NA
HAJI NASSOR, PEMBA:::
WIZARA
ya Afya Zanzibar, imepiga marufuku kwa daktari yeyote, kumlazimisha mwananchi
kuchoma chanjo ya kinga ya Corona, na badala yake, chanjo hiyo itaendelea kuwa ya
hiari ya mtu binafsi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya
simu Januari 13, 2023, Waziri wa wizara hiyo Zanzibar, Nassor Ahmed Mazurui, alisema hakuna mtu
yeyote, mwenye mamlaka ya kumlazimisha mwengine, kuchanja chanjo hiyo.
Alisema, bado kila mtu yuko huru ama kuamua kuchanja
au kukataa kufanya hivyo, kwani suala la kinga ni la hiari ya mtu binafsi, na
sio kumlazimisha kama ilivyozuka kwa baadhi ya madaktari kulalamikiwa.
Alisema bado msimamo wa wizara ya Afya, ni kuona
chanjo hiyo inakuwa ya hiari, na wala hukuna daktari yeyote wala mfanyakazi wa
wizara, mwenye nguvu na mamlaka ya kumlazimisha mtu kuchanja.
‘’Kama kuna daktari anawalazimisha watu kuchanja
chanjo ya Corona, hilo ni kosa kisheria, maana bado msimamo wa serikali kuwa
chanjo hiyo, ni hiari,’’alisema.
Hata hivyo Waziri huyo wa Afya wa Zanzibar Nassor
Ahmed Mazurui, alisema atafuatilia kwa karibu katika hospitali zote za Unguja
na Pemba, ili kujua kuna madaktari wamekuwa wakiwalazimisha wananchi kuchanja.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema, wanachopaswa
kufanya madaktari na wahudumu wengine wa afya, ni kuwaelimisha wananchi, juu ya
faida za chanjo hiyo.
‘’Lakini pia wanaweza kuwaeleza wananchi athari za
mtu asiyechanja, aina za chanjo zilizokubaliwa, ipi unachoma mara moja na ipi mara
mbili, lakini sio kuwalazimisha,’’alisema.
Hayo yamekuja hivi karibuni, baada ya baadhi ya wananchi
kisiwani Pemba, kulalamikia tabia iliyozushwa, na baadhi ya madaktari,
kuwalazimisha kuchoma chanjo ya Corona.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa
masharti ya kutochapishwa majina yao walisema, kwa wanaokataa wamekuwa wakielezwa
kuwa, wanaweza kukosa matibabu pindi watakapokwenda hospitalini.
Walisema wamekuwa, wakilalamika, kutokana na amri
ya madaktari hao, ambao baadhi yao wamekuwa wakipita majumbani na kuwalazimisha
kwenda kuchanja.
Wananchi wa shehia za Mwambe, Kengeja, Msingini
Chake chake, Kwale, Ole, Micheweni, Wawi, Kiuyu Mbuyuni na Mtambwe wamesema,
wamelazimishwa kuchanjwa, chanjo ya corona.
Vijana Omar Haji Khamis na mwenzake Nadia Issa Ali
wa Kengeja, waliotaka majina yao yachapishwe, walisema juzi waliporudi kwenye
safari zao, walikuta ujumbe unaowataka kufika hospitali kupata chanjo.
‘’Niliposema kuwa mimi siendi, tuliambiwa na
waliotupa salamu, kuwa hata matatibabu mengine huwenda nayo
tukayakosa,’’alisema Omar.
Kadika Mkubwa Mashiri na mwenzake Assa Khamis
Mohamed wa Mtambwe walisema, wao waliwashuhudia madaktari wakipita nyumba hadi
nyumba, sio tu kuwashawishi bali ni kuwalazimisha.
Akizungumza hivi karibuni, Afisa Mdhamini wizara ya
Afya Pemba Khamis Bilali Ali, amerejea kauli yake, ya kuwaomba wananchi kupata
chanjo hiyo, ili kujikinga na corona.
‘’Corona bado ipo, na zipo njia kadhaa za kujikinga
na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na chanjo, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka
kila baada ya muda na kuacha mikusanyiko isiyo ya msingi,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Afisa Mdhamini huyo, alisema
ambao hawastahiki kupata chanjo hiyo ni watoto waliochini ya miaka umri wa 18
na wale ambao sindano zinawadhuru pekee.
Mwezi Machi 11, 2020 Shirika la Afya Ulimwengini ‘WHO’
itangaaza kuwa ugonjwa Corona kuwa ni janga, la taifa hii ilitokana na kasi
yake ya kuua na kusambaa.
Kisha WHO ikiwashauri wananchi kujiinga kwa kupata
chanjo ambayo ni dawa ya kibaologia iliyokubaliwa na wataalamu wa afya, kwa
lengo la kukinga, kujenga, ulinzi wa mwili na ugonjwa fulani husika kwa mujibu
wa aina chanjo.
Hivi karibuni kituo cha Ulaya cha kudhibiti na kuzuwia
magonjwa (ECDC) na ‘WHO’ wanakadiria kuwa watu 470,000 wenye umri wa zaidi ya
miaka 60, wamenusurika kifo katika nchi 33 kote barani Ulaya, tangu chanjo hiyo
ilipoanza kutolewa.
Mwisho
Comments
Post a Comment