IMEANDIKWA NA
ZUHURA JUMA, PEMBA
WAZIRI
wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Shamata Shaame Khamis
amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha inasimamia vyema
utekelezaji wa mradi wa Kijani (SASA) Pemba utakaoimarisha ustahamilivu wa
mazingira, ambao unalenga kuleta mageuzi ya upatikanaji wa huduma bora nchini.
Alisema kuwa, mradi huo utasaidia
upatikanaji wa maji safi na salama, kufanya ukarabati wa maskuli 19 na
ukarabati wa vituo vya afya kumi (10), kuwawezesha wajasiriamali wadogo wadogo kwa
kuwapatia mafunzo na mikopo nafuu, kuwasaidia akinamama wanaolima mwani pamoja
na usimamizi wa usafi wa mazingira katika miji.
Akizindua mradi huo katika Uwanja wa
michezo Madungu Chake Chake Waziri huyo alisema kuwa, ni vyema mradi wa Kijani (Green
and Smart Cities Programe) utekelezwe kwa haraka, ili wananchi wanufaike kwani
ni muhimu sana kwao.
‘’Tuhakikishe mradi huu tunautekeleza
kwa malengo tuliyoyakusudia na Serikali inaendelea kuthamini michango ya
washirika wa maendeleo wa ndani na wa nje wakiwemo Umoja wa Ulaya (EU) na
kuahidi kushirikiana ili kufanikiwa zaidi,’’ alisema Waziri.
Alisema kuwa, EU umeshatoa misaada
mbali mbali ya utaalamu, kifedha na nyenzo tofauti katika nchi, ambapo tangu
mwaka 1975 wameshashachangia zaidi ya Euro bilioni mbili kwa maendeleo ya nchi
ya Tanzania kupitia miradi mbali mbali.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu
Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ Mikidad Mbarouk Mzee alisema,
mikataba miwili ya ruzuku kwa ajili ya mabadiliko ya mradi wa Kijani (SASA) katika
vitongoji vya miji ya Pemba vyenye jumla ya misaada ya Euro milioni 75 ambazo zitatumika
katika mradi huo unaolenga kuimarisha ustahamilivu wa miji.
‘’Tunaishukuru EU kwa msaada wa fedha
mbali mbali za uchumi wetu ikiwemo katika maeneo ya uchumi wa buluu na
mabadiliko ya hali ya hewa, udhibiti na mageuzi ya taasisi, mpango wa ukuaji wa
mitaji kwa wajasiriamali kwenye masuala ya kilimo na utawala, ukusanyaji wa
takwimu za jinsia na udhibiti wa kazi za nishati,’’ alisema Naibu huyo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba
Salama Mbarouk Khatib alisema kuwa, wamaefarajika sana kupata mradi huo na
kueleza kuwa watashirikiana na kuunga mkono jitihada hizo kwa kufanya usimamizi
na ufuatiliaji.
Mapema Mkurugenzi wa Mradi huo
Martino Vinci alisema, mradi huo unalenga kuboresha miundombinu ya mijini,
kuimarisha huduma za msingi kama vile usimamizi wa maji safi na taka na kuibua
fursa za kiuchumi kwa vijana, wanawake pamoja na biashara ndogo ndogo katika
sekta ndogo za kilimo cha mwani na kuchakata taka.
‘’Nina furaha sana ya kusherehekea
pamoja nanyi katika uzinduzi wa miradi hii na ninasisitiza kuwa dhamira yetu ya
kufikia matokeo chanya yataonekana hivi karibuni,’’ alieleza.
Mtekelezaji wa mradi huo kutoka
shirika la misaada la Ubelgiji (Enabel) Koenraad Goekint alifahamisha kuwa, mradi
huo utaboresha ufanisi wa kazi katika taasisi zenu, mazingira mnayoishi na
maisha ya familia zenu, watoto, vijana na wanawake.
‘’Katika mwaka mmoja au miwili ijayo
tunatarajia kuona skuli zikiwa na hali bora kwa watoto, jamii zikiwa na maeneo
ya umma yaliyoboreshwa, upungufu wa taka, usambazaji bora wa maji na usafi wa
mazingira,’’ alifahamisha.
Mkurugenzi wa shirika la OIKOS Mary
Birdi alifafanua ushirikiano unahitajika katika miradi inayotekelezwa, kwani
itawasaidia wananchi mbali mbali na kuboresha miundombinu.
Balozi wa EU nchini Tanzania Christine Grau alisema kuwa, hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi wa Pemba itakayowasaidia kuwa na mazingira bora na hewa ya kuvutia.
Mradi huo unaoendeshwa na Wizara ya
Nchi Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ chini ya
Ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), unatekelezwa katika mikoa ya Tanga Mjini,
Mwanza na kisiwani Pemba.
MWISHO.
Comments
Post a Comment