi mara nne mfululizo, katika sherehe za elimu bila malipo Zanzibar, kwa
wanaume.
Ingawa wanawake
wanashikilia ushindi kwa Pemba, na kwenye fainali huishia ushindi wa pili,
ingawa kwa hali zao si haba.
Licha ya timu
ya wanawake ya ‘basketball’ skuli ya Uweleni kufanya vyema, bado inakabiliwa na
changamoto kubwa ya ukosefu wa uwanja.
Akizungumza
na makala haya, kocha wa basketball wa timu ya wanawake wa skuli ya sekondari
ya Uweleni, Mohamed Salim Khamis (Gabs) anasema, kutokuwa na uwanja maalum kwa
wanafunzi wa kike, hasa katika hatuwa za awali.
Uwanja mmoja
ambao wanacheza wanaume, ndio huo huo wanaochezewa na wanawake, huku ukiwa sehemu
ya uwazi ni jambo linalowapelekea watoto wa kike kujiskia aibu.
“Nna uhakika
kama tutapata uwanja wa kufanyia mazoezi uliostara kwa watoto wa kike,
tutachukuwa nafasi ya kwanza kwenye fainali, bila wasiwasi kama tunavyochukuwa
kwa wanaume,”anasema kocha.
Akizungumzia
vipaji vya michezo kwa watoto wa kike skulini hapo vipo hasa katika mchezo huo
wa basketball ila linalowarejesha nyuma ni uwanja pekee.
Anaelezea
kutokuwa na uwanja maalum wa watoto wakike ndio kunakowatia hofu jamii na
wazazi kushiriki watoto wao katika michezo na kusema ni uhuni.
Mwalimu
anaeshughulikia michezo Skuli ya sekondari Uweleni Abdulla Ali Abdalla anasema
asilimia kubwa ya watoto wa kike skulini hapo wanapenda michezo hasa wa
basketball, ila wazazi hawaridhii kutokana na mchanganyiko wakati wa ufanyaji
wa mazoezi.
JUHUDI ZA SKULI KUENDELEZA BASKETBALL
KWA WANAWAKE
Mwalim Abdul
anasema ni pamoja na kuwashajihisha wanafunzi wa kike kushiriki katika michezo,
hatimae kuwa na utayari wa wanafunzi wenyewe kutokana na mapenzi ya mchezo huo.
Nyingine ni
kuwapongeza wanafunzi wa michezo kila mwaka na kuwapa zawadi waliofanya vizuri
zaidi, pamoja na kuzungumza na wazazi kuhusiana na umuhimu wa michezo kwa
watoto wa kike na jinsi unavyowadhibiti na vishawishi vibaya.
WANAFUNZI WA KIKE
Maimuna Fatawi
Khamis anasema kushiriki kwake katika mchezo huo kumemletea faida ikiwemo ya
kuimarisha afya, kutembea sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi pamoja na
kupata zawadi.
“Mimi nishakwenda
baadhi ya mikoa ya Tanzania bara, hadi nimefika nchi ya Uganda, kupitia michezo
hujiuliza kwa hali ya kawaida ningefikaje,”anasema
kwa bashasha.
Fatma Masoud
Kombo, anasema kwa vile michezo ni ajira baada ya kumaliza skuli, ataweza
kujiajiri kupitia michezo bila ya kusubiria serikalini.
“Pamoja na
maneno mengi nnayoambiwa kama michezo kwa wanawake haina tija, haisaidii lakini
sikubali kwani wapo wanawake wengi ‘wamewini’ kupitia michezo,”anasema.
Nasra Ali
Sheha anasema, licha ya kutokuwa na uwanja wa kufanyia mazoezi ya mchezo
basketball, lakini anaendelea na ataendelea kufanya vizuri.
“Wapo
wanafunzi wenzetu wanatuonea choyo na wanataka kuingia katika michezo, ingawa wanakatazwa
kwao wanaambiwa michezo ni uhuni,”anasema bila hofu.
MIKAKATI YA SKULI
Msaidizi Mwalimu
mkuu skuli ya sekondari Uweleni Khamis Mohamed Ussi, anasema baada ya kukaa
pamoja na uongozi wa walimu wa michezo, wameamuwa kutengeneza goli moja nyuma ya
skuli yao, ili wanafunzi wa kike wafanye mazoezi.
Anasema, ijapokuwa
goli hilo ni la kienyeje ‘local post’ lakini linawasaidia, kiunyonge hasa
ukianagalia mchezo huo unahitajika kuchezwa kwenye sakafu, ila wao wanacheza
kwenye vumbi.
‘’Ilitubidi
tuunde, tuwaze maarifa hayo, kwani bila ya hivyo ni shida kwa watoto wa kike
kufanya mazoezi pamoja na wanaume,”alisema.
WAZAZI
Subira
Mohamed, anasema mwanzo hakuwa tayari mtoto wake wa kike kuingia katika michezo,
ingawa baada ya kuelimishwa na walimu kuhusu faida yake, alikubali.
“Kilichonifanya
nikatae mwanangu kuingia michezoni ni uchezaji wa pamoja, kati yao na wale wa
kiume, jambo hilo si zuri kiutamaduni,”anasema.
Hashim Abdalla
Ali, lazima tukatae wazazi maana kama wameamuwa kuchezesha mpira huo kwa watoto
wa kike, wangewaekewa uwanja wao mbali, usiotumiwa na wanaume.
Said Omar
Ali, anasema ni jukumula serikali kupitia wizara husika, ni kujenga viwanja vya
michezo kwa watoto wa kike ili kufanyia mazoezi katika skuli ya Uweleni,
linazingatiwa.
“Tulikuwa
tushakataa watoto wa kike wasiingie katika michezo, lakini baada ya kuitwa na waalimu
na wakatupa faida ya michezo kwa vijana wetu wakike, nikakubali,”anasema.
TAMWA ZANZIBAR
Afisa mradi
wa kukuza usawa wa kijinsia na ujumuishi kwenye michezo Khairat Haji, anasema
baada ya kuona watoto wa kike wako nyuma katika sula la michezo.
Ndipo chama
cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar kupitia mradi wa
michezo kwa maendeleo, imeona ipo haja ya kushirikiana na vyombo vya habari
kuibuwa changamoto za aina hiyo.
Anasema, ni
kweli watoto wa kike wako nyuma katika ushiriki wa michezo, na kuwataka
waandishi wa habari kuhakikisha, wanatumia kalamu zao kulisemea jambo hilo, ili
kuondokana na mawazo finyu.
Anasema
lengo la mradi wa michezo kwa maendeleo unaodhaminiwa na shirika la maendeleo
la kimataifa la Ujerumani, ambao unatekelezwa na jumuiya ya wanasheria wanawake
Zanzibar ‘ZAFELA’, kituo cha majadiliano kwa vijana ‘CYD’ ni kuhakikisha
wanawake wanashiriki katika michezo, kwa hali ya kuridhisha.
‘Kwa vile
kila mtu anayo haki ya kushiriki michezo, kwa nini wanawake wabakie nyuma na
tutahakikisha usawa wa kijinsia unapatikana katika michezo,’’alisema.
WIZARA HUSIKA
Mkuu wa divisheni
na utamaduni kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mzee Ali Abdalla,
anasema ni vyema walimu wakuu wachukuwe
nafasi zao, kuweza kujenga viwanja vidogo vidogo, ili watoto wa kike
wasikatishe michezo yao.
Anasema watoto
wakipata uwanja wa karibu, wataweza kuvutiwa zaidi, kwani akili ya mtoto bora
ni ile inayojengwa na kiwiliwili bora, ambapo ni kupitia michezo ni sehemu moja
wapo.
KANUNI ZA MCHEZO HUO
Shabaha ya
mchezo ni kushinda vikapu vingi kuliko timu nyingine, na mpira unaotumiwa
kimataifa ni mpira wa ngozi au ‘mata sintetiki’, wenye kipenyo cha milimita 749
hadi 780 na uzito wa gramu 567 hadi 650.
Uwanja huwa
na vipimo vya mita 28 kwa 15 ambapo wakati wa mchezo huwa kuna marefa 2-3
uwanjani wakati kando ya uwanja hukaa waamuzi wengine wanaoshika wakati na
miniti za magoli na makosa.
MWISHO
Comments
Post a Comment