NA HAJI NASSOR, PEMBA::
WAZAZI na walezi kisiwani Pemba, wamekumbushwa kuwa, sio haki
watoto wenye ulemavu kukoseshwa haki zao za msingi, kama elimu na kuchanganyika
na wenzao, kwa sababu ya ulemavu walionao.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Idara ya watu wenye
ulemavu kisiwani humo, Mashavu Juma Mabrouk, wakati akizungumza na wazazi,
walezi na wanafunzi wa madrssa za Umi ya Vikunguni na ile ya Annajah ya
Machomane Chake chake, kwenye ziara iliyoandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada
wa Kisheria Zanzibar.
Alisema, bado baadhi ya wazazi na walezi, wamekuwa
wakijenga dhana kuwa, mtoto mwenye ulemavu anahiari ya kumpatia elimu, na
asiyekuwa na ulemavu ndio mwenye haki kamili.
Alieleza kuwa, dhana hiyo isiwapitikie wazazi hata
siku moja katika maisha yao, na badala yake wawe na haki sawa watoto wenye
ulemavu na wengine, ili kutimiza matakwa ya kisheria.
Mratibu huyo alisema, suala la uwep wa changamoto
kwenye sekta ya elimu kama vile uhaba wa vifaa visaidizi kwa watoto wenye
ulemavu, isiwe sababu ya kuwafungia ndani na kuwakosesha haki hiyo.
Alieleza kuwa, sera ya elimu inataka watoto wote
wenye umri wa kupata elimu, wawepo kwenye mfumo wa elimu, ili zinapotokea
changamoto, ziwakuwate wakiwa madarasani.
‘’Ipo tabia ya baadhi ya wazazi, wakiona wamepata
mtoto mwenye ulemavu, ameshapata kichaka cha kumtopeleka skuli au madrassa,
akifikiria kuwa hawezi na atachekwa na wenzake, hilo sio sahihi,’’alieleza.
Hata hivyo amewataka wanafunzi waliomo kwenye mfumo
wa elimu, kuendelea kuwashawishi wazazi na walezi wao, ikiwa kuna wenzao wenye
ulemavu wamefungiwa ndani, nao waandamane nao kutafua elimu.
Katika hatua nyingine Mratibu huyo wa Idara ya watu
wenye kisiwani Pemba Mashavu Juma Mabrouk, ameitaka jamii kuendelea kupanga
mikakati madhubuti, ili kuwalinda na udhalilisha watoto wenye ulemavu.
‘’Watoto wote wanakabiliwa na hali mbaya ya
kufanyiwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji, ingawa sasa wabakaji wamekua
wakikimbilia zaidi kwa watoto wenye ulemavu, wakidhani hawawezi kueleza
chochote mahakamani,’’alieleza.
Hata hivyo alisema wazo la Idara ya Katiba na Msaada
wa Kisheria Zanzibar, kuandaa ziara ya kuwapitia wanafunzi, ili kuzungumza nao
juu ya namna ya kukabiliana na matendi hayo, ni nzuri.
Kwa upande
wake Mwakilishi wa Idara ya
Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar ofisi ya Pemba Mohamed Massoud Said, alisema,
moja ya dalili ya mtu anaetaka kumdhalilisha mtoto, huanza kwa kumuonesha picha
za ngono, kumnunulia zawadi, kumpa fedha, na kuendelea kwa maneno ya ushawishi
juu ya udhalilishaji.
Hata
hivyo, amewataka wanafunzi, waalimu, wazazi na walezi kuitumia Idara hiyo, kwa
kutoa taarifa za matukio hayo, au uwepo wa watu wanaojaribu, kuzifanyia sulhu
kesi za udhalilishaji.
Mkurugenzi
wa Jumuiya wa wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor
Bilali Ali, amesema kama jamii haikushirikiana katika ulinzi wa watoto,
kusitarajiwe matendo hayo kupungua.
Akizungumza
kwenye ziara hiyo, Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi
la Pemba Safia Saleh Sultan, aliwataka wanafunzi hao, kutomruhusu mtu yeyote,
kuuchezea mwili wake.
‘’Sehemu
zako za siri ni mali yako, usimuonesha mtu mwengine wala usikubali kuguswa kama
hakuna sababu inayokubalika, maana huo ndio mwanzo, wa udhalilishaji
unapoanzia,’’alieleza.
Hata
hivyo amesema, lazima ulinzi kwa watu wenye ulemavu uimarishwe mara mbili, ili
wawe huru na matendao ya udhalilishaji wa kijinsia.
Mwalimu
mkuu wa Almadra-ssatul-Annajah Imani Ali Mohamed, alisema ziara hiyo kwao ni
faraja, katika kuwakumbusha wanafunzi juu ya kujikinga na matendo hayo.
Kwa
upande wake Msaidizi mwalimu mkuu wa Almadra-ssatul-Umi ya Vikunguni Zubeda
Yussuf Mohamed, alisema bado wazazi hawajaona umuhimu, wa kushirikiana na
waalimu, katika malezi ya watoto.
Ziara
hiyo ya kutoa elimu ya kupambana na makosa ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia,
ni muendelezo ya mikakati ya Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, katika
kuhakikisha kundi la wanawake na watoto, linaishi pasi na ukatili.
Ripoti ya Jeshi la Polisi Zanzibar, inaonesha, kwa mwaka 2021, kulikuwa na matendo 1,222 ya wanawake na watoto kudhalilishwa Unguja na Pemba.
Aidha
ripoti nyingine ikaonesha kuwa, kulikuwa na matukio 610 ya aina hiyo, kwa
kipindi cha miezi mitatu mitatu ya mwaka 2021 na 2022.
Mwisho
Comments
Post a Comment