NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
KIJANA Gizahibu Ali Amour miaka 38 aliyekatwa miguu yote miwili, miaka mitatu
iliyopita kwa tuhma za wizi, shehia ya Pujini wilaya ya Chake chake, amepona na
kupata ulemavu wa kudumu.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi kwa njia simu, Januari 8, 2023 alisema licha ya kuwa bado yuko hai, lakini amepata ulemavu
wa kudumu na kulazimika kutembelea miguu ya bandia.
Alisema, mguu mmoja wa bandia aliununua kwa
shilingi 400,000 ambapo kwa hatua za awali alichangia na ndugu na jamaa,
marafiki na madaktari katika hospitali aliyokuwa amelazwa.
Alieleza kuwa, sasa ni mwaka mmoja, tokea atoke hospitali na kutumia miguu ya bandia, na imeanza kumbana na kuanza
kuisaidia kwa mgongo mawili.
Kijana huyo alieleza kuwa, kama
hakupata usaidizi tena, anachokiona mbele yake, ama ni kubakia nyumbani muda wote
au kutembelea magongo, kwenye safari zake ndogo ndogo.
‘’Kwani nipo nyumbani na ilikuwa
natembelea vyema miguu yangu ya bandia, lakini sasa imeshaanza kuchakaa na kama
sikupata ufadhili, itabidi nitembelee magongo,’’alieleza.
Akizungumzia kuhusu maisha yake,
alisema kwa sasa anaowatoto watano wanaomtegemea, ingawa hana mke anayemsaidia
kimaisha.
‘’Hali yangu ya maisha kwa sasa, ni ya
kubahatisha, siku zote ili nipate chakula kazi kubwa ni kuomba msaada kwa wahisani, wapita
njia na kisha ndio niwapelekee na watoto wangu,’’alieleza.
Hata hivyo alisema, tuhuma za yeye
kuwa ni mwizi na kupelekea kukatwa miguu miwili, hazikuwa za kweli, na ndio
maana hadi leo hakuna aliyemlalamikia.
Kwa upande mwengine, wapo watu 25
waliwahi kuhojiwa na Jeshi la Polisi mkoa wa kusini Pemba, kwa tuhma za
kumshambulia kijana huyo.
Ingawa hakukua na yeyote alipandishwa
mahakamani, na baada ya kuhojiwa watu hao wote, waliachiwa huru, huku kijana
huyo kwa wakti huo akiendelea kuuguaza majereha.
Mmoja kati ya wanafamilia wa kijana
huyo, ambae hakupenda jina lake lichapishwe, alisema kijana huyo baada ya
kumuuguza kwa mwaka mmoja na nusu, sasa anatembea kwa kutumia miguu ya bandia.
Alieleza kuwa, kijana huyo alionewa
kwa kudhaniwa kuwa aliiba, ingawa hadi leo, hakuna yeyote aliyeripoti kwa jeshi
la Polisi kuibiwa jambo lolote.
Alieleza kuwa, ni vyema kwa sasa,
kwa wale watuhumiwa zaidi ya 25 waliokamatwa na kuhojiwa na kisha kuachiwa,
kuona haki inatendeka, kwa vile kijana wao amepata ulemavu.
‘’Kijana Gizahibu Ali Amour miaka 38,
alikutikana pembezoni mwa barabara, akilalamikia maumivu makali, baada ya watu wasiojulikana, kutumia kitu chenye ncha kali, kumkata miguu yote,’’alieleza.
Baadae, mpatwa na jali huyo, alifikishwa hospitali ya Chakechake kwa matibabu, ingawa ilishindikana na kupelekwa hospitali ya Mkoa ya Abdalla mzee, Mkoani Pemba.
Aliyekuwa Katibu wa hospital hiyo,
Ali Omar Mbarawa, alithibitisha kumpokea majeruhiwa huyo, na kusema imeshindikana,
kuvirejesha viungo hivyo vya miguu yake.
“Ni kweli tulimpokea mjeruhiwa akitokea
hospitali ya Chakechake kwa rufaa, akiwa hali mbaya, maana viungo vyake vya
miguu viko mbali na yeye, na sio rahisi kuvirejesha tena,’’alieleza.
Aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi
mkoa wa kusini Pemba Said Omar Dadi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo,
lilitokea August 4, mwaka 2018 majira ya saa 2:00 usiku.
Hata hivyo Kaimu Kamanda huyo amekemea vikali
tabia ya wananchi kujichukulia sheria mikononi, wanapoona kuna mtu ametenda au
anania ya kufanya uhalifu katika sehemu zao.
Miezi miwili iliopita kijana mwengine
wa Pujini Abdalla Mohamed Amour ‘babu dii’ alipigwa ndani mwake na watu wasiofahamika na kusababisha kupata ulemavu wa mguu na mkono.
Kwa mujibu wa taarifa za uhalifu
zilizochapishwa na Jeshi la Polisi Tanzania mwaka 2017, imeonesha kuwa matukio
ya kujichukulia sheria mikononi, yamezidi kuongezeka nchini, ambapo katika
kipindi cha Januari hadi Disemba, 2017 watu 917 waliuawa.
Aidha taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi
Tanzania, ilieleza kuwa, idadi hiyo iliongezeka kidogo, ikilinganishwa na watu
912 waliouawa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2016, ambapo hilo ni ongezeko
la watu 5 ambao ni sawa na asilimia 0.5.
Kwa Zanzibar pekee katika kipindi
hicho cha miaka miwili, Jeshi hilo la Polisi liliripoti idadi ya watu 47
waliouwawa, huku mkoa wa mjini Magharibi ukiwa na watu 34, kusini Unguja saba.
Mkoa wa kusini Pemba, wakiripotiwa
wanne, wakati Mkoa wa kaskazini Pemba na Mkoa wa kaskazini Unguja wakiwa na
idadi sawa ya mtu mmoja mmoja, ingawa kwa mikoa ya kipolisi Konondoni iliongoza
kwa watu 189, ikifuatiwa na Temeke 128.
Mwisho
Comments
Post a Comment